Na Mwandishi wetu, Dodoma
SPIKA wa Bunge, Anne Makinda amewaonya Wabunge akisema bunge si sehemu ya kugombanisha wananchi na serikali bali ni taasisi ya kuisimamia serikali.
Makinda alitoa kauli hiyo jana jioni wakati akitangaza uamuzi wa Kamati ya Kanuni ya Bunge kuhusu hotuba ya bajeti ya kambi ya upinzani ya Wizara ya Habari, Vijana na Michezo.
Mapema asubuhi, Spika Makinda alisitisha kusomwa hotuba ya kambi ya upinzani ya Wizara hiyo, baada ya Mbunge wa Jimbo la Mbozi Mashariki, Godfrey Zambi, kusimama kwa mujibu wa kanuni 68(1) na 64A kuomba mwongozo wa Spika akitaka hotuba hiyo isisomwe kwa sababu imejaa uchochezi.
Zambi alisema mambo yanayozungumzwa ndani ya hotuba hiyo iliyosomwa na Waziri kivuli wa wizara hiyo, Joseph Mbilinyi (Sugu) kuanzia ukurasa wa 1 hadi 14 imejaa uchochezi na kauli zinazotolewa na msemaji wa kambi hiyo kuhusu serikali ya CCM ni nzito na haziwezi kunyamaziwa.
Katika hotuba yake, Sugu alisema serikali inakandamiza uhuru wa habari kwa kuwateka nyara wanahabari, kuwang’oa kucha, kuwang’oa meno na kuwaua.
“Wapi serikali ya CCM imewaua, imewang’oa kucha na kuwatesa wanahabari? Mheshimiwa tusikubali hotuba kama hizi ziletwe bungeni na kusikilizwa na wananchi.Naomba kutoa hoja taarifa hii isitishwe, iende kuandikwa upya,” alisema Zambi.
Baada ya ombi hilo, Spika Makinda alisimama na kuwambia Wabunge kwamba hivi karibuni walipitisha azimio la kutotoa kauli za uchochezi bungeni.
Kutokana na kauli hiyo, Spika Makinda alitangaza kusitisha shughuli za bunge hadi saa 11:00 jioni jana na kuitaka Kamati ya Kanuni ikae ijadili hotuba hiyo kabla ya kusomwa tena.
Akitoa uamuzi wa Kamati jana jioni, Makinda aliiagiza kambi ya upinzani kuondoa katika hotuba yake masuala yanayohusu mauaji ya mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Chanel Ten, Daud Mwangosi, ili kulinda hali ya kuingiliana kimajukumu kati ya muhimili wa Bunge na Mahakama kwa kuwa suala la mauaji ya mwanahabari huyo liko mahakamani.
Aidha aliagiza maneno yaliyomo kuanzia ukurasa wa 1-14 yaondolewe.
“Kwa madhumuni ya uendeshaji wa shughuli bora za bunge tumefanya majadiliano ili kupitia kwa kina maelezo yaliyomo kwenye kurasa hizo kuingiliana mhimili wa bunge na mahakama na kuondoa lugha za uchochezi,” alisema Spika Makinda.
Lakini hata pale, Sugu alipopewa nafasi ya kuendelea kusoma hotuba yake, bado majina ya Daud Mwangosi yaliendelea kujirudia.
Hata hivyo, Makinda alifafanua akisema hotuba ya kambi ya upinzani ya wizara hiyo haikurikodiwa.
Mapema akiwasilisha hotuba ya Wizara ya Habari, Vijana na Michezo, waziri wa wizara hiyo, Dk. Fenella Mukangara, alisema serikali inajiaanda kuwa na sheria ya habari na kuimarisha matangazo ya TBC.
No comments:
Post a Comment