Joseph Ngilisho,Arusha
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arusha mjini, Jublet Shiletiwa Kileo (65) amefariki dunia ghafla nyumbani kwake Kaloleni jijini Arusha jana asubuhi.
Kileo katika kipindi cha uhai wake alikuwa mfanyabiashara maarufu jijini Arusha, akimiliki biashara mbalimbali na mwanasiasa nguli aliyekitumikia chama tangu enzi za mwalimu Nyerere na kushika nyadhifa mbalimbali.
Akizungumzia kifo cha kaka yake, Humphrey Kileo, alisema kaka yake aliamka vizuri jana asubuhi na kwenda kuzima taa za nje na hakuwa na matatizo yoyote ya kiafya.
Kileo alisema alipokuwa sebuleni ghafla alimwita na alipokwenda alimkuta ameanguka na alimpa mkono na kumtaka kuangalia watoto na hapo hapo aliaga dunia.
Alisema kaka yake amefariki kwa shinikizo la damu na hakuwa na ugonjwa wowote, kwani juzi walikwenda kanisani na kurudi na asubuhi ya jana, alikuwa mzima wa afya.
“Ndugu yangu amefariki dunia katika mazingira ya kuhuzunisha na kusikitisha sana, kwani hakuwa na ugonjwa wowote na ameacha pengo kubwa mno katika familia yetu,”alisema.
Kileo alisema mazishi ya kaka yake, yatafanyika mahali alipozaliwa katika kijiji cha Nkuu Nkweshoo, kilichopo Machame wilayani Hai Mkoani Kilimanjaro.
Marehemu Kileo ameacha mke na watoto saba, wakiwemo wanaume watatu na wanawake wanne na wajukuu na vitukuu kadhaa.
Alikuwa Mwenyekiti wa CCM Arusha kwa miaka 12 na pia alikuwa Diwani wa kata ya Kaloleni, kwa miaka 10 kabla ya kuangushwa mwaka jana, katika uchaguzi mkuu wa chama uliopita.
No comments:
Post a Comment