Habari za Punde

Kificho alipongeza UNDP

Na Himid Choko
SPIKA wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho amesema wajumbe wa Baraza hilo hivi sasa wako makini zaidi baada ya kujengewa uwezo mkubwa wa kiutendaji chini ya ufadhili wa Shirila la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Alisema kwa kipidi kirefu UNDP kupitia miradi tofauti ya kusaidia mabunge, imeweza kusaidia kutoa taaluma ya utendaji wa vyombo hivyo nchini.

Alisema kwa upande wa Baraza la Wawakilishi, chini ya miradi hiyo limekuwa likifaidika kwa mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa wajumbe wa baraza hilo pamoja na watendaji.

Aidha alisema UNDP kwa kiasi kikubwa imesaidia vitendea kazi ndani ya baraza hilo ikiwemo usafiri.


Spika Kificho alisema hayo jana wakati akizungumza na Naibu Mkurugenzi Mkaazi wa UNDP nchini,Mandisa Mashologu ofisini kwake Chukwani.

Alisema kutokana na mafunzo hayo hivi sasa anaridhishwa na utendaji wa wajumbe hao, jambo ambalo limejenga heshima na imani kubwa kwa wananchi kuhusiana na maendeleo ya chombo chao cha Kutunga Sheria.

Akitoa mfano Spika Kificho alisema wajumbe wa baraza tayari wamejengewa uwezo katika masuala ya uchambuzi wa bajeti na miswada ya sheria na mafanikio yake yameanza kuonekana.

Alisema kutokana na mafunzo hayo wajumbe wa baraza hilo hivi sasa wamekuwa makini zaidi wakati wa uchambuzi wa bajeti ya serikali na miswada ya sheria, kitendo ambacho mara nyengine kinawaweka katika wakati mgumu baadhi ya mawaziri na watendaji wa serikali kwa ujumla.

Alisema hali hiyo inapelekea uwajibikaji mzuri wa wajumbe wa baraza hilo pamoja na mawaziri suala ambalo ni zuri kwa ustawi wa jamii na maendeleo ya taifa.

Spika kificho alimueleza Naibu Mkurugenzi huyo wa UNDP kuwa hata katika utendeji wa kamati za baraza hilo, umeimarika ambapo hivi sasa kamati zimekuwa zikiibua mambo mengi yanayohususiana na udhaifu au mafanikio ya utendaji wa serikati na taasisi zake.

Amelishukuru shirika hilo kwa misaada yake kwa baraza la wawakilishi na taifa kwa ujumla na kuahidi kuendelea kuitumia vyema fursa inayotolewa na shirika hilo.

Kwa upande wake, Mandisa Mashologu alisema anaridhishwa na matumizi ya misaada inayotolewa na shirika hilo kwa baraza la wawakilishi nha kuahidi kuendelea kufanyakazi kwa karibu zaidi na ofisi hiyo.

Alisema UNDP iko tayari kuendelea kusaidia vyombo vya kutunga sheria lengo likiwa ni kuimarisha kuongeza uwazi wa utendaji wa taasisis hizo.

Alisema ni muhimu kwa wananchi kufahamu kwa uwazi kinachotendeka ndani ya vyombo hivyo ikiwa ni njia moja wapo ya kukuza demokrasia na utawala bora hapa nchini.



No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.