Hassan Hamad (OMKR)
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema tofauti ya dini na vyama vya siasa isiwe sababu ya kuwagawa Watanzania.
Amesema Watanzania wamekuwa wakiishi kwa muda mrefu na kuvumiliana, na kwamba ni vyema utamaduni huo ukaendelezwa kwa maslahi ya wananchi na taifa kwa ujumla.
Maalim Seif ametoa tamko hilo Mkoani Arusha, baada ya kutembelea eneo la kanisa lililotokea mripuko na kusababisha vifo vya watu watatu na wengine 66 kujeruhiwa.
Amesema kwa niaba yake, Serikali na Chama Cha Wananchi CUF, wanalaani kitendo hicho cha kikatili, na kuwataka waumini wa dini hiyo na watanzania kuwa wastahamilivu wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Parokia ya Mtakatifu Joseph Mkoani Arusha Julius Mbaga, amesema tukio hilo lilitokea kwenye uzio wa jengo hilo wakati waumini wa dini hiyo wakiwa katika ibada zao,na kusambaa kwa kasi na hatimaye kusababisha maafa hayo.
Maalim Seif pia amekutana na viongozi wa Jimbo kuu katoliki la Arusha na kuwataka kuwa na subra kutokana na msiba uliolikumba kanisa hilo Jumapili iliyopita.
Wakati huo huo Maalim Seif alitembelea Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru Mjini Arusha kuwajuilia hali baadhi ya majeruhi wa tukio hilo waliolazwa katika hospitali hiyo ambapo hadi sasa watu 34 wanaendelea na matibabu wakiwemo wanawake na watoto.
Maalim Seif aliwasili Mkoa Arusha akitokea Mikoa ya Manyara na Singida ambako alikuwa na ziara ya siku mbili.
No comments:
Post a Comment