Habari za Punde

RC ajitangaza balozi wa fistula


Na Matina Nkurlu, Geita
KAMPENI inayoendelea mikoani ya kuelimisha wananchi juu ya fistula imewahamasasisha wakazi wa mji wa Geita huku Mkuu wa Mkoa huo, Said Magarula akionesha dhahiri kuguswa na kutangaza kuwa yupo tayari kuwa balozi wa fistula katika mkoa wake ili kumaliza tatizo hilo.

Msafara wa kampeni ya fistula unaojumuisha wataalamu kutoka hospitali ya CCBRT, mabalozi wa fistula ambao ni wanawake waliowahi kupatwa na tatizo hilo na Balozi wa chapa ya Vodacom Msanii Mwana FA uliingia mjini Geita jana na kuendesha kampeni ya wazi kwa wananchi.

Msafara huo unafadhiliwa na kampuni ya Vodacom na Vodafone ya Uingereza ikiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha siku ya fistula duniani Mei 23, kitakachofanyika jijini Dar es salaam.

Wakionesha kuguswa na ushuhuda uliotolewa na mabalozi wa fistula pamoja na elimu ya jumla kuhusu tatizo la fistula kwa wanawake, wakazi hao walisema wapo tayari kuungana na wafadhili wa kampeni ya kutokomeza ugonjwa huo nchini ifikapo mwaka 2016.

"Fistula muisikie tu kwa mbali na wala msiombe kuishuhudia kwa macho, ni mbaya na inatutesa sana wanawake kampeni hii inatupa faraja na kutufanya tujisikie kuwa sasa tupo salama wakati wa kujifungua,” alisema Salma Daudi wakati akitoa maoni yake wakati wa kamepni hiyo.

Aidha baadhi ya vijana na wanaume waliofika kwenye tukio hilo walisema baada ya kupata ushuhuda kutoka kwa wanawake waliowahi kupatwa na ugonjwa huo pamoja na elimu iliyotolewa ikiwemo ujumbe kwamba fistula inatibika tena bila malipo kwa gharama za Vodacom na Vodafone, wamehamasika.

"Ukweli nimeguswa sana na kama mwanamme nimehamasika kutoa mchango wangu katika jamii na hata kuwa tayari kumvumulia mke wangu iwapo atapatwa na tatizo hilo wakati wa kujifungua kwa kuwa fistula inatibika, mmetugusa sana na tunashukuru kwa kutufikia,”alisema Magige John mkazi wa Geita.

Magige aliiomba Vodacom kuhakikisha inafanya kila jitihada kuhakikisha kampeni hiyo inafika Tanzania nzima ili kuhakikisha kila mtu anapata elimu ya fistula na hasa kufahamu kwamba inatibika tena bila malipo huku akitoa rai kwa wanaume kuwa na mtazamo tofauti juu ya fistula.

Akizungumza katika kampeni hiyo Mkuu wa Mkoa,Magarula aliahidi kutumia nguvu na rasilimali za mkoa ukiwemo mtandao wa kiserikali kutoka ngazi ya mkoa hadi kitongoji kuhakikisha ujumbe wa fistula unamfikia kila mkazi wa Geita.

Alisema sio uamuzi rahisi kwa kampuni ya biashara kuamua kwa makusudi kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwezesha matiababu kwa wanawake wanaopatwa na ugonjwa huo hivyo fursa hiyo lazima ipewe heshima na kutumika kwa masilahi ya taifa.

"Natambua kuwa changamoto kubwa tuliyanayo katika huduma za afya ni gharama za matiabbu, wenzetu hawa Vodacom wameshajitolea tena kwa asilimia mia moja, hivyo sioni kwa nini tuendelee kujificha, kuogopa na kuteseka," alisema.

"Naipongeza Vodacom na Vodafone ya Uingereza kwa kuamua kwa makusudi kuendesha kampeni na pia kufadhili kampeni hii kwa wananchi wetu, hili ni jambo kubwa na muhimu linalopaswa kuungwa mkono, serikali haina kikwazo kutoa ushirikiano kwa jambo lolote lenye masilahi ya taifa,” alisema.

Kwa wastani Vodacom na Vodafone hutumia kiasi cha shilingi 700,000 hadi 900,000 kugharamia matibu ya mgonjwa mmoja wa fistula.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.