Na Ali Cheupe
UONGOZI wa klabu ya Malindi inayoshiriki ligi kuu ya soka Zanzibar, umetishia kuiondoa timu yake kisiwani Pemba, ambako iko kwa ajili ya mechi za ligi hiyo.
Malindi imetoa madai ya kufanyiwa hujuma kuwa ndiyo sababu ya kutaka kuchukua hatua hiyo.
Akizungumza kupitia kituo kimoja cha redio hapa Zanzibar, Katibu Mkuu wa klabu hiyo Mohammed Masoud Rashid, amesema uamuzi huo ulifikiwa mara baada ya kupokea taarifa za pambano lao dhidi ya Jamhuri lililochezwa juzi uwanja wa Gombani.
Viongozi walioandamana na timu hiyo wamewanyooshea vidole waamuzi wa mchezo huo, wakidai kwamba wameshirikiana na viongozi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) kisiwani humo kuikandamiza timu hiyo.
Katibu huyo amedai kuwa, awali walijuilishwa na mjumbe wa kamati tendaji ya ZFA Taifa Masoud Attai, kuwa klabu chama hicho kitapeleka waamuzi wawili kutoka Unguja kwa ajili ya kusaidiana na wenzao wa Pemba, lakini akashangazwa ZFA Pemba kuwakataa waamuzi hao.
"Hapa ndipo napata picha ya kile kinachosemwa kuwa ZFA ziko mbili, Unguja na Pemba. Iweje upande mmoja unaamua na mwengine unakaidi ikiwa wote ni wamoja'', alihoji kwa hasira kiongozi huyo.
Masoud alifika mbali kwa kudai kuwa, kulifanyika kikao cha siri kati ya viongozi wa ZFA Pemba na waamuzi, kwa lengo la kupanga mikakati ya kuziangamiza timu za Unguja.
Alipoulizwa ni wapi alikozipata taarifa hizo, Masoud alisema, "Kwenye mchele hakukosi chuwa, baada ya kumalizika kikao tu mwamuzi mmoja aliwajuilisha viongozi wetu na hatimae ushahidi ukaonekana uwanjani."
Akitilia mkazo madai hayo, alisema siku zote Malindi inafungwa na haijawahi kulalamika lakini kwa vitendo vya kiajabu walivyofanyiwa kwenye pambano lao na Jamhuri ambapo Malindi lililala kwa mabao 3-1, timu yake haina haja ya kuendelea na mchezo wowote kisiwani humo, ili kuepusha vurugu.
Ratiba ya ligi hiyo inaonesha kuwa, masarahange hao watashuka tena kwenye dimba la Gombani kesho kupepetana na Chipukizi.
Wenye Malindi washakufa wacheni waliopo wafanye watakavyo, klabu za asili za zanzibar zimeisha kwa mfano vikokotoni, malindi, miembeni na kikwajuni sasa imebakia mifupa tu
ReplyDeleteHawa Malidi kufugwa ndio imukuwa nongwa!!! Mimi sioni sababu kwa nini ZFA kupeleka waamuzi Pemba wakati huko Pemba wako waamuzi Wa ngazi juu!!! Lakini pia kwanini na Hawa Malindi wang'ang'ania kuchezeshwa na waamuzi kutoka Unguja? ....????? Hapa kuna walakini......
ReplyDelete