Na Juma Khamis, Pemba
BAADA ya kufanya utafiti mdogo na kubaini kuwa moja ya vyanzo vilivyosababisha wanafunzi wa kidato cha nne kufeli katika mitihani ya kitaifa mwaka 2012 ni wazazi kutokujua umuhimu wa elimu, walimu skuli ya sekondari Fundo wameanzisha darasa la watu wazima lenye wanafunzi 360.
Wanafunzi hao wamegawanya katika madarasa 13 na wanafundishwa siku mbili kwa wiki.
Akizungumza na Zanzibar Leo, mwalimu Suleiman Ali Said alisema walimu wanaowafundisha wazee hao ni walimu kutoka skuli hiyo pamoja na wanafunzi wanne waliofeli mitihani ya kidato cha nne mwaka uliopita.
Alisema wazee hao wanafundishwa kujua kusoma na kuandika pamoja na kujengewa uwezo wa kupenda kufuatilia na kuchangia maendeleo ya elimu ya watoto wao.
Alisema moja ya sababu kubwa zilizochangiwa wanafunzi wa kisiwa hicho kufanya vibaya katika mitihani hiyo ni wazazi kutojali maendeleo ya watoto wao na kuwashirikisha katika shughuli za uvuvi hata kama wako kidato cha nne.
“Tunaamini hii itakuwa dawa na tuna hakika tutafanikiwa,” alisema.
Wanafunzi hao wanafundishwa bure isipokuwa wanachotakiwa ni kununua mabuku na kalamu kwa ajili ya kuandikia.
No comments:
Post a Comment