Na Mwandishi wetu, Dodoma
BAADA ya Wabunge kuikataa bajeti ya Wizara ya Maji kutokana na kutoridhika na kiwango cha fedha kilichotengwa kwa wizara hiyo, hatimae serikali imekubali kuongeza shilingi bilioni 184.5.
Waziri wa Fedha, Dk. Wiliam Mgimwa aliliambia Bunge kuwa serikali imeliangalia kwa kina tatizo la maji na kuungana na hoja za Wabunge kuwa tatizo la maji lipewe kipaumbele.
Alisema fedha hizo zitatokana na mafungu ya bajeti ya serikali ikiwemo posho ambayo hayataathiri shughuli za serikali.
Mapema jana, Spika wa Bunge alilazimika kusitisha shughuli za bunge hadi saa 11:00 jioni baada ya Wabunge kutaka kupatiwa taarifa za maandishi za marekebisho ya bajeti ya wizara ya maji.
Spika alichukua uamuzi huo ili kuipa nafasi serikali kutayarisha taarifa za marekebisho ya bajeti hiyo na kusambazwa kwa wabunge.
Wiki iliyopita, Wabunge waliikataa bajeti ya wizara hiyo iliyowasilishwa na Waziri Profesa Jumanne Maghembe wakisisitiza kuwa bajeti haitoshi kutokana na hali ya upatikanaji wa maji nchini kuwa mbaya.
Mbali na kueleza hali mbaya ya upatikanaji maji majimboni, wabunge wengine walitoa ushahidi kuwa wanakotoka hulazimika kuoga kwa zamu na wakati mwengine hawaogi kwa siku kadhaa.
Spika Makinda ndiye alieahirisha kupitishwa bajeti ya wizara hiyo, wakati akitoa majibu ya mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Iramba Mashariki, Mwigulu Nchemba (CCM).
Nchemba katika hoja yake ya kuombwa mwongozo alitaka mjadala wa bajeti ya wizara hiyo usitishwe ili kutoa nafasi kwa serikali kukaa na Kamati ya Bajeti kuangalia namna ya kutatua ufinyu wa fedha zilizotengwa.
No comments:
Post a Comment