HOTUBA YA MHESHIMIWA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR, BALOZI SEIF A. IDDI KATIKA UZINDUZI WA WIKI YA USALAMA BARABARANI
HOTELI YA BWAWANI TAREHE 22 APRILI, 2013
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wiki ya Usalama Barabarani na Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi,
Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano,
Wageni waalikwa,
Mabibi na Mabwana.
Assalamu Alaykum,
Mheshimiwa Mwenyekiti,
Awali ya yote sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kukutana hapa tukiwa wazima. Aidha, nachukua nafasi hii kuishukuru Kamati ya Kitaifa ya Wiki ya Usalama Barabarani kwa kunipa heshima hii ya kuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa Wiki ya Usalama Barabarani. Shukrani zangu pia ziwafikie nyote mliohudhuria katika uzinduzi huu.
Ndugu Wananchi,
Muda mfupi ujao Mwenyezi Mungu akituwezesha tutashuhudia tukio la kihistoria katika Visiwa vyetu vya Zanzibar, tukio la uzinduzi wa Wiki ya Usalama Barabarani ikiwa ni sehemu ya kutathmini utekelezaji wa mpango wa miaka kumi ya Usalama Barabani uliozinduliwa na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi tarehe 14 Disemba, 2011. Mpango huo una lengo la kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za barabarani kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020.
Uelewa wa hali ya usalama barabarani duniani umeongezeka baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kueleza kuwa watu wapatao milioni 1.3 hufa na watu wapatao milioni 50 hujeruhiwa ulimwenguni kila mwaka.
Ndugu Wananchi,
Ajali za barabarani zinashika nafasi ya pili kwa kusababisha vifo vingi baada ya ukimwi hasa kwa watu wenye umri wa kuanzia miaka 5 hadi 29 na pia ni ya tatu kwa watu wenye umri wa 30 – 44 kwa kusababisha vifo vingi baada ya ukimwi na kifua kikuu.
Ajali za barabarani zina athari kubwa sana kiuchumi kwani zinapelekea GDP ya dunia kupungua kwa asilimia 3 hadi 6.
Uzinduzi huu wa Wiki ya Usalama Barabarani hapa Zanzibar unafanyika wakati ambapo ulimwengu mzima unakabiliwa na changamoto la ongezeko la ajali za barabarani. Ajali za barabarani zimeleta madhara makubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla. Ajali za barabarani huwaondoa ndugu zetu ambao ndio tegemeo la familia zetu na pia ndio nguvu kazi ya Taifa letu. Aidha, ajali za barabarani huwaacha watu na ulemavu ambao kwa kiasi kikubwa hupunguza uwezo wao wa uzalishaji mali katika kujipatia kipato chao kinachowaendesha katika maisha yao ya kila siku.
Ajali za barabarani ni jambo linaloweza kuepukika iwapo kila Taasisi itawajibika ipasavyo kwa mujibu wa sheria za usimamizi wa usafiri barabarani.
Miongoni mwa mambo yanayochangia ajali hapa nchini tunayoshuhudia kila siku ni:-
- Utumiaji wa simu wakati wa kuendesha gari barabarani.
- Mwendo wa kasi maeneo wanayoishi watu wengi.
- Kutokutii sheria za barabarani.
- Kujitokeza kwa vijana wanaoendesha vespa na pikipiki barabarani kwa mwendo wa kasi hasa wakati wa jioni na usiku.
- Wavunjaji wa sheria za barabarani kutokuchukuliwa sheria zinazofaa kutokana na vitendo vya rushwa.
- Wapandaji wa vyombo vya magurudumu mawili kuacha kutumia helmet na kadhalika.
- Kutokuwepo kwa alama za barabarani za kupunguza mwendo maeneo yanayoishi watu wengi.
Ndugu Wananchi,
Changamoto iliyo mbele yetu ni kujiuliza kwa pamoja ni kitu gani cha kufanya katika kupunguza ajali za barabarani?
Jambo moja muhimu la kuzingatia ni kuwa suala la kusimamia usalama barabarani linahitaji ushiriki wa kila mmoja, kwani bila mashirikiano ya pamoja si rahisi kuweza kuondosha tatizo la ajali za barabarani nchini.
Kwa muda mrefu sasa wananchi tumejenga dhana potofu kuwa, suala la kusimamia ajali za barabarani ni la Kikosi cha Usalama Barabarani (Traffic) na Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano pekee na ndio maana hisia za matukio ya ajali hujaa mioyoni mwa watu pale tu ajali zinapotokea na kuondoka muda mfupi baada ya matukio hayo.
Ndugu Wananchi,
Katika kuhakikisha suala la ajali za barabarani zinapungua kwa kiasi kikubwa nchini mwetu na duniani kwa ujumla, Umoja wa Mataifa unazitaka Taasisi zilizopewa mamlaka ya kusimamia usalama barabarani kuzingatia mambo yafuatayo:-
- Kuhamasisha ushirikishwaji wa jamii katika masuala ya usalama barabarani.
- Kukuza na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa Taasisi mbali mbali zinazoshiriki katika usimamizi wa usalama barabarani ili kuwa na matumizi mazuri ya barabara.
- Kujenga mwamko na uelewa miongoni mwa wananchi juu ya umuhimu wa masuala ya usalama barabarani.
- Kujenga utashi wa hisia za kisiasa katika masuala ya usalama barabarani. Ikiwa ni pamoja na kujenga dhana mpya kwa jamii kuwa, suala la usalama barabarani ni jukumu la kila mmoja, na si suala linalowahusu Jeshi la Polisi na Wizara zinazohusiana na usafiri pekee.
- Kuwa na mikakati ya pamoja katika kusimamia shughuli za usalama barabarani.
- Kila chombo kufuata sheria kwa mujibu wa taratibu ikiwa ni kuondosha suala la muhali.
Ndugu Wananchi,
Serikali kwa upande wake imeanzisha Kamati maalum ya Kudumu ya kusimamia suala la usalama barabarani ikiwa na jukumu la kuhakikisha vifo vinavyotokana na ajali za barabarani vinapungua kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020. Kamati hii itatathmini hali halisi kila mwaka na kupendekeza hatua za kuchukuliwa ili kufanikisha malengo ya millenia.
Ndugu Wananchi,
Katika uadhimishaji wa Wiki ya Usalama Barabarani kutakuwa na matukio mbali mbali yanayohusu usalama barabarani ikiwa ni pamoja na utolewaji wa elimu ya usalama barabarani, ukaguzi wa vyombo vya moto na kadhalika. Hivyo, natoa wito kwa madereva kutoa ushirikiano mkubwa katika maadhimisho ya Wiki ya Usalama Barabarani. Aidha, katika wiki hiyo nachukua nafasi hii kuwaomba wananchi kuwa wastahamilivu kutokana na aina ya usumbufu wowote unaoweza kujitokeza.
Ndugu Wananchi,
Katika juhudi za kuyafikia malengo ya mpango wa miaka kumi ya usalama barabarani natoa wito kwa madereva kutoendesha mwendo wa kasi wanapokuwa barabarani, kutii sheria za barabarani, kuwajali watumiaji wengine wa barabara ikiwa ni pamoja na waenda kwa miguu, wapanda baiskeli na watu wenye mahitaji maalum.
Ndugu Wananchi,
Kwa upande wa Serikali itahakikisha kuwa inasimamia vilivyo sheria za barabarani kwa kuwachukulia hatua wale wote wanaokaidi sheria hizo. Serikali pia inahakikisha kuwa barabara zinazojengwa zinakidhi viwango ikiwa ni pamoja na uimara wa barabara zenyewe, upana, pamoja na kuwekwa alama za barabarani.
Ndugu Wananchi,
Ni ukweli usiofichika kuwa katika sekta ya usafiri barabarani ziko changamoto nyingi ambazo tukifuata sheria za usalama barabarani tutaziondoa moja baada ya moja.
Najua kuwa zipo gari nyingi zinazotoa huduma za kusafirisha wananchi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyengine na hata zinapangiana zamu, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba baadhi ya gari hizo zinawanyanyasa wananchi ambao ndio abiria wao kwa kutowafikisha mwisho wa safari kama walivyoomba ruhusa ya usafirishaji pamoja na kuwatolea lugha zisizofaa.
Ndugu Wananchi,
Nachukua fursa hii kutoa wito kwa wananchi wote ambao wanatumia usafiri wa daladala na usafiri wa magari ya shamba kuchukua hatua za kuziripoti katika Vituo vya Polisi au katika Idara ya Usafiri na Leseni gari zote ambazo zitawafanyia vitendo vitakavyokiuka sheria za barabarani ili hatua kali za kisheria dhidi yao zichukuliwe. Aidha, ninakuombeni mtoe mashirikiano yanayofaa ili kuhakikisha vitendo hivyo vinakomeshwa.
Ndugu Wananchi,
Natumia fursa hii kuliamuru Jeshi la Polisi, kikosi cha Usalama Barabarani kusimamia sheria za usalama barabarani na kuondowa muhali kwa wote wanaokiuka sheria za barabarani kwa kuwachukulia hatua kali za kisheria kwani hakuna mtu aliyejuu ya sheria
Ndugu Wananchi,
Kama nilivyokwisha kusema hapo awali kuwa, suala la usalama barabarani linahitaji nguvu za pamoja kwa kila mmoja kutoa mchango wake, kwani waswahili wanasema “Kidole kimoja hakivunji chawa” kwa pamoja tunaweza kutokomeza ajali za barabarani kama unavyoelezea ujumbe wa mwaka huu kuwa “KUONDOA AJALI ZA BARABARANI NI JUKUMU LETU SOTE!”.
Mwisho, napenda kukushukuruni nyote mliyohudhuria katika shughuli hii muhimu inayohusiana na usala wa maisha yetu.
Baada ya maelezo hayo, sasa natamka rasmi kuwa, “Wiki ya Usalama Barabarani imezinduliwa rasmi”.
Ahsanteni kwa kunisikiliza
vifonaajalizabarabarani,vitapungua,kwajitihadanabidiiyamakusudi,yakuwachukuliahatua,maderevawazembe,tukiliwezahilo,vifonaajalivitapunguaaukwishakabisa
ReplyDelete