Habari za Punde

Dk Shein : Rejeeni nyumbani kuongeza kasi ya maendeleo

Wanafunzi wa kitanzania waliopo China wengi wao wakiwa Wanafunzi wanaosomea fani mbali mbali wakimsikiliza kwa makini Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la mapinduzi . Mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Ubalozi wa Tanzania Nchini China katika mji wa Beijing.
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein,akizungumza na Watanzania waliopo Chinawengi wao wakiwa Wanafunzi wanaosomea fani mbali mbali,mazungumzo hayo yalifanyika katika ukumbi wa Ubalozi wa TanzaniaNchini China katika mji wa Beijing.

Na Said Ameir, China
 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka watanzania wanaosoma nje kurudi nyumbani wamalizapo masomo yao ili wasaidie kujenga mazingira mazuri ya kuharakisha maendeleo.
Dk. Shein amesema hayo leo mjini Beijing China wakati alipokuwa akizungumza na watanzania walioko nchini humo mwanzoni mwa ziara yake ya kikazi ya siku saba nchini China.
“Mkimaliza mrudi nyumbani kuitumikia nchi yenu kwa bidii kwani hakuna atakayetujengea nchi yetu” aliwaeleza watanzania hao ambao wengi wao ni wanafunzi katika vyuo mbalimbali nchini humo.
Alifafanua kuwa mipango mikubwa ya Maendeleo ya taifa kama vile Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2020 na Dira ya Mendeleo ya Tanzania Bara 2025 pamoja na mipango ya kupambana na umasikini ya MKUKUTA na MKUZA haiwezi kufanikiwa bila ya jitihada za watanzania wenyewe.


“China ni mfano mzuri kwetu, tujifunze kutoka kwao wanafanya kazi kwa bidii na sasa nchi yao imepiga hatua hadi kuwa nchi ya pili yenye uchumi mkubwa huku ukikua kwa kasi ya asilimia 10 kwa mwaka”alifafanua.
Amewataka watanzania hao kuthamini mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China wa kuwapa fursa za masomo katika nchi hiyo kwa kujifunza kwa bidii ili sehemu ya kuimarisha ushirikiano kati ya China na Tanzania.
“Mwaka jana watanzania 900 walipata nafasi za masomo nchini humu na Serikali ya China imeahidi kutuongezea hivyo tuzitumie vyema fursa hizi kuendeleza nchi yetu”aliwaambia.
Dk. Shein amesema ziara yake nchini China ina lengo la kuimarisha uhusiano mzuri wa kindugu na kirafiki uliopo kati ya Tanzania na China na kwamba ziara kama hizo zinazofanywa na viongozi ni muhimu kuziweka karibu Serikali na wananchi wa Tanzania na China.
Alibainisha kuwa changamoto mojawapo hivi sasa ni kupunguza pengo la kibiashara kati ya nchi mbili ambapo upande wa Tanzania unaagiza zaidi bidhaa kutoka China huku ikisafiri bidhaa chache nchini humu
Kuhusu hali ya uchumi nchini aliwaleza kuwa kwa ujumla uchumi mwelekeo wa uchumi wa Tanzania kwa kuwa umekuwa kwa asilimia karibu 7 mwaka jana kutoka asilimia 6.3 mwaka 2011 huku mfumuko wa bei ukishuka hadi asilimia 6.8 mwaka jana kutoka asilimia 19.8 kmwaka 2011.
“Kwa upande wa Zanzibar mwenendo wa uchumi wetu umekuwa mzuri kwa mfano mwaka 2011/2012 kiwango cha ukuaji kilikuwa asilimia 6.8 na matarajio kwa mwaka 2012/2013 ni asilimia 7 hadi kufikia asilimia 7.5 mwaka 2013/2014”alifafanua.
Juu ya mchakato wa mabadiliko ya Katiba Dk. Shein aliwaeleza watanzania hao kuwa mchakato huo unakwenda kama ulivyopangwa na kuwahakikishia kuwa unafanyika kwa uwazi na kufuata taratibu zilizowekwa za kuendesha mchakato huo.
"Mchakato unaendelea vyema kama ulivyopangwa na Tume inatekeleza majukumu yake kama hadidu za rejea zilizovyoelekeza na inafanya hivyo kwa uwazi "alieleza
Wakati huo huo Balozi wa Tanzania anayemaliza muda wake nchini China Balozi Philip Marmo ameipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kudhamini wanafunzi wengi kuchukua masomo mbalimbali nchini China.
Balozi Marmo alieleza kuwa hivi sasa kuna wanafunzi wa kitanzania wengi nchini humo wakiwemo wanaodhaminiwa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Serikali ya Watu wa Chia na wanaojisomesha wenyewe.
“Tuna wanafunzi 249 wanaosomeshwa kupitia Serikali ya China, 31 wanaodhaminiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wengine wanajisomesha wenyewe” alisema Balozi Marmo ambaye alitoa wito kwa Serikali ya Tanzania nayo kudhamini vijana wake kusoma nchini humo.
Balozi Marmo ambaye katika mabadiliko ya hivi karibuni alimehamishiwa nchini Ujerumani alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na China hivi sasa ni mzuri na kuongeza kuna haja ya kuongeza watumishi katika ubalozi hapa China kwa kuwa kumekuwa na mahitaji mengi kwa vile watanzania wengi hivi sasa wanakuja China kufanya shughuli mbalimbali kama masomo na biashara.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kesho pamoja na mambo mengine anatarajiwa kuwa na mazungumzo rasmi na Rais wa China Bwana Xi Jinping na Makamu wa Rais Bwana Li Yuanchao.

1 comment:

  1. maendeleo hayawezi kupatikana kwa kuwa nyinyi viongozi wenyewe mmeweka mbele maslahi yenu na ya familia zenu , kama uzalendo uanzie kwenu ili muwe mfano kama alivyokuwa mtume saw , yeye alikuwa na mamlaka makubwa na eneo kubwa la utawala hazina yote ilikuwa chini yake , lakini alikuwa akiishi nyumba gani? alipofariki aliacha nini? je alikuwa na mabody gad? jee alikuwa na maeskot akitembea? au akilindwa? kiongozi yoyote aliye mwadilifu haitaji kulindwa wala kuwa na maeskot, huyu ndio mfano wa kiongozi anayetakiwa kuigwa na kila mtu bila kujali dini anayoiamini

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.