Waliberia watua Dar kubadili matokeo
Na Mwandishi Wetu
MECHI ya marudiano ya Kombe la Shrikisho la Soka (CAF) kati ya Azam FC na Barracks Young Controllers II ya Liberia, itachezeshwa na waamuzi kutoka visiwa vya Comoro.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Aprili 6, mwaka huu katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
CAF imeteua Adelaide Ali kuwa mwamuzi wa kati, ambapo mwamuzi msaidizi namba moja ni Amaldine Soulaimane na Ibrahim Mohame atakuwa msaidizi namba mbili.
Mwamuzi wa mezani (fourth official) ni Ansudane Soulaimane.
Kwa mujibu wa taarifa za Shirkisho la Soka Tanzania kupitia kwa Ofisa Habari wake Boniface Wambura, Kamishna wa mechi hiyo itakayoanza saa 10.30 jioni atakuwa Abdelhamid Radwan kutoka Misri.
Katika taarifa hiyo, Wambura amesema maofisa hao wa mechi hiyo watafikia kwenye hoteli ya Holiday Inn.
Wakati huo huo, Barrack Young Controllers II imewasili nchini jana asubuhi kwa ndege ya PrecisionAir ikitokea Nairobi, Kenya ilikotua kuunganisha safari hiyo iliyoanzia Monrovia kupitia Accra, Ghana.
Timu hiyo iliyofikia hoteli ya Sapphire Court, jana jioni ilitarajiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Karume ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake kwa ajili ya mechi hiyo huku wapinzani wao Azam wakiendelea kujinoa kwenye uwanja wao wa Azam Complex.
Azam itashuka dimbani siku ya Jumamosi kuwavaa Waliberia hao, huku ikiongoza kwa mabao 2-1 iliyovuna jijini Liberia wiki mbili na ushei zilizopita, na itahitaji sare tu ili kuweza kusonga mbele kwenye kinyang’anyiro hicho ikiwa timu pekee ya Tanzania iliyobaki kwenye mashindano ya kimataifa.
Simba ya Dar es Salaam na Jamhuri ya Zanzíbar ambazo zote zilishiriki ligi ya mabingwa, zilitolewa na timu za Libolo Recreativo ya Angola na St. George ya Ethiopia mtawalia.
No comments:
Post a Comment