Habari za Punde

Dk Shein akutana na Mkurugenzi Mkuu taasisi ya kimataifa ya utafiti wa kilimo

 Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilkimo (IITA) yenye Makao Makuu nchini Kongo Dk.Nteranya Sangiinga,alipofika Ikulu Mjini Zanzibar na ujumbe wake leo.[
Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo (IITA) yenye Makao Makuu nchini Kongo Dk.Nteranya Sangiinga,(aliyesimama) akitoa maelezo kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,wakati wa mazungumzo akiwa na Ujumbe wake Ikulu Mjini Zanzibar leo. [Picha na Ramadhan Othman,Ikulu.]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu
 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameeleza kuwa juhudi za pamoja katika tafiti za kilimo kwenye mazao hasa ya muhogo na mpunga zinaweza kuleta tija na kuzidisha ongezeko la chakula katika nchi za bara la Afrika ikiwemo Zanzibar.
Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo (IITA), Dk. Nteranya Sanginga akiwa na ujumbe wake, mazungumzo yaliofanyika Ikulu mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake Dk. Shein alisema kuwa utafiti katika sekta ya kilimo ni njia moja wapo katika ukombozi wa kilimo cha aina zote na ndio maana Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inaendelea kukiimarisha kituo chake cha Utafiti kiliopo Kizimbani.
Alieleza kuwa uamuzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Kilimo (IITA), kuzindua mradi wa utafiti wa mazao ya kilimo kwa nchi za ukanda wa joto hapa Zanzibar kutaweza kuleta tija na manufaa katika kuimarisha sekta ya kilimo hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Dk. Shein alisema kuwa mradi huo ambao unazijumuisha nchi 20 ikiwemo Tanzania utasaidia kwa kiasi kikubwa kupanuka kwa tafiti kwenye sekta ya kilimo ambayo ndio sekta mama hapa Zanzibar na Afrika kwa ujumla.
Pamoja na hayo, mbali ya kuzinduliwa kwa mradi huo Dk. Shein alieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa jengo jipya la utafiti wa sayansi kwa nchi hizo lilojengwa jijini Dar-es-Salaam nako kutaongeza idadi ya tafiti na watafiti nchini Tanzania na katika bara la Afrika kwa ujumla.
Alieleza kuwa kuwepo kwa kituo hicho hicho kutaisaidia Zanzibar katika kuendeleza juhudi zake katika tafiti kadhaa za kilimo kupitia kituo chake cha utafiti cha Kizimbani sambamba na kuimarisha mazao ya muhogo, mpunga na mengineyo.
Kwa upande wa zao la muhogo, Dk. Shein alisema kuwa kituo cha utafiti cha Kizimbani kimo katika kuendelea na tafiti mbali mbali za mbegu zikiwemo mbegu za muhogo.
Kutokana na juhudi hizo Dk. Shein alieleza haja ya kuutumia muhogo katika kuzalisha bidhaa tofauti za chakula zinazotokana na zao hilo hasa ikizingatiwa kuwa zao la muhogo ni chakula maarufu katika nchi kadhaa za bara la Afrika ikiwemo Tanzania.
Alieleza kuwa zao la muhogo limekuwa likitumika sana na kuwa chakula muhimu hapa nchini, hivyo ipo haja ya kuliendeleza hasa ikizingatiwa ni zao linalostahamili ukame.
Kwa upande wa zao la mpunga, Dk. Shein alisema kuwa Serikali tayari imeshaweka mikakati maalum kwa kushirikiana na Washirika wa Maendeleo katika kuhakikisha Zanzibar inazalisha mpunga ili kupunguza idadi ya mchele unaoagiziwa nje ya nchi.
Sambamba na hayo, Dk. Shein alitoa shukurani kwa Rais Mstaafu wa Nigeria Mhe. Olasegun Obasanjo kwa mwaliko wake aliomletea wa ufunguzi wa jengo jipya la utafiti wa sayansi linalotarajiwa kuzinduliwa Mei13 mwaka huu jijini Dar-es-Salaam.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa IITA, Dk. Nteranya Sanginga, alimueleza Dk. Shein kuwa uzinduzi wa mradi huo hapa Zanzibar umeiwakilisha Tanzania nzima kwa upande wa taasisi hiyo ambapo Tanzania ni miongoni mwa nchi 20 zilizomo katika mradi huo.
Mradi huo ambao unajikita zaidi na tafiti katika mazao yanayostaamili ukame katika nchi za joto yakiwemo mazao ya muhogo, mtama, mpunga, viazi na mahindi ambapo Tanzania itajikita zaidi na zao la muhogo na mpunga.
Alieleza kuwa taasisi hiyo yenye makao makuu yake Ibadan, Nigeria imekuwa na mashirikiano mazuri kati yake na Wizara ya Kilimo ya Zanzibar kupitia taasisi yake ya utafiti iliyopo Kizimbani.
Aidha, Mkurugenzi huyo alileza kuwa mradi huo wa miaka mitano utaendeshwa kwa upande wa Unguja na Pemba ambapo pia, unajumuisha uangalizi wa mbegu, mafunzo kwa wakulima, tafiti kadhaa katika mbegu za muhogo pamoja na kuishirikisha sekta binafsi.
Alieleza kuwa miongoni mwa mazao yatakayofanyiwa utafiti ni zao la muhogo ambalo ni miongoni mwa zao kuu la chakula katika bara la Afrika ambapo Nigeria inaongoza kwa kuzalisha zao hilo na ya pili ni Congo ikifuatiwa na Tanzania.
Alisema kuwa taasisi hiyo imeweza kuwasaidia wakulima katika kuzalisha chakula cha kutosha kwa kutumia tafiti kadhaa katika nchi za Afrika hasa zile za ukanda wa joto.
Akieleza kuhusu uzinduzi wa jengo jipya la utafiti wa sayansi linalotarajiwa kuzinduliwa mwezi ujao huko Dar-es-Salaam, Mkurugenzi huyo alieleza kuwa lengo la taasisi ya IITA la kuwa na watafiti wengi linaweza kufikiwa katika bara la Afrika ambapo Zanzibar nayo itanufaika.

1 comment:

  1. haya mambo ya kusimamiwa dr sheni hayakuelekea , si ungerahisisha tu , mko watu wachache hapo ukumbini , kuna ulazima gani wa huyo mtu kusimama , au unataka utukufu? jee hujui utukufu uko kwa Mola tu , wengineo wote sisi ni mavi tu , uoza unanuka tukifa hata ukimtupia fisi atakimbia

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.