Habari za Punde

Balozi Seif Akutana na Balozi Mpya wa Uingereza Ofisini Kwake Vuga.


 
 Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bibi Dianne Melrose akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ofisi yake iliyopo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbeni.
Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bibi Dianna Melrose akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ofisi yake iliyopo ndani ya Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbeni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mke wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Mama Fatma Karume akisalimiana na Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Dianna Melrose katika jingo la Baraza la Wawakilishi Mbweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.(Picha no Hassan Issa wa - OMPR – ZNZ)


Press Release:-

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Uingereza ina uwezo wa kusaidia juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika Taaluma ya kuimarisha Kilimo cha umwagiliaji Maji ambacho kimepewa msukumo zaidi.


Alisema Serikali imemua kuimarisha Kilimo hicho lengo likiwa kuongeza chakula sambamba na kuwapunguzia umaskini wananchi walio mwengi ambao ni Wakulima.

Balozi Seif alisema hayo wakati akizungumza na Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bibi Dianna Melrose hapo Ofisini kwake kwenye Jengo la Baraza la Wawakilishi Mbweni Nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Alisema zaidi ya asilimia 70 ya Wananchi wa Zanzibar wako Vijijini wakijishughulisha na harakati za kilimo hali iliyopelekea Serikali kujikita zaidi katika kuimarisha miundo mbinu ya kilimo ambapo umwagiliaji maji ukipewa kipau mbele.



“ Sio mbaya kwa Uingereza ambayo ina utaalamu mkubwa katika sekta ya elimu ikasaidia Zanzibar kwa vile wananchi wengi wa Visiwa hivi wanaishi kwenye maeneo ya kilimo “. Alifafanua Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimueleza Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania kwamba Zanzibar pia ina nyengine kadhaa za uwekezaji ikiwemo Viwanda vya usindikizaji matunda ambapo wafanyabiashara wa Uingereza wana nafasi ya kuitumia Fursa hiyo.

Akizungumzia suala la kukabiliana na maafa yanapotokea Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na juhudi ya kuwasiliana na washirika wa maendeleo katika kuijengea uwezo idara ya Maafa ili itekeleze vizuri majukumu yake.

Alisema hatua hiyo imekuja kutokana na Zanzibar kukumbwa na ajali za meli mbili za abiria zilizotokea katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni na kusababisha maafa makubwa yaliyoleta simanzi miongoni mwa Wananchi.

Mapema Balozi wa Uingereza Nchini Tanzania Bibi Dianna Melrose alisema Nchi yake itaendelea kushirikiana na Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukuza uhusiano wa muda mrefu uliopo kati ya pande hizo mbili.

Balozi Dianna alifahamisha kwamba Mataifa hayo mawili yamekuwa yakibadilishana Taaluma katika masuala ya matumizi sahihi ya ardhi sambamba na utawala bora ili kufanikisha dhana nzima ya demokrasia baina ya Viongozi na Wananchi.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
17/4/2013.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.