Na Kija Elias, Moshi
MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC-CCM) na Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa amewataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi kuwa na utaratibu wa kukosoana pindi wanapokosea badala ya kusubiri vyama vingine viwasemee.
Hayo aliyasema jana mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akikabidhi kadi kwana wanachama wapya 155 kwa tawi jipya la Chuo Kikuu cha Ushirika na Biashara (MUCCOBS).
Silaa alisema kumekuwa na tabia ya viongozi wa CCM, kulalama na kuonea aibu hata makosa yanapotendeka kwa viongozi wa ngazi za chama kwa kuogopa kufukuzwa.
"Ndugu zangu wananchama, kukosoana ni sehemu ya kuleta maendeleo katika jamii yoyote ambayo inajali demokrasia ya kweli na kama hatutaweza kusema kwa kuhofia kufukuzwa hiki chama mtakiua, semeni msioneane aibu kama kiongozi kakosea semeni," alisema Silaa.
Alisema vyama vya upinzani nchini vimepata nguvu kubwa kutokana na baadhi ya watendaji wa CCM ngazi za vijiji, kata, wilaya na mikoa kushindwa kuwawajibisha viongozi wanapokosea kwa kuogopa kufukuzwa.
Aidha alisema kitendo hicho kimewapunguzia heshima mbele ya wananchi na kusababisha majimbo mengine kuchukuliwa na wapinzani.
Hata hivyo,aliwataka viongozi hao kukosoana kwa utaratibu na kwamba anayekosea aangaliwe kama yeye na sio kama chama kwani sio wote ni wachafu.
Kwa upande wake Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kazidi alisema wapo baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiwatumia wanavyuo kuanzisha migomo kwa madai CCM iliyoko madarakani ndio imeyaleta hayo.
Awali akisoma taarifa ya wanavyuo wa MUCCOBS kwa niaba ya wanachama wa CCM mbele ya mgeni rasmi, David Waryoba alisema umefika wakati kwa CCM kufanya maamuzi dhidi ya wanaokichafua chama hicho.
No comments:
Post a Comment