Na Mwantanga Ame
SERIKALI imewapa kazi mawakili wake kushauri hatua za kuchukuliwa watu waliotajwa katika ripoti ya uchunguzi ya Baraza la Manispaa.
Waziri wa Nchi (OR) na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame, aliliambia baraza kuwa serikali imeanza kulichukulia hatua suala hilo, kwa kuwasilisha ripoti kwa mawakili ili kushauri hatua za kuchukua.
Alisema baada ya jopo la mawakili kukamilisha kazi hiyo, watarejesha kazi hiyo serikalini ili iangalie namna ya kuifanyia kazi.
Alisema baada ya kupokea mapendekezo kutoka kwa mawakili, serikali itayafikisha mbele ya Baraza la Mapinduzi (BLM).
Aliwaomba wajumbe wa baraza kuwa wavumilivu wakati serikali ikisubiri maoni kutoka kwa mawakili wake ili iangalie hatua za kuchukua.
Alisema kwa kiasi kikubwa wizara hiyo imetekeleza maagizo 41 ya Kamati Baraza la Wawakilishi yaliyotolewa katika kikao kilichopita.
Akitaja baadhi ya maagizo hayo,alisema ni pamoja utoaji wa elimu kuhusu vitambulisho vya Mzanzibari mkaazi ambapo kupitia redio tofauti kazi hiyo imefanywa huku taasisi hiyo ikiwa katika hatua za mwisho kuandaa utaratibu wa kusajili wageni, na kutekeleza mpango wa kuzifanyia matengenezo nyumba za Ikulu.
Katika kikao kilichopita cha Baraza,wawakilishi waliiomba serikali kutoa majibu juu ya hoja mbali mbali za uchunguzi uliofanywa na wajumbe wa baraza hilo kuhusu baraza la Manispaa.
Baraza hilo lilidaiwa kuingia mikataba yenye utata hasa ile inayohusu biashara eneo la Saateni huku wawakilishi wakiiomba serikali kuwachukulia hatua baadhi ya watendaji wakuu.
Akiwasilisha maoni ya Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hamza Hassan Juma, alisema serikali inapaswa kuchukua maamuzi magumu juu ya suala la migogoro ya ardhi inayoendelea.
Alisema migogoro ya ardhi haipaswi kuachwa kuendelea kwani inatishia amani na utulivu.
Alisema hali hiyo inatokea zaidi katika ukanda wa utalii kutokana na baadhi ya wamiliki kujenga makuta makubwa ambayo huzuia wananchi kuyatumia maeneo hayo kwa shughuli zao za kila siku.
Aidha, alisema ipo haja kwa serikali kufikiria kuifanyia mabadiliko ofisi ya Mpiga Chapa Mkuu wa serikali kwa kuanzisha shirika, ili kusaidia kuifanya taasisi hiyo kuwa na mipango bora ya kujiendesha.
Aliwataka watu wanaodaiwa na taasisi hiyo kulipa madeni yao.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Ferej, akiwasilisha ripoti ya utekelezaji maagizo ya kamati ya kudumu ya baraza,alisema sehemu kubwa ya maagizo yaliyotolewa yametekelezwa.
Alisema kati ya maagizo hayo ni pamoja na kusimamia tatizo la kuingiza mifuko ya plastiki ambapo hivi sasa imeonekana kupungua na miradi 65 imefanyiwa ukaguzi katika kupambana na tatizo la uchafuzi wa mazingira.
Mwakilishi wa Jimbo la Kitope, Makame Mshimba Mbarouk, alisema bado kuna haja kwa serikali kufikiria namna ya watendaji na viongozi wakuu wanavyotekeleza majukumu yao nchini.
No comments:
Post a Comment