Othman Khamis, OMPR
CHINA inatarajia kuikabidhi serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jengo jipya la skuli ya msingi ya Mwanakwerekwe ‘C’ katika kipindi cha siku chache baada ya ujenzi kukamilika.
Ujenzi huo umekuja kufuatia ziara ya aliyekuwa Naibu Waziri Mkuu wa China, Hui Liangyu ambae ameshastaafu aliyoifanya Zanzibar na kutia saini mkataba kati ya serikali yake na Zanzibar katika masuala ya uchumi na ufundi ukiwemo pia mradi wa ujenzi wa skuli hiyo.
Mkataba huo ulilenga kuipatia Zanzibar jumla ya RMB 60,000,000 sawa na shilingi za Kitanzania bilioni 14.8 ambapo kati ya fedha hizo ujenzi wa skuli hiyo pekee umegharimu dola za Marekani milioni 1.6.
Balozi Mdogo wa China aliyepo Zanzibar,Chen Qiman alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ofisini kwake katika jengo la Baraza la Wawakilishi.
Balozi Qiman alisema wahandisi wa ujenzi huo wako katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa jengo hilo.
Alisema sera za China za ushirikiano na mataifa ya Afrika ikiwemo Tanzania na Zanzibar kwa ujumla ilitiliwa mkazo zaidi na Rais wa nchi hiyo, Xi Jinping wakati wa ziara yake ya kwanza Tanzania hivi karibuni.
Alisema kupitia sera hizo, China itaendelea kuunga mkono jitihada za Zanzibar za kukijengea mazingira mazuri ya elimu kizazi chake cha sasa kwa faida ya baadaye.
Naye Balozi Seif ameishukuru China kwa hatua zake za kuendelea kuunga mkono Zanzibar kuelekea kwenye maendeleo.
Alisema China kwa kipindi kirefu imekuwa ikiisaidia Zanzibar kitaaluma na hata uwezeshaji katika nyanja tofauti za maendeleo, kiuchumi na ustawi wa jamii.
Ujenzi wa skuli hiyo ulioanza mapema mwezi Agosti mwaka jana ulitanguliwa na ule wa skuli ya msingi ya Kijichi iliyopo wilaya ya Magharibi Unguja.

No comments:
Post a Comment