Habari za Punde

Kamisheni ya Atomiki yawatoa hofu watumiaji simu


Na Ameir Khalid
KAMISHENI ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imeeleza kuwa hakuna athari zozote zinazotokana na mionzi ya simu za mikono na minara ya simu iliyojengwa karibu na makaazi ya watu.

Akiwasilisha mada katika warsha ya siku moja kwa waandishi wa habari na wahariri, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia, Dk. Mwijarubi Nyaruba, alisema hakuna madhara yoyote katika matumizi ya simu za mikononi kwa afya za binadamu, licha ya baadhi ya watu kujenga hofu kubwa juu ya hatima zao kiafya zinazotokana na matumizi ya simu.

Alisema katika utafiti uliofanywa na taasisi hiyo, umebaini kuwa simu za mkononi hazina madhara ya aina yoyote, katika mfumo mzima wa afya ya binadamu, hivyo wananchi wanapaswa kuondoa hofu, na kama wana wasiwasi ni vyema wakapunguza matumizi ya simu za mkononi.


“Utafiti ambao ulifanyika kwa baadhi ya mikoa ya Zanzibar na Tanzania Bara umebaini kuwa simu za mikononi hazina madhara ya aina yoyote, lakini kama mwananchi ana wasiwasi juu ya hili, basi ni vyema akapunguza matumizi ya simu, au kuweka sauti ya wazi,” alisema.

Kuhusu minara iliyojengwa karibu na makaazi ya watu, alisema asili ya minara haitoi mionzi kama watu wanavyodhani, badala yake kinachotoa mionzi ni antena zinazofungwa kwenye minara hiyo, hivyo alisema hakuna athari yoyote kwa wananchi kupitia minara hiyo.

Alisema zipo taarifa zinazoenezwa mitaani kuwa matumizi ya simu za mikononi na minara hiyo inasababisha kansa, suala ambalo katika utafiti uliofanywa hakuna ushahidi wowote wa jambo hilo.

Hata hivyo, aliwashauri wananchi kuhakikisha wanafuata ushauri unaotolewa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), katika kuondosha wasiwasi juu ya matumizi ya simu za mikononi.

Mapema akifungua warsha hiyo, Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano, Issa Haji Ussi ‘Gavu’, alisema sekta ya mawasiliano nchini imepiga hatua kubwa ambapo hivi sasa Zanzibar inakadiriwa kuwa na minara 200, huku vyombo vya vituo vya redio na television navyo vikiongezeka kwa kasi.

Alisema kutokana na wananchi wengi kujenga hofu ya maisha yao juu ya matumzi ya minara na simu za mikononi, ni vyema kwa taasisi hiyo kufanya utafiti wa mara kwa mara kwa simu, ili kuwaondoshea hofu wananchi.

Akifunga warsha hiyo Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Issa Mlingoti, alisema simu za mkononi na minara yake hutoa kiwango kidogo cha mionzi,ingawa wanasayansi wametoa matokeo ya utafiti yanayoonesha kiwango fulani cha athari ya matumizi ya simu za mkononi, lakini athari hizo ni ndogo na hazina madhara kwa afya ya mwanadamu.

Alisema viwango vya mionzi kutoka vyombo vya mawasiliano vimepimwa kwenye miji ya Dar es Salam, Arusha, Mwanza, Mbeya na Unguja, ambapo kwa Unguja pekee vipimo vilifanyika katika wilaya zote sita katika maeneo 15.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.