Habari za Punde

Uchaguzi mdogo Chambani Juni 16

Na Mwandishi wetu
 
Uchaguzi mdogo katika Jimbo la Chambani, Pemba, unatarajia kufanyika Juni 16, mwaka huu.
 
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Salum Hemed Hamis, kufariki dunia Machi 28, mwaka huu.
Aidha, uchaguzi huo utaenda sambamba na wa madiwani katika Kata 26 za Halmashauri 21, kwa ajili ya kujaza nafasi zilizoachwa wazi kufuatia baadhi ya waliokuwa wanashikilia nafasi hizo kujiuzulu, kufukuzwa, kuhama vyama au kufariki.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jullius Mallaba, uteuzi wa wagombea wa kiti cha ubunge utafanyika Mei 17, mwaka huu, kwa kufuatiwa na kampeni ambazo zitafanyika Mei 18 hadi Juni 15, mwaka huu.
Alisema uteuzi wa uchaguzi mdogo wa madiwani utafanyika Mei 14, mwaka huu, wakati kampeni zitakuwa ni Mei 15 hadi Juni 15, mwaka huu.
Kata zitakazohusika katika uchaguzi mdogo wa Madiwani ni Stesheni (Nachingwea), Nyampu-Lukano na Lugata (Sengerema), Genge na Tingeni (Muheza), Ibugule (Bahi), Langiro (Mbinga), Manchila (Serengeti), Iyela (Mbeya), Mbalamaziwa (Mufindi), Runzewe Mshariki (Bukombe) na Mianzini (Temeke).
Nyingine ni Dalai (Kondoa), Minepa (Ulanga), Makuyuni(Monduli), Bashnet (Babati), Kimandolu, Elerai, Kaloleni na Themi (Arusha), Iseke (Singida), Dongobesh (Mbulu), Ng`ang`ange (Kilolo), Ifakara (Kilombero), Msanze (Kilosa) na Mnima (Mtwara).
Salim Hemed Hamis alifariki dunia katika hospitali ya Taifa Muhimbili alipolazwa siku moja baada ya kuanguka ghafla wakati akishiriki katika vikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
 
Chanzo - Nipashe

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.