Na Salum Vuai, Maelezo
ILI kuwahamasisha watendaji wa taasisi mbalimbali za umma kujikita katika michezo, Shirika la Save The Children na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), wamekabidhi mipira kwa timu za soka za Benki Kuu (BOT) na kampuni ya simu ya Zantel.
Hafla ya makabidhiano hayo ilifanyika hivi karibuni katika ukumbi wa VIP uwanja wa Amaan, ambapo kila timu ilipata mipira kumi, ambayo inatolewa kupitia mradi maalumu wa kugawa mipira Unguja na Pemba uliozinduliwa Januari 9, mwaka huu na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein katika uwanja wa Amaan.
Wakitoa shukrani zao, nahodha wa timu ya BOT Hamad Mohammed Hamad na Mwenyekiti wa timu ya wafanyakazi wa Zantel Mohammed Ahmed Jaye, walisema msaada huo umekuja wakati muafaka, ikizingatiwa timu hizo zimo katika mazoezi na mechi za kirafiki kujiandaa na mashindano mbalimbali.
Walisema, pamoja na kazi zao za kutoa huduma kwa jamii, wafanyakazi hao pia wanajishughulisha na michezo ili kuiweka miili yao katika afya njema, na kupunguza uzito unaotokana na kukaa muda mwingi katika viyoyozi.
Mwenyekiti wa BTMZ Sharifa Khamis Salim, alisema hatua ya kuzigaia mipira taasisi hizo, ni kuwawezesha wafanyakazi kujishughulisha na michezo kila wanapotaka muda, pamoja na kufikisha ujumbe wa kupinga unyanyasaji na udhalilishaji wa watoto katika jamii.
No comments:
Post a Comment