Habari za Punde

Wajawazito watakiwa kutojifungulia nyumbani


Na Joseph Ngilisho,Arusha
WAJAWAZITO Mkoani Arusha, wametakiwa kuhudhuria vituo vya afya, ili waweze kujifungua salama na kuepuka vifo visivyo vya lazima.

Ombi hilo lilimetolewa na Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Oldonyowasi iliyopo katika kijiji cha Oldonyowasi,kata ya Oldonyosambu, Zipporah Nyaurah, wakati akizungumzia changamoto Zinazowakabili watoa huduma kijijini hapo.

Alisema zahanati hiyo japo ipo kijijini lakini ina vifaa vya kisasa, ila cha kushangaza wanawake wanaohudhuria kliniki ni wengi, hata hivyo wanaojifungua hapo ni wachache na hawazidi 10 kwa mwezi.


Alisema ni aibu wajawazito kujifungulia nyumbani,huku akiitaka jamii kuwa mstari wa mbele, kuhamasisha wanawake kupenda kuhudhuria kliniki, ili kupata ushauri wa daktari.

Alisema zahanati hiyo iliyojengwa kwa ushirikiano na wadau wa maendeleo, ikiwemo msaada kutoka Ujerumani, licha ya kutoa huduma za afya,inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa umeme, jenereta na uhaba wa nyumba za wafanyakazi.

“Nawaomba kinamama waje kujifungulia kwenye zahanati yetu ni aibu kujifungulia majumbani, labda itokee bahati mbaya lakini kama mnakuja kupimwa kliniki, kwa nini msije kujifungua hospitali ili kama kuna tatizo basi msaidiwe,”alisema.

Pia aliiomba serikali kuangalia uwezekano wa kupata umeme kijijini hapo, ili waweze kutumia vifaa vya kisasa vilivyopo hospitali na kuweza kufanya upasuaji.

Alisema uchache wa watumishi na ukosefu wa usafiri ni tatizo kubwa linalosababisha wakati mwingine zahanati hiyo kushindwa kujifungua kwa wakati kutokana na ukosefu wa usafiri.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.