Risala ya Jumuiya Ya Waajiri
(ZANEMA) Katika Kuadhimisha
Siku Ya
Wafanyakazi Duniani (May Day) Zanzibar
Uwanja wa
Amaan Zanzibar
1/05/2013
Mh. Mgeni Rasmi, kwa niaba ya Jumuiya Ya Waajiri
Zanzibar,(ZANEMA) naomba nitowe shukrani zangu za dhati, kwa Shirikisho la
Vyama vya Wafanyakzi Zanzibar (ZATUC) kwa kutualika katika kuadhimisha siku ya
wafanyakazi duniani. Kwetu sisi waajiri, hii ni heshima kubwa na dalili tosha
kuwa kuna ushirikiano mkubwa baina ya waajiri na vyama vya wafanyakazi
Zanzibar.
Mh. Mgeni Rasmi, Wafanyakazi wa Zanzibar leo wana
ujumbe wao unaosema
“Katiba
mpya izingantie usawa wa haki na maslah ya wafanyakazi”
Ni haki yao
kudai. Ni haki yao kupata maslah bora. Lakini ni wajibu wao vilevile
kufanyakazi kwa ufanisi na tija. Ujumbe wa ZATUC kwa kuitaka katiba izingatie
haki na maslah maana yake wanataka majadiliano na mapatano sio nguvu wala
mapambano. Hili niwapongeze kwa kuchaguwa njia muafaka wa kutaka madai yao
yafikiriwe.
Suala hili la wafanyakazikudai haki zao halikuanza
leo, Miaka 124 (1889) iliyopita, kule Marekani , Chicago wafanyakazi walidai
haki na maslah lakini njia iliyotumika ilisababisha watu kadhaa kupoteza maisha
yao .
Hiyo ni historia, haisahauliki na hatutaki
tuirejee. Waajiri wa leo wanaamini
kuwa majadiliano sehemu ya kazi ( social diologue) ndio suluhisho la matatizo sehemu ya kazi.
Shirika la Kazi Duniani limejitahidi sana kuweka
misingi na haki sehemu za kazi kwa kupitisha mikataba na maazimio yake. Mikataba
miwili muhimu ambayo nchi nyingi duniani zimeridhia ni Mikataba namba 87 na 98 juu
ya Haki Ya Kujiunga na Majadiliano“freedom of Association and Collective
Bargaining”
Waajiri wanakubaliana na wazo hilo. Hata hivyo
katika katiba ya Jamhurri ya Muungano ya Tanzania ibara ya 20 na ile ya Zanzibar ibara ya 20 zote
zimetowa fursa kubwa juu ya wafanyakazi kujiunga na kudai maslah mazuri
kutokana na kazi zao.
Lakini Mheshimiwa mgeni
Rasmi wafanyakazi wasisahau kuwa siku zote haki na maslah bora sehemu ya kazi
ni pamoja na wajibu wao wakiwa kazini . Kama tungeruhusiwa waajiri kuongeza
neno katika ujumbe wa Vyama vya Wafanyakazi, waaliongeza kitu Katiba mpya izingantie usawa wa haki , maslah
na wajibu wa wafanyakazi.”
Kumtaka muajiri aweke
maslah bora pahala ambapo hapana uzalishaji wenye tija ni mtihani.
Mh, hayo ni ya wafanyakazi
ambao sasa hivi wamo kwenye ajira. Lakini katika kuwasikiliza vilio vya
wafanyakazi wenye ajira lazima tuende samamba na kuliangalia kundi jengine.
Kuna kundi la vijana ambao hawana ajira ambalo linajumuisha
1. Vijana wanawake kwa wanaume
waliomaliza masomo yao, lakini hawana ajira
2. Vijana wenye ujuzi lakini
bado hawajaajiriwa na bahati mbaya
hawajajiajiri kwa matatizo mbali mbali ikiwemo mitaji
3. Kuna watu tayari wanazo
ajira lakini uwezo wao wa kufanyakazi ni mdogo kitaaluma. Uwezekano wa kukusa
ajira zao ni mkubwa.
Tatizo hili ni la dunia,
tusilidharau hata kidogo. Migogoro mingi inayotokea duniani leo chanzo kikubwa
ni vijana kukosa ajira.
Katika mkutano wa 101 uliofanywa
kule Geneva mwaka 2012 Shirika la Kazi duniani lilitilia mkazo suala zima la
ajira kwa vijana na waajiriri walitakiwa kushirikiana kiamilifu katika
kupambana na tatizo hili. Mambo
yafuatayo yalitiliwa mkazo zaidi
·
Uajiri na
sera za uchumi
·
Uajiri,Elimu,
Mafunzo na Ujuzi
·
Ujasiriamali
na kuajiajiri wenyewe
·
Sera juu
za Soko la ajira
Waajiri tunalitilia mkazo
suala hili kwasababu kama suala hili litapata ufumbuzi , waajiri wataweza
kuwaajiri wazalendo wengi zaidi jambo ambalo litaondoa gharama za kuchukuwa
wafanyakazi, wa baadhi ya fani, nje ya nchi jambo ambalo kwetu ni gharama.
Mheshimiwa tusikatae
ukweli , tuna ajira hazina watu na (ujuzi na uwezo wa watu wetu) na wakati
huohuo tunawatu hawana ajira (kwa maana ya watu wetu hawana ujuzi) . Hili ni
tatizo lazima litafutiwe ufumbuzi.
Mheshimiwa Mgeni rasmi
sisi Waajiri tungefurahi sana kuona ajira zote zinachukuliwa na wazalendo
lakini tujiulize ni kweli kila ajira inaweza kuchukuliwa na kila mtu bila
kuzingatia ujuzi na uwezo?
Waajiri tunajuwa, kuwa
sasa muelekeo wa Serikali ni kuanzisha viwanda kama njia moja ya kuongeza pato
la nchi na ajira . Tarehe 19 January 2013. Mh Raisi wa Zanzibar ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Biashara Zanzibar
ilisisitiza kuwa sasa tunaelekea kwenye viwanda na hatuna mzaha kwa hili.
Ni kweli sasa Zanzibar
inataka kuikuza sekta ya Viwanda . lakini pakuanzia ni wapi? Mara nyingi
tunahesabu
1. Kwanini viwanda vilikufa Zanzibar?.
2. Uongozi, Ujuzi, uzowefu ,
fedha na vianzio vyake
3. Mitaji, Zana na vifaa
4. Hali ya uwekezaji
5. Umeme, maji,miundo mbinu
6. Masoko na viwango
7. leseni na makodi makubwa, nk
Haya ni muhimu sana lakini
suala moja bado halijapewa uzito nalo ni muhimu, ni suala zima la Raslimali
watu na Ujuzi (Human Capital).
Hatuwezi kuiedeleza sekta
yoyote ile kama hatujaamua kwa makusudi kukuza raslimali watu. Serikali na
sekta binafsi tushirikiane kuwaendeleza vijana ili waajirike katika sekta hii
vyenginenevyo, tutaendelea kuunda ajira
zisizokuwa na watu, wakati tukiwa na watu wasiokuwa na ajira.
Mheshimiwa, Tunaishi
katika dunia ambapo kuna mashindano makubwa ya
·
uzalishaji,
·
mitaji,
·
uwekezaji,
·
teknologia na
·
soko la ajira .
Haya yote kwa pamoja
yanachangia ajira iweje na maslah ya muajiri pamoja na wafanyakazi. Tunataka
watu watakaoweza kupambana na hali hii.
Tumo ndani ya Soko la
pamoja la Afrika ya mashariki ambapo 2010 tumeridhia uingiaji wa watu na bidhaa
katika nchi zetu.Katika hali hiyo waajiri bado tunakabiliwa
na mtihani mkubwa katika ngazi
zote, juu ya nani wamuajiri.
Mheshimiwa kwa kutaka
mambo yaende vizuri Waajiri wote wanachangia 5% ya mishahara ya wafanyakazi
wote ili kusaidia vijana wetu kupata mafunzo ya amali ili waajirike na kuweza
kuingia katika soko la ajira. Lakini sisi waajiri bado tuna maswali mengi.
a. Kiasi cha fedha
zinazokusanywa ni kikubwa mno,kwa kuendeleza vyuo vya amali, lakini waajiri bado
hawajaekewa wazi hadi hii leo wamechangia kiasi gani.
b. Hatuja ekewa wazi matumizi
ya fedha hizi na mipango ya baadaye.
Kwa kuzingatia hayo na
mengineyo Waajiri Tunashauri:
1. Kuangalia upya Uajiri na sera za uchumi.
2. Iko haja ya Uajiri, Elimu, Mafunzo na Ujuzi yawekewe
mikakati ya hali juu.
3. Serikali ishirikiane na
Waajiri na wadau wengine waipitie mitaala yetu ili iweze kuzalisha vijana
kulingana na soko la ajira
4. Serikali kuweka mazingira
rafiki kwa waajiri kupunguza msururu na ukubwa usumbufu wa kodi, bei za umeme, maji, leseni, ushuru nk
na kuwa na kituo kimoja cha mambo ya leseni na kodi (one stop centre) ili Waajiri wapunguziwe
usumbufu wa kumjuwa nani ana dhamana gani.
5. Taaluma za ujasiriamali na
ujuzi zifanane na mahitaji ya masoko.
6. Serikali ianzishe Viwanda au iwakaribishe
wawekazaji sambamba na kupanua Kilimo cha kisasa na cha kibiashara
ambavyo vitaweza kutowa nafasi za ajira na kukuza uchumi.
7. Iko haja Kwa Wizara zote
na taasisi zote za Serikali na Watu Binafsi kwa pamoja kuifanya zanzibar kuwa
nikituo kikubwa cha uwekazaji na biashara.
Kwa mujibu wa takwimu za
utafiti juu ya uchumi wa Zanzibar mwaka 2011, waajiri binafsi wameajiri
wafanyakazi 15,620 kati ya hao wanaume ni 10,778 na wanawake 4,08423. Huu ni
mchango mkubwa wa waajiri kwa nchi yetu.
Mwisho kabisa, naomba
nitowe wito kwa wale ambao hawataki kufahamu au pengine hawajui, kuwa waajiri,
kushiriki katika mambo yanayohusu, mipango, majadiliano, sera, sheria,
maazimio, mikataba na mengineyo yanayohusiana nayo, ya kitaifa na kimataifa
kuhusu kazi na ajira ni haki yao si fursa au upendeleo.
Ahsanteni
kwa kunisikiliza.
Salahi Salim Salahi
Mkurugenzi Mtendaji
Jumuiya Ya Waajiri Zanzibar
(Zanzibar Employers Association) ZANEMA
Tel. +255 0242236921
Mobile: 0777424797
No comments:
Post a Comment