Habari za Punde

Mpango wa ujenzi wa viwanja vya Mnazimmoja kulikoni?

Na Salum Vuai
 
YAPATA miaka miwili sasa, tangu tuliposikia kuwa serikali kupitia Baraza la Manispaa Zanzibar ina mpango wa kuvifanyia matengenezo makubwa viwanja vya michezo Mnazimmoja ili kuzuia kutuwama kwa maji.
 
Ni jambo linaloeleweka kuwa, kutokana na maumbile na hali ya kijiografia ya viwanja hivyo, vimekuwa na kawaida ya kutuwama maji kila msimu wa mvua unapofika hali inayoleta usumbufu. Viwanja vya Mnazimmoja ambavyo ni maarufu kwa shughuli za michezo, vinafahamika kwa kuwa tangu zamani hata kabla ya Mapinduzi ya 1064, vimekuwa vikikusanya vijana wa timu mbalimbali kuonesha vipaji vyao na kuvikuza.
 
Kila wakati wa asubuhi na jioni, vijana kutoka maeneo mbalimbali ya manispaa wanamiminika viwanjani hapo kufanya mazoezi na kujiendeleza kimichezo.
 
Lakini harakati hizo husita kila msimu wa mvua unapofika na hivyo kuwakosesha wanamichezo fursa ya kufanya mazoezi au kucheza mechi zao za kirafiki na za kimashindano.


Kwa kuwa serikali inatambua tatizo hilo, ndipo ilipokuja na mpango unaotarajiwa kulimaliza nalo ni kutumia utaalamu wa ndani na nje ili kutafuta njia ya kuzuia maji yasiendelee kutuwama viwanjani hapo.
 
Ingawa tunafahamu kuwa ‘mambo mazuri hayataki haraka’, lakini pia tukumbuke kwamba ‘ngoja ngoja nayo huumiza matumbo’. Tunaelewa kuwa ni kweli serikali imedhamiria kutekeleza mradi huo mkubwa ambao kama utafanikiwa, utakuwa umewakomboa vijana wanamichezo wanaovitumia viwanja vya Mnazimmoja, na kuwa huru kufanya mazoezi kwa muda wote.
 
Lakini ni muda mrefu umepita bila kusikia maendeleo ya mpango huo na hatua iliyofikiwa katika kutafuta wafadhili watakaoshughulikia mradi huo.
 
Kila siku zikienda, viwanja hivyo vinazidi kupoteza haiba yake kwani mbali na kujaa maji wakati wa mvua, pia kumeibuka tabia ya kuchoma moto nyasi zake kunakofanywa na watu badala ya kufyeka kwa kutumia mapanga.
 
Kwa mtu anayevijua viwanja hivyo ambaye ameondoka nchini kwa miaka mingi iliyopita, kama atakuja leo Zanzibar na akatembelea viwanjani hapo, hatakosa kushangaa kutokana na hali ilivyo sasa. Kwa kuwa muda mrefu umepita baada ya kauli ya serikali kwamba inatafuta namna ya kujenga miundombinu itakayosaidia kuvinusuru viwanja hivyo, tunadhani iko haja sasa kwa mamlaka husika kuvunja ukimya na kueleza kinachoendelea.
 
Sote tunajua kuwa, ili kuleta maendeleo michezoni, viwanja ndio nyenzo muhimu kabla vifaa vyengine. Kwa hivyo, kwa kuwa wanamichezo wamesubiri sana, tunadhani huu ni wakati wa kulivalia njuga suala la kuvitengeneza viwanja hivyo, ili kukidhi mahitaji ya vijana katika kujiendeleza kimichezo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.