Na Said Ameir , Ikulu
Makamu Mwenyekiti wa CCM
Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa viongozi wa chama hicho kuwa na
mpango maalum wa kuelimisha jamii mara kwa mara kuhusu historia na
malengo ya Mapinduzi
matukufu ya mwaka 1964 pamoja na Muungano wa Tanzania wakati wote badala
kulifanya jambo hilo kuwa la msimu.
Dk. Shein ambaye pia ni Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitoa wito huo jana wakati
alipokuwa akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa chama hicho huko
Kinduni Wilaya ya Kaskazini ‘B’ katika mkutano wa majumuisho ya ziara
yake ya kichama
ya siku mbili katika mkoa wa Kaskazini Unguja.
“Tuwe na mpango maalum kwenda
kwa wananchi hasa vijana kuzungumzia Mapinduzi na Muungano wetu isiwe kwa msimu
kwa sababu tunapokuwa kimya tunatoa fursa kwa wengine kusema wayatakayo na
kupotosha umma”alisema Dk. Shein.
Sambamba na wito huo Dk.
Shein aliwataka viongozi hao kuwaelimisha pia wanachama wa chama hicho na
wananchi kwa jumla Katiba na Sheria ili kuwaepusha na kufanya vitendo vya
uvunjaji sheria kutokana na kukosa ufahamu wake.
“Tuwaelimishe wanachama wetu
Katiba na Sheria ili kuwaepusha na kuingia katika matatizo ambayo yanatokana na
kutojua sheria na Katiba ya nchi”alieleza Dk. Shein.
Alifafanua kuwa imedhihiri
katika baadhi ya matukio ya uvunjifu wa amani baadhi ya vijana wameingia kwa
kufuata mkumbo bila kufahamu kuwa wanavunja sheria za nchi na kutahamaki wako
katika mikono ya vyombo vya dola.
Dk. Shein aliwataka viongozi
wa CCM kwenda kwa wananchi kutangaza mafanikio ya utekelezaji wa Ilani ya CCM
ili wasiwape nafasi watu wengine ambao wameamua kujipa sifa ambazo hawastahiki.
Aliongeza kuwa mafanikio hayo
yameifanya Zanzibar kuwa kipenzi cha washirika wa maendeleo ambao wamekuwa bega
kwa bega kusaidia jitihada za Serikali za kuimarisha maendeleo na ustawi wa
wananchi wa Zanzibar.
“Wahisani wetu wameridhika na
jitihada zetu za kuwatumikia wananchi na ndio maana kila mara wamekuwa wakija
nchini kwetu kuzungumza masuala mbalimbali ya ushirikiakiano kati ya nchi yetu
na nchi zao”alisema.
Kwa hivyo aliwahimiza
viongozi kuelimisha wanachama na wapenzi wa CCM juu ya Ilani ya Uchaguzi na
Mwelekeo wa Sera ya Chama hicho kwa miaka 2010 hadi 2020 ili waweze kukieleza
vyema chama hicho mbele ya umma.
Katika mkutano huo Makamu
Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alirejea tena wito wake wa kuwataka wananchi
wasivunje sheria kwa makusudi kwa kujenga hisia kuwa Serikali inawaogopa.
“Watu wanaofanya vitendo
hivyo wasidhani wako juu ya sheria. Ninawakumbusha kuwa hakuna mwananchi aliye
juu ya sheria nikiwemo mimi mwenyewe ninayeongoza Serikali”alisisitiza Dk.
Shein.
Alibainisha kuwa yeye akiwa
Rais anaendesha nchi kwa kufuata Katiba na Sheria ya nchi na kuongeza kuwa
hamuogopi mtu katika kuongoza Serikali lakini anapaswa kumheshimu kila
mwananchi na ndivyo anavyofanya kuwaheshimu wananchi wote.
“Zanzibar kuna Serikali ya
Mapinduzi na inaongozwa na Rais anayetoka CCM. Katika kuiongoza Zanzibar
simuogopi mtu bali namheshimu kila mwananchi kwa kuwa ni wajibu wetu
kuheshimiana” Dk. Shein alieleza.
Makamu Mwenyekiti wa CCM
aliupongeza ushirikiano na mshikamano mzuri wa uongozi baina ya Chama cha
Mapinduzi na Serikali mkoani humo na kutoa wito kuimarishwa zaidi ushirikiano
huo kuongeza ufanisi wa utendaji.
Mapema akizungumza
kumkaribisha Dk. Shein Naibu Katibu Mkuu wa CCM Vuai Ali Vuai alieleza kuwa
katika ziara ya siku mbili mkoani humo Chama cha Mapinduzi na jumuiya zake
kimeweza kuingiza wanachama wapya 4865 miongoni mwao 2996 ni wa CCM na 1869 ni
wa jumuiya zake.
Vuai alimshukuru Dk. Shein
kwa kueleza kwa uwazi na kutetea Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964 na
Muungano ambapo alitoa wito kwa viongozi
wengine wa chama hicho wakiwemo mawaziri, wabunge, wajumbe wa Baraza la
Wawakilishi pamoja na madiwani kuyazungumzia masuala hayo kama ambavyo Makamu
Mwenyekiti amekuwa akifanya.
Katika ziara hiyo ya chama
ambayo ni ya kwanza tangu achaguliwe kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa
CCM Zanzibar Dk. Shein aliweka mawe ya msingi ya majengo ya ofisi za chama
hicho ngazi ya matawi na jimbo pamoja na maskani.
Dk. Shein anatarajiwa
kuwasili kisiwani Pemba Jumapili ambapo Jumatatu ijayo atazindua mbio za Mwenge
wa Uhuru katika sherehe zitakazofanyika huko katika kijiji cha Chokocho Wilaya
ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba na baadae kuendelea na ziara ya kichama katika
mikoa miwili ya Pemba kuanzia Jumanne ijayo.
nenda zzako huko , kaburi liko karibu linakusubiri na adhabu kali ya Mungu kwa unafiki wako huo bado unazungumza habari za mapinduzi feki na muungano wa dhuluma , humwogopi Mola? au unafikiri una veto?
ReplyDelete