Habari za Punde

Kamati za BLW kuanza kazi wiki ijayo


·      Maafisa wa Serikali waombwa kuzipa ushirikiano

·      Wajumbe wahaha  uwenyeviti wa Kamati hizo.

·      Wenyeviti kujulikana wiki ijayo

·      Hamza kuongoza tena Kamati ya Afisi za viongozi.

Na Himid Choko, BLW
Kamati za Kudumu za Baraza la Wawakilishi zitaendelea na kazi zake za kawaida kuanzia Mei 13 hadi Mei 24 2013.

Katibu wa Baraza la wawakilishi la Zanzibar, Yahya Khamis Hamad  amesema  Kamati ya Kusimamia Afisi za  Viongozi Wakuu wa Kitaifa na Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala,  Kamati  ya Kuchunguza  na Kudhibiti  Hesabu za Serikali na Mashirika  (PAC), pamoja na Kamati ya Fedha , Biashara na Kilimo zitafanyakazi zake  Unguja.

Aidha ndugu Hamad  amezitaja Kamati zitakazofanya kazi zake Pemba  kua ni Kamati ya Ujenzi na Mawasiliano, Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii pamoja na  Kamati ya Mifugo, Utalii , Uwezeshaji  na Habari.

Amesema Miongoni mwa  kazi zitakazofanywa na Kamati hizo ni  Uchaguzi wa Wenyeviti  na Makamo wenyeviti wa Kamati hizo pamoja na Kufuatilia  Utekelezaji wa Bajeti ya Kila Wizara na taasisi zake kwa Kipindi cha Januari- Machi 2013.

Wakati huo huo katibu huyo wa  za Baraza la Wawakilishi amewaomba maafisa na watendaji wa kila wizara Wizara  na taasisi zao kutoa mashirikiano  ya kutosha kwa Kamati hizo ili kuweza kufanikisha vyema majukumu ya Kamati hizo .


Amesema Kamati hizo zimeundwa kihalali kutafuta taarifa zitakazoliwezesha Baraza la Wawakilishi ambalo ndio chombo chenye uwakilishi  wa moja kwa moja wa wananchi kuweza kusimamia vyema  utendaji wa shughuli za serikali.

“Kwa msingi huo , watendaji wa Mawizara wana jukumu la kutoa taarifa sahihi  juu ya mambo  wanayoyashughulikia  katika utumishi wote wa umma ili kuwawezesha  wananchi kupitia wawakilishi wao  kujua mambo yanayofanywa kwenye   Mawizara  ya serikali kwa maslahi yao” alisisitiza Katibu huyo wa Baraza la Wawakilishi.

Amesema hiyo ndio dhana kubwa  inayojenga wajibu wa Serikali na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuhusiana na haki za Kamati.

Kwa mujibu wa kifungu cha 88 (d) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 Miongoni mwa kazi za Baraza la Wawakilishi ni kuidhinisha na kusimamia mipango ya maendeleo ya Serikali  katika njia ile ile ambayo Bajeti ya mwaka inaidhinishwa.

 

 

Hata hivyo  amesema  Kamati ya Viongozi Wakuu wa Kitaifa tayari  imeShafanya Uchaguzi  kwa Dharura Maalum na kumrejesha tena Mheshimiwa Hamza Hassan Juma (Kwamtipura)  kuendelea kuwa  Mweyekiti wa kamati hiyo.

Aidha  Kamati hiyo  imemchagua Mheshimiwa Saleh Nassor Juma (Wawi) kuwa Makamo mwenyekiti wa kamati hiyo.

Mapema Mwezi uliopita Spika wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, Mheshimiwa Pandu  Ameir Kificho  aliZIpanguwa    Kamati za Kudumu za Baraza hilo na kuzipanga upya .

 Wajumbe hao wapya watazitumikia Kamati hizo kuazia Mwezi Mei 2013 mpaka kuvunywa kwa Baraza   hapo mwaka 2015.

Kwa upande wa Kamati ya Kusimamia Afisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa ni  Hamza Hassan Juma (Kwamtipura), Subeit Khamis Faki (Micheweni), Ali Mzee Ali ( Kuteuliwa) , Shadya Mohammed Suleiman ( Viti Maalum), Makame Msimba Mbarouk (Kitope),  Saleh Nassor Juma (Wawi) na Ashura Sharif Ali (Viti Maalum).

Kwa Upande wa  Kamati ya  Katiba , Sheria na Utawala  ,  walioteuliwa ni Mansour Yussuf Himid ( Kiembe Samaki), Wanu Khafidh Ameir (viti Maalum) , na Suleiman Hemed Khamis  (Konde). Wengine ni Abdullah Juma Abdullah (Chonga) , Bikame Yusuf Hamad (Viti Maalum) na Nassor Salin Ali (Rahaleo). Kamati hii hapo kabla ilikua ikiongozwa na Mwakilishi wa Mfenesini ALI Abdullah Ali.

Aidha katika uteuzi huo Mwakilishi  wa Mji Mkongwe Ismail Jussa Ladhu  amehamishwa kutoka Kamati yake ya awali ya Katiba, Sheria na utawala  na sasa anatumikia   Kamati ya Mawasiliano na Ujenzi . Wengine walioteuliwa  kuunda Kamati ya hii ni Marina Joel Thomas ( Kuteuliwa), Mohamed Haji Khalid (Mtambile) , Hussein Ibrahim Makungu (Bububu), Mahamoud  Moh,d Mussa (Kikwajuni) , Salma Mohammed Ali (Viti Maalum) na Mheshimiwa Panya Ali Abdullah ( Viti Maalum). Kamati hii ilikuwa ikkua ikiongozwa na Makame Mshimba Mbarouk (Kitope)

Kwa upande wa Kamati ya Maendeleo ya Wanawake na Ustawi wa Jamii  ambayo ilikuwa ikiongozwa na Amina Idd Mabrouk ( Viti Maalum ) sasa inaundwa  na Mgeni Hassan Juma ( Viti Maalum), Mwanaidi Kassim Mussa (Viti Maalum), Hassan Hamad Omar (Kojani), Farida Amour  Mohammed ( Viti Maalum), Addi Mossi Kombo (Matemwe), Ali Salum Haji (Kwahani) na Mohammed Mbwana Hamad (Chambani).

Aidha katika uteuzi huu Mheshimiwa Spika amewabakisha  Omar Ali Sheikh (Chake Chake), Mbarouk Wadi Mtando (Mkwajuni), Shamsi Vuai Nahodha (Mwanakwerekwe), Fatma Mbarouk Said (Amani) kuwa Wajumbe wa Kamati ya Kuchunguza na Kudhibiti  Hesabu za Serikali na Mashirika (PAC). Wengine walioteuliwa katika Kamati hiyo ni Rafai Said Rufai (Tumbe), Mwajuma Faki Mdachi (Viti Maalum) na  Salma Mussa Bilal (Viti Maalum) na Salim Abdullah Hamad (Mtambwe). Kamati hio ilikua ikiongozwa na Omar Ali Shehe.

 Wanaounda Kamati ya Fedha, Biashara na Kilimo ni pamoja na Salmin Awadh Salmin (Magomeni), , Hamad Masoud Hamad (Ole ), Viwe Khamis Abdullah (Viti Maalum), Asha Abdu Haji (Viti Maalum), Hija Hassan Hija (Kiwani) na Raya Suleiman  Hamad ( Viti Maalum), na  Jaku Hashim Ayoub (Muyuni).

Katika Kamati ya Mifugo, Utalii na Uwezeshaji na Habari walioteuliwa ni Asha  Bakari Makame (Viti Maalum) ambae alikua mwenyekiti wa Kamati hiyo hapo kabla, Mlinde Mabrouk Juma (Bumbwini) na Kazija Khamis Kona ( Viti Maalum). Wengine ni Asaa Othman Said (Wete), Abdullah Mohammed  Ali (Mkoani), Amina Iddi Mabrouk (Viti Maalum), Mussa Ali Hassan ( Viti Maalum) na Mohammedraza Hasanali Dharamsi (Uzini).

Habari kutoka ndani ya Baraza  Wawakilishi zinasema kwamba  wajumbe wengi wamekuwa wakihaha na kupiga kampeni za chini kwa chini huku wakionyesha nia ya kugombea nafazi za uongozi wa Kamati hizo.

Wenyeviti na Makamo wenyeviti wa Kamati zote watajulikana wiki ijayo baada ya kamati hizo kufanya uchaguzi wa viongozi wao.

 

 
 

 

 

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.