Na Abdi Suleiman, Pemba
SEKTA ya michezo katika Mkoa wa Kusini Pemba, imeelezewa kuwa imepiga hatua kubwa katika kipindi cha mwezi Aprili hadi Disemba mwaka 2012.
Hayo yameelezwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa, wakati akiwasilisha ripoti ya mkoa wake, kwa Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.
Alisema, mbali ya kusimamia vyema ligi za madaraja tafauti za mpira wa miguu, mkoa huo pia umeweza kuziandalia mashindano mbalimbali timu za mpira wa wavu na mpira wa pete kwa wanawake, kwa kuziandalia mashindano dhidi ya timu za Tanzania Bara, Unguja na Kaskazini Pemba.
Aidha alisema, mkoa wake kupitia sekta ya michezo, umeweza kujenga uhusiano mzuri na wenzao wa mkoa wa Tanga, baada ya kufanyika mazungumzo kati ya mratibu wa michezo Pemba, na viongozi wa Tanga.
Katika hatua nyengine, Tindwa alisema mkoa wake umeyafanyia matengenezo madogo uwanja wa Gombani, ili kuwawekea wanamichezo mazingira mazuri.
Hata hivyo, alisema sekta ya michezo bado inakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokamilika kwa baadhi ya sehemu za uwanja wa Gombani, ikiwemo njia ya kukimbilia (running track), ambayo alisema inapunguza haiba ya uwanja huo.
No comments:
Post a Comment