Joseph Ngilisho,Arusha
MBUNGE wa Arusha mjini, Godbless Lema ameachiwa kwa dhamana ya shilingi milioni moja baada ya kushtakiwa kwa makosa ya uchochezi katika mahakama ya Mkoa Arusha.
Lema alifikishwa mahakamani hapo majira ya saa 2:50 asubuhi akiwa kwenye gari dogo chini ya ulinzi mkali wa polisi na kupandishwa kizimbani saa 3:56 asubuhi ambapo mwendesha mashtaka wa serikali, Elianenyi Njiro alidai mahakamani kwamba mshitakiwa alitenda kosa la uchochezi kinyume na kifungu cha sheria namba 390 na kifungu kidogo namba 35 cha sheria ya adhabu ya mwaka 2002.
Akiwa mbele ya hakimu Devota Msofe wa mahakama hiyo,Njiro alidai kuwa maneno yaliyotamkwa na mshtakiwa huyo kuwa ”Mkuu wa Mkoa anakuja kama anakwenda kwenye sendoff, hajui chuo cha uhasibu kilipo wala hana taarifa za mauaji ya mwanafunzi, ameshindwa kuwapa pole wafiwa na kusikiliza shida zenu na amesema hawezi kuzungumza na wanafunzi wasio na nidhamu” ni uchochezi.
Katika kesi hiyo Lema aliwakilishwa na wakili, Method Kimomogolo akisaidiwa na Humphrey Mtui,hata hivyo mawakili hao walilalamikia kitendo cha mteja wao kunyimwa dhamana na polisi na kujikuta akisota kwa siku tatu mfululizo mahabusu ya polisi.
Baada ya kusomewa mashtaka yanayomkabili, Lema alikanusha na kuiomba mahakama impatie dhamana ambapo hakimu anaesikiliza kesi hiyo, alimtaka kujidhamini kwa shilingi milioni moja.
Kesi yake imeahirishwa hadi Mei 29 wakati itakapotajwa tena.
Katika mahakama hiyo kulikuwa na umati mkubwa wa wafuasi na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mashabiki, wafuasi na wanachama wa chama hicho walifurika katika mahakama hiyo kwa ajili ya kushuhudia mashtaka dhidi ya Mbunge huyo.
Polisi wa kukabiliana na ghasia walitanda katika viunga vya mahakama ili kuhakikisha usalama unaimarishwa.
Lema alitokea moja kwa moja mahabusu alikokuwa akishikiliwa tokea alipokamatwa kwa tuhuma za uchochezi wa vurugu zilizosababishwa na wanafunzi kwenye chuo cha Uhasibu mwanzoni mwa wiki iliyopita wakilalamikiwa mwenzao kuuawa.
Baada ya kuachiwa, Mbunge huyo aliongozana na wafuasi wake kwa msafara wa maandamano na mapikipiki kuelekea ofisi za chama hicho.
Akizungumza na wafuasi wake,alilitaka jeshi la polisi na vyombo vingine vya dola mkoani hapa,kubuni mikakati mbadala ya kumdhoofisha kisiasa,kwani mbinu za kumkamata na kumweka mahabusu amekuwa mzoefu wa matukio na kwamba anajua kulala na kunguni,kutopiga mswaki na kutumia choo cha watu wengi.
Aidha alisema misukosuko inayomwandama ya kukamatwa na kuwekwa mahabusu mara kwa mara, inamkomaza na kumjengea umaarufu kwa jamii hususani wapiga kura wake.
No comments:
Post a Comment