Na Ali Haji, Pemba
WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali,Ali Juma Shamuhuna, amewataka Walimu Wakuu Wilaya ya Wete,kubadili mwenendo mbaya wa utendaji wao wa kazi na badala yake wazidishe usimamizi kwa walimu walio chini yao kama njia ya kuepuka aibu ya matokeo mabaya katika skuli zao.
Alisema pamoja na ukweli kwamba matokeo mabaya ya mitihani yamesababishwa na mambo mengi lakini sababu mojawapo ni kukosekana usimamizi thabiti wa Walimu Wakuu kwa walimu walio chini yao.
Shamuhuna, aliyasema hayo jana katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu cha Benjamin Mkapa Wete,alipokuwa akizungumza na Walimu Wakuu na Wasaidizi wao, Wenyeviti wa Kamati za skuli,Madiwani na Masheha ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku nne kisiwani Pemba ya kuzungumza na wadau wa elimu.
Alisema kuoneana muhali kunakoendelezwa na Walimu Wakuu,kunasababisha walimu kuchelewa kufika kazini licha ya kwamba wanalipwa nauli.
Aidha alisema hali hiyo inasababisha utoro wa walimu na hivyo kunapelekea kutokukamilika mitaala wakati wa kufundisha.
“Inashangaza kwamba pamoja na bajeti kubwa tunayotumia kulipia nauli za walimu bado walimu wanachelewa kazini kwa kusubiri msaada, kusubiri magari ya mawe na gari nyengine za panda shuka,”alisema Shamuhuna.
Akitoa taarifa ya Elimu ya Wilaya ya Wete, Afisa wa Elimu wa wilaya hiyo, Khamis Said Hamad, alisema wilaya yake inakabiliwa na upungufu wa zaidi ya walimu 150 wa skuli za msingi.
Wilaya ya Wete ina skuli za msingi 21 na msingi na kati nane 8 zenye wanafunzi 22,289 wanaofundishwa na walimu 470.
Afisa wa Elimu hiyo, alisema upungufu huo inawezakana ndio uliosababisha kushuka kiwango cha ufaulu wa mitihani ya darasa la saba 7 ambapo wilaya ya Wete katika mitihani ya mwaka 2012 ulishuka kutoka na nafasi ya kwanza ulioizoea hadi nafasi ya nne.
Afisa huyo aliuelezea upungufu huo wa walimu kuwa mkubwa zaidi katika skuli zilizoanzishwa hivi karibuni zikiwemo skuli ya Kokota, Finya na Mkota.
Akizungumzia ujenzi wa madrasa mpya, alisema wananchi katika wilaya ya Wete wameonesha mwamko mkubwa kujitolea kwenye ujenzi wa madrasa.
Alisema mpaka sasa wilaya ya Wete ina majengo 13 yaliojengwa kwa nguvu za jamii ambayo yana vyumba vya kusomea 57 lakini majengo hayo hayajakamilika kwa sababu yanasubiri nguvu za wizara kukamilika kwa sehemu zilizobakia ikiwa ni pamoja na kuezeka.
Akitoa mchango wake katika mkutano huo, Mwalimu Mkuu wa skuli ya Mzambarauni aliiomba Wizara ya Elimu kuipitia upya sera yake mwaka 2006 kwa vile baadhi ya vipengele vyake vimekwamisha maendeleo ya elimu.
Alitoa mfano wa maelekezo yanayowataka wanafunzi ya darasa la kwanza kusoma hadi darasa la nane ambayo yamewapa mzigo mkubwa zaidi watoto hao na hayawasaidii kama ilivyokusudiwa.
Aidha, alitoa wito wa kuangalia zaidi maslahi ya walimu hasa walimu wazoefu ambao mishahara yao imepunguzwa kwa mabadiliko mapya ya muundo wa utumishi ambayo kimsingi wao hayawahusu.
No comments:
Post a Comment