Habari za Punde

Ushirikishwaji wananchi kuongeza ufanisi

Na Nasima Haji
USHIRIKISHWAJI wa wananchi na uelewa wa mambo mbali mbali kutachangia mabadiliko ya maendeleo na kuongezeka ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.

Hayo yamebainika katika majadiliano ya ushirikiano wa manufaa ya wote yaliyofanyika jana hoteli ya Bwawani mjini Unguja.

Washiriki wa majadiliano hayo walisema hatua hiyo inatoa fursa kila upande kutoa mawazo na kufanyiwa tathmini yakinifu na mbinu bora ya utekelezwaji wake.

Akifungua majadiliano hayo, Mwenyekiti wa mjadala huo, Dk. Idriss Musli Hija, alisema mpango huo unatoa fursa ya kukutana na wananchi na kujadiliana katika sekta mbali mbali za maendeleo.

“Lengo ni kuendeleza dhana ya ‘mmoja akifanikiwa na mimi nimefanikiwa’. Hatuwezi kuendelea kwa kukwamishana,” alionya Dk. Idriss ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja.


Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara Tanzania, Raymond Mbilinyi, alisema utaratibu kama huo unawaleta pamoja wadau ambapo nchi nyingi duniani zimeanza kuufuata na umeonesha mafanikio ya maendeleo endelevu ikiwemo Malaysia.

Aidha, alisema majadiliano hayo yana umuhimu kwa Tanzania kwani yatachangia kutekeleza dira ya maendeleo ya 2020 na mpango wa maendeleo wa miaka mitano.

“Majadiliano kama hayo yanaleta mabadiliko ya haraka ya kiuchumi na kijamii kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania,” alisema.

Katika majadiliano hayo mada kadhaa ziliwasilishwa zikiwemo; kuhamasisha teknolojia kwa mageuzi ya kiuchumi, umuhimu wa ubunifu katika megeuzi ya kiuchumi na kijamii Tanzania; mchango wa kiuchumi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii, mchango wa viwango vya ubora wa bidhaa katika mageuzi ya kiuchumi na kijamii na umuhimu wa usalama katika kudumisha amani na maendeleo endelevu.

Kuhusu usalama wa bidhaa, Afisa Mdhibiti Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania, Julitha Tibanyenda, alisema bidhaa zisizo salama zinasababisha magonjwa, vilema na vifo kwa watumiaji na matatizo mengine kadhaa hali inayohitaji kudhibiti hali hiyo.

Washiriki wa majadiliano hayo walisema mfumo wa elimu hautoi nafasi ya kuwajenga vijana kuwa wabunifu ambapo masomo yanasomeshwa kinadharia zaidi kuliko vitendo.

Aidha, waliongeza kuwa tafiti zinazofanywa hazifuatiliwi kiasi cha kushindwa kutekeleza yale yanayobainika kuwa ni kikwazo cha kutokuwa na maendeleo katika sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

Pia, walipendekeza kuwa kuna haja ya kuwa na sera itakayosimamia ukuaji wa teknolojia na mfumo wa elimu utakaowajenga vijana kupata taaluma kuhusiana na teknolojia ili kuwa wabunifu na hatimaye kufikia maendeleo yaliyokusudiwa.

Majadiliano haya yamesimamiwa na Baraza la Biashara la Zanzibar (ZBC) na Baraza la Biashara la Taifa la Tanzania (TNBC) ambapo mkutano wa kitaifa utasimamiwa na Ofisi wa Waziri Mkuu Tanzania na wa kimataifa utasimamiwa na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano huo utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 28 Juni hadi Julai 1, 2013.

Mkutano huo uliwashirikisha wanasiasa, wanataaluma, wasanii, Jumuiya za kiraia na wanahabari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.