Habari za Punde

Bodi ya mikopo yaanza kupokea maombi

Na Mwandishi wetu, DSM
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Tanzania (HESLB) imetangaza kuanza kupokea maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na vyuo vikuu pamoja na wanafunzi wanaoendelea kwa mwaka wa masomo 2013/2014 kuanzia Mei 1, 2013.

Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Bodi hiyo, Cosmas Mwaisobwa aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa maombi ya mikopo yatafanyika kwa njia ya mtandao kupitia anuani ya http://olas.heslb.go.tz.

Alisema vipeperushi maalum vyenye maelezo ya jinsi ya kuomba mkopo kwa njia ya mtandao vinapatikana kwenye vyuo vya elimu ya juu, ofisi za elimu za wilaya,watoa huduma ya intaneti, makao makuu ya Bodi ya Mikopo na ofisi za bodi ya mikopo za kanda.

Pia alisema maelezo hayo ya mikopo yanapatikana kwenye tovuti ya bodi ambayo ni: www.heslb.go.tz.

Waombaji wapya wanatakiwa kulipa ada ya maombi ya mikopo ya shilingi 30,000 huku wanafunzi wanaoendelea l wataendelea kulipa ada ya maombi ya shilingi 10,000.

"Wanafunzi wa mwaka wa pili, tatu na nne ambao walilipa ada ya maombi ya shilingi 30,000 katika miaka ya masomo ya 2009/2010, 2010/2011 na 2011/2012 hawatakiwi kulipa tena ada hiyo ya maombi ya mikopo," alisema.

Mwaisobwa alisema mwombaji wa mkopo huo anapaswa kuwa na sifa ambazo zimetajwa katika kifungu cha 17 cha sheria namba 9 ya mwaka 2004 ambazo ni pamoja na na mwombaji kuwa raia wa Tanzania.

Alitaja sifa nyingine kuwa ni kudahiliwa katika chuo cha elimu ya juu, kutokuwa na njia nyingine ya kugharamia elimu ya juu, kufaulu mitihani ya mwaka uliotangulia kwa waombaji wanaoendelea na masomo pamoja na kuwa mhitaji.

"Bodi inasisitiza kwamba waombaji wa mikopo wazingatie muda uliopangwa na pia kufuata kwa umakini taratibu zote zilizoainishwa,” alisema na kusisitiza kuwa hakutakuwa na muda wa ziada baada ya muda uliopangwa kupita.

Alisema mwisho wa kupokea maombi hayo ni 30 Juni 2013.

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu kwa mwaka wa masomo wa 2012/2013 iliwapatia mikopo wanafunzi wapatao 94,703.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.