Habari za Punde

Mwandishi wa habari mmoja huuawa kila wiki

Na Kunze Mswanyama, DSM
IMEELEZWA kuwa,kila wiki mwandishi wa habari mmoja huuawa huku kesi moja kati ya kumi za kuuawa,kuteswa na kujeruhiwa kwa waandishi hufikishwa mahakamani ikiwa ni idadi ndogo kabisa ikilinganishwa na wingi wa matukio yanayotokea duniani kote.

Aidha,chanzo cha kuuawa,kuteswa na kujeruhiwa kwa waandishi wa habari duniani ni kutokana na kuibua uovu unaofanywa na watawala ambapo ufisadi,rushwa na matumizi mabaya ya madaraka yanayoripotiwa na vyombo vya habari,huwakera baadhi ya wahusika ambao huamua kuficha matendo yao kwa kuwaua,kuwajeruhi na kuwatesa waandishi wa habari kote duniani.

Hayo yalibainishwa jana wakati wa kutangaza maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambapo siku hiyo mada mbalimbali zitajadiliwa huku azimio la Arusha la vyombo vya habari,litatolewa ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa Mfuko wa Mwangosi utakaotumika kuwafadhili waandishi wa habari waliopatwa na majanga wakiwa kazini.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari na Mwenyekiti wa Waandishi wa habari wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) nchini,Al Amin Yusuph, mazingira ya ufanyaji kazi kwa waandishi wa habari duniani,siyo salama ambapo tahadhari kubwa inatakiwa kuanzia vyumba vya habari hadi kwenye matukio ya kihabari.

Alisema,wao kama Umoja wa Mataifa,wameamua kuhangaikia usalama wa waandishi wa habari ambapo kwa mujibu wa utafiti wao,kama vyombo vya habari vitafanya majukumu yao vyema,kutakuwa na maendeleo huku wananchi wakitakiwa kufanya maamuzi kutokana na taarifa wanazopata kupitia vyombo vya habari.

Alisema vyombo vya habari vya vijijini ambavyo vilikuwa havina malalamiko ya kufuatiliwa na vyombo vya usalama,vimeanza kuripoti kufuatiliwa na watu wa usalama jambo linalotishia uwepo wa uhuru wa habari.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Vyombo vya Habari (TMF),Ernest Sungura,alisema wamejipanga ili kutoa fedha kwa waandishi wa habari nchini kufanya utafiti mbalimbali na kuuhabarisha umma ambapo jambo hilo linapaswa kwenda sambamba na maslahi bora kwa waandishi wa habari.

“Wahariri mnatakiwa kujipanga vyema ndani ya vyumba vya habari ili kuwalinda waandishi wenu,wekeni ulinzi ikiwa ni pamoja na milango yenye teknolojia za kisasa za kufungua milango ambapo waandishi wote watapewa funguo hizo ambazo zinakuwa zimewekwa kwenye teknolojia ya kisasa,” alisema.

Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Umoja wa Klabu za Waaandishi wa Habari (UTPC),Jane Mihanji,alisema umefika wakati waandishi wa habari kuacha kuandika malalamiko ya watu wengine na huku wakiyapa kisogo malalamiko yao yanayoendana na mazingira mabovu ya kazi ikiwa ni pamoja na ufinyu wa mishahara yao.

Siku ya uhuru wa vyombo vya habari iliyoasisiwa na Umoja wa Mataifa kupitia shirika la Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia mwaka 1991,Windhoek nchini Namibia ikitaka kuzikumbusha serikali za nchi wanachama wa UN kuheshimu haki za binadamu na demokrasia kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Katika kongamano hilo ambalo litahudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi wanachama wa Shirikisho la Afrika Mashariki,litafanyika mjini Arusha,Mei 2-5 huku waandishi wengi wa habari wakitarajiwa kuhudhuria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.