Habari za Punde

G20 zashauriwa kuwekeza EAC

Na Othman Khamis, OMPR
MATAIFA yanayoendelea kiuchumi (G20) yameshauriwa kuwekeza katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki(EAC) ili kuunga mkono ukuaji wa uchumi.

Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Yoweri Museveni wa Uganda katika mkutano wa 11 wa wakuu wa jumuiya hiyo uliofanyika hoteli ya kimataifa ya Ngurdoto mkoani Arusha.

Rais Museveni alisema mataifa hayo yanaweza kuongeza nguvu zao katika kusaidia miradi ya miundombinu ya barabara,mawasiliano na sekta binafsi.

Alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki imelenga kunyanyua maisha ya wananchi wake kwa kuimarisha sekta zisizo rasmi kwa vile uwezo wa serikali hizo katika kutoa ajira hasa kwa vijana bado ni mdogo.

Alitolea mfano wa Uganda ambayo imejidhatiti katika kuimarisha nguvu za sekta binafsi ili kupunguza wimbi la vijana wengi wanaomaliza masomo ambao hubaki wakizurura mitaani bila kazi.

“Vijana popote pale walipo ndio nguvu kazi ya taifa. Hivyo bado upo umuhimu wa kuwaandalia mazingira mazuri yatakayotoa fursa ya kuyatumikia vyema mataifa yao,” alisema.

Akiwahutubia viongozi hao wa EAC ambao ni Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi, Waziri Mkuu wa Rwanda,Pierre Damien, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi akimuwakilisha Rais wa Zanzibar,Rais Museveni alimpongeza Rais wa Kenya Uhuru Kenyata kwa kujumuika pamoja katika mkutano huo baada ya kuchaguliwa kuiongoza Kenya.

Alisema wananachi wa Kenya wanastahiki kupongezwa kutokana na hatua yao ya kufanya uchaguzi katika hali ya amani na utulivu.

Akiuhutubia mkutano huo kwa mara ya kwanza baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Kenya, Kenyata alisema Kenya inaendelea kujivunia kuwa mwanachama wa EAC.

Alisema uanachama huo unasaidia kuendeleza ushirikiano wa ujirani mwema uliopo katika kuimarisha masuala ya kiuchumi, forodha, usafiri wa anga na hata ule wa barabara zinazounganisha mataifa hayo wanachama.

Kenyata aliwaahidi viongozi wa jumuiya hiyo kwamba nchi yake itaendelea kuwa huru kwa mwananchi yeyote wa jumuia hiyo kuishi au kuwajibika katika shughuli za kiuchumi.

Alieleza kwamba wanajumuiya ya Afrika Mashariki wana wajibu wa kufanya kazi pamoja katika kuona ushirikiano wa jumuiya hiyo unaendelea kuwa wa kudumu.

Akizungumzia amani, Kenyata alisema nchi hiyo itaendelea kuunga mkono harakati za kuimarisha hali ya ulinzi ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki na pembe ya Afrika.

Mkutano huo wa wakuu wa EAC umemteua Charles Kackson Njoroge kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo uteuzi unaotarajiwa kuanza rasmi tarehe 9 Juni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.