Na Mwantanga Ame
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar inajiandaa kuja na sheria kukabiliana na ongezeko la misumeno ya moto, ambapo sasa misumeno inapunguzwa hadi kufikia minne tu.
Hayo yameelezwa jana na Jumuiya ya Wanamisitu Tanzania kanda ya Zanzibar,inayosimamia uhifadhi wa vianzio vya maji Mwera hadi Kianga, wakati wakizungumza na waandishi wa habari ofisini kwao Maruhubi mjini Unguja.
Rahika Hamad, mjumbe wa Jumuiya hiyo,alisema serikali kupitia wizara ya kilimo na misitu, imeanza mchakato wa kuandaa sheria hiyo itakayozuia misumeno ya moto kuingia nchini.
Alisema katika utekelezaji wa mpango huo serikali inakusudia kuhakikisha misumeno ya moto inabakia minne itakayotumika nchini kote kwa utaratibu maalum.
Alisema misumeno hiyo itakuwa ikitolewa baada ya kutolewa sababu za msingi zitazothibitishwa na taasisi husika.
Alisema serikali inakusudia kuchukua hatua hiyo kupunguza matumizi ya misumeno hiyo kutokana na kusababisha ongezeko la ukataji miti.
Alisema baadhi ya nchi tayari zinatekeleza sheria kama hiyo, ambapo misumeno imepunguzwa hadi kufikia mmoja tu unaotumika nchi nzima.
Alisema tayari hekta 1,000 za miti ya asili imeteketezwa hali ambayo ikiachiwa inaweza kuigeuza Zanzibar jangwa.
Alisema athari za ukataji miti zimesababisha kukauka vianzio vingi vya maji.
Zanzibar tayari ilishawahi kuendesha operesheni ya kuichoma moto misumeno iliyokamatwa,lakini bado matumizi ya misumeno hiyo inaendelea.
No comments:
Post a Comment