Na Salim Said Salim
NAMNA ambavyo mwili wa binadamu umegawika unatoa mafunzo makubwa kwa wale
wanaotaka kujifunza na wasiotaka.
Kila sehemu ya mwili au kiungo cha binadamu huwa na kazi yake maalumu. Kazi
ya mdomo ni kusema, iwe kwa sauti kubwa, ndogo, upole au ya ukali.
Macho hufanya kazi ya kuona, masikio kusikia kinachozungumzwa kwa sauti kubwa
au kunong’onwa, pia huwa inanusa harufu na kutoa pumzi, miguu inatusaidia kwenda
na kadhalika.
Hata siku moja sijapata kusikia bega kufanya kazi ya akili au meno kumsaidia
mtu kukimbia mbio. Hivyo ndivyo ilivyo kwa maisha ya kila siku ya mwana wa Adam
na Hawa.
Hali hii ni kielelezo kizuri tulichopewa na Mola wetu (kwa wale tunaoamini
kuwepo kwa Mwenyezi Mungu) juu ya umuhimu wa kazi na hatari za watu kuingiliana
katika kazi zao na majukumu waliyonayo, iwe katika familia zao au jamii.
Ni kwa mantiki hii ya mgawanyo wa kazi uliopo katika mwili wa binadamu ndiyo
Waswahili wa ukanda wa Pwani wakaja na msemo wa kukataa mtu mmoja kufanya kazi
zote unaoeleza…. “Mlalamikaji Msomali, mwendesha mashitaka Msomali na hakimu
Msomali.”
Lengo la usemi huu ni kuitahadharisha jamii juu ya hatari ya anayelalamika
kuwa ndiye huyo huyo anayefungua mashitaka na hata kuchukua kazi ya hakimu. Hapa
unajitokeza umuhimu wa mgawanyo wa kazi katika kutekeleza na kusimamia sheria na
katika kutoa haki.
Kwa upande wa Mrima (Bara) upo usemi unaofana na huu unaotoa onyo kwa kesi ya
nyani kumpa ndegere kuhukumu.
Ni katika mtazamo huu nilioueleza ndiyo katika dunia ya leo ukasisitizwa
umuhimu wa kugawana majukumu ili kuhakikisha demokrasia inastawi na utawala wa
haki na sheria unafanya kazi, ikiwa pamoja na mfumo wa mahakama huru.
Polisi nao wakapewa madaraka na mamlaka ya kuwabana wanaotuhumiwa na uhalifu
na kufanya uchunguzi juu ya tuhuma zinazowakabili ili kupata ushahidi wa
kuwasilishwa mahakamani kwa kutolewa hukumu.
Lakini katika kuonyesha kuwa polisi hawasimamii uendeshaji wa mashitaka ndiyo
pakaundwa ile tunayoielewa kama Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP).
Tanzania Bara imekuwa na ofisi hii kwa zaidi ya miaka 40 sasa. Zanzibar
ilikawia kuwa na ofisi hii, lakini iliamua kwenda sambamba na ulimwengu wa mfumo
haki na sheria miaka 12 iliyopita kwa kuanzisha ofisi ya DPP.
Kwa hili Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inastahili pongezi, ijapokuwa
ilikawia kufanya hivyo. Wazee walitupa faraja kwa kutwambia bora kukawia kufika
kuliko kutoifanya safari kabisa (Better late than never).
Kwa bahati mbaya, katika siku za karibuni kumeonekana kuingiliwa kikazi au
kuwekewa vizingiti ofisi ya DPP katika utendaji wake wa kazi na kupelekea baadhi
ya watu kujiuliza: Tunaelekea wapi?
Wapo watu, tena wengi, walioanza kuwa na wasiwasi mkubwa kwamba tunaonekana
kutaka kurudi (au kurudishwa) kule tulikotoka kwa ‘mlalamikaji Msomali,
mwendesha mashitaka Msomali na hakimu Msomali.’
Ule ndio wakati tuliokuwa na zile zilizoitwa mahakama za wananchi (people’s
courts) ambazo wengi wa mahakimu wake walikuwa hawajui kusoma wala kuandika,
watu ambao umri mkubwa ulikuwa umewapunguzia hekima na busara na matokeo yake
kusinzia wakati walipokuwa wakisikiliza kesi.
Kichekesho kikubwa zaidi ni kuwa aliyeendesha mashitaka baadaye ndiye
aliyekuwa mtetezi wa hao hao aliowatia hatiani, yaani jana alisema wana makosa
na siku ya pili anaiambia mahakama kwamba washitakiwa hawana makosa.
Mfano ni ule wa kesi ya uhaini kufuatia kuuawa kwa Rais wa kwanza wa
Zanzibar, Abedi Amani Karume mwaka 1972.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali alisema washitakiwa walikuwa na hatia na baadaye
akaja kuwatetea na kusema hawana hatia. Huko ndiko ilikotoka Zanzibar.
Miongoni mwa mifano iliyojitokeza karibuni na kuanza kutia shaka kama upo
utawala wa haki na sheria Zanzibar ni namna ambavyo jamii imesikia juu ya baadhi
ya kesi nyeti zinazoendelea Zanzibar. Miongoni mwao ni ile ya kijana Omar Musa
Makame anayetuhumiwa kumuua Padre Evaristus Mushi miezi miwili iliyopita.
Katika kesi hii tulielezwa kuwa Ofisi ya DPP ilikataa kutoa hati ya mashitaka
kwa Jeshi la Polisi. Ofisi ya DPP na Polisi zilirushiana mpira juu ya mvutano
huu kwa kila upande kukataa kueleza kwanini hati ya mashitaka ilikuwa
haikutolewa.
Huu sio utawala bora, wa ukweli na uwazi kwa sababu kilichoonekana hapa ni
usiri na wahusika kutojiamini katika utendaji wao wa kazi.
Hili ni suala ambalo umma unaficha watu haki ya kupewa habari zake na kitendo
cha kuficha watu kupata habari ni ukiukaji wa haki za binadamu.
Lakini baadaye tukaona mshitakiwa amefunguliwa mashitaka, lakini pia
haikuelezwa kama cheti cha kuruhusu kesi hiyo kuanza kilitolewa, na kama ni
hivyo kwa misingi gani na ni nini kilichotokea hata ofisi ya DPP ikasalimu
amri.
Hapa ipo shaka na tayari zinasikika tetesi nyingi katika jamii juu ya suala
hili nyeti, nyingine zikiwa zimeongezwa chumvi na nyengine zimepunguzwa
sukari.
Ukimya na uvumi kwa kiasi fulani vinapunguza imani ya wananchi kwa serikali
yao, Jeshi la Polisi na ofisi ya DPP.
Wananchi pia wanataka walezwe kwa nini polisi walikaa na mshitakiwa kwa zaidi
ya wiki mbili bila ya kumfikisha mahakamani wakati sheria inakataza hilo
kufanyika. Au ndiyo tuseme polisi ndio wenye haki ya kuvunja sheria za nchi hii
na raia ndio wanaolazimika kuziheshimu?
Ni muhimu katika masuala kama haya kwa kila taasisi kuelewa mipaka ya kazi
yake, kuheshimu wajibu na mamlaka ya taasisi nyingine na umma kuelezwa kwa uwazi
kila jambo linalowagusa maisha yao na mwelekeo wa nchi yao.
Wale wanaofikiri wanaweza kufanya watakalo, waelewe zama zile zimepita na
wasije kusema wanaonewa ikifika siku wakawajibishwa kwa kuvunja sheria
zilizotungwa na Baraza la Wawakilishi na kuwekewa sahihi na Rais wa Zanzibar ili
zitumike.
Nchi yetu imesaini mikataba ya kuheshimu haki za binadamu, hivyo tunalazimika
kuheshimu yale yote yaliyomo katika hiyo mikataba, ikiwa pamoja na mtindo wa
kuendesha kesi kwa staili za ‘kumuachia Msomali kumkamata mtuhumiwa, kumfungulia
mashitaka na kumhukumu’.
Mahakama nayo inapaswa kusimama kidete kusimamia uhuru wake iliopewa kisheria
na wale wote wanaoichezea wachukuliwe hatua za kisheria, lakini sio kwa uonevu
bali kwa misingi ya sheria.
Baadhi yetu tunaojifanya kuwa na vifua vipana kutokana na madaraka tuliyonayo
au kwa sababu nyingine, lazima tuelewe kuwa mtu huhukumiwa kwa maovu yake na sio
mema yake.
Viongozi wa Jeshi la Polisi wanapaswa kuelewa mipaka yao ya kazi na kuheshimu
wajibu na mamlaka ya taasisi nyingine. Ipo siku watarudi uraiani na
watakapotakiwa maelezo kwa yale ambayo jamii inahisi hayakuwa ya haki ambayo
waliyatenda walipokuwa kazini wasilalamike.
Mtu huvuna anachokipanda, kwa hivyo wajitahidi kupanda mbegu nzuri ili mavuno
yao hatimaye yawe mazuri.
Viongozi wetu, wakiwemo maafande, wanapaswa kujifunza kwa yale yanayowakuta
wengine baada ya kustaaafu.
Hii leo watu wanawalalamikia viongozi wakuu wa nchi kama rais na waziri mkuu
na hata kuwafungulia mashitaka. Kama hao wanashitakiwa patakuwa na ugumu gani
kuwashitaki waliokuwa wakuu wa Jeshi la Polisi?
Tujifunze kwa tunayoyaona na kuyasikia. Dunia hii ni hadaa na ulimwengu ni
shujaa. Tusikubali kudanganywa na wakati tulionao, tuangalie usoni na kumuoma
Mungu atusaidie na kutupa hatima njema.
Lakini hatma njema hujengwa na mtu mwenyewe na kinachofanywa na jamii baadaye
ni kuitilia mbolea na kupalilia.
Narudia. Tunapaswa kuwa na hadhari na tusijaribu hata wakati mmoja kuzichezea
sheria za nchi. Tukizichezea sheria ipo siku hizo sheria tunazozichezea
zitatugeukia na kutuchezesha shere.
Wakati huo umri wetu utakuwa mkubwa, wengine tukitumia mkongojo kwenda na
kwahivyo kushindwa sio kucheza hiyo shere tu, bali hata kuisikia au kutikisa
mikono, miguu au kichwa.
Chanzo - Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment