Habari za Punde

Zanzibar na China zasaini mikataba mengine ya mashirikiano


 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi wa Maendeleo Omar Yussuf Mzee,akitiliana saini makubaliano ya kibishara kwa upande wa serikali ya Zanzibar na Naibu Waziri wa Biashara wa China Liu Cigui,katika ukumbi wa mikutano wa China World Hotel,wakishudiwa na baadhi ya mawaziri na maafisa wa Serikali zote mbili Zanzibar na China
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Uchumi wa Maendeleo Omar Yussuf Mzee,akibadilishana Hati ya saini ya Mikataba ya uhusiano wa biashara na Naibu Waziri wa Biashara wa China Liu Cigui,baada ya kutilianan saini katika ukumbi wa mikutano wa China World Hotel
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, na Naibu Waziri wa Biashara wa China Liu Cigui,katika ukumbi wa Mikutano wa World Hotel China,ambapo alifanya mazungumzo na kutiliana saini Makubaliano masuala ya Biashara
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein, akipeana  na Mkono wa shukurani na Naibu Waziri wa Biashara wa China Liu Cigui,baada ya kutiana saini makubaliano katika nyunja za kibiashara kati ya Serikali ya China na Zanzibar, katika  ukumbi wa Mikutano wa World Hotel China.
 
Picha na Ramadhan Othman, Beijing China
 
Na Said Ameir, Beijing China
Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China jana zilitiliana saini makubaliano ya ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Utiaji saini huo uliofanyika mjini Beijing, China umeshuhudiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ambaye yuko nchini humo kwa ziara ya kikazi ya siku saba.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Mendeleo Omar Yusuf Mzee alitia saini makubaliano hayo kwa niaba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makubaliano ya kwanza ni ya ushirikiano katika sekta ya afya ambapo Serikali ya China itasaidia ujenzi wa chumba cha wagonjwa mahututi na vifaa vyake katika Hospitali Kuu ya Manazi Mmoja. Makubaliano mengine ni ya mafunzo ambapo Serikali ya China itatoa nafasi za mafunzo ya muda mfupi kwa maafisa habari na maafisa mipango wa Serikali ya Zanzibar.
Makubaliano mengine ni ya ushirikiano katika sekta ya uvuvi hususan katika ufugaji wa mazao ya baharini na utafiti wa mambo ya bahari ambao utekelezaji wake utashirikisha Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar-SUZA.

Aidha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha, Uchumi na Mipango ya Maendeleo Omar Yusuf Mzee siku hiyo alitia saini Mkataba wa utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mradi wa Mkonga wa Mawasiliano katika hatua ya utekelezaji kwa matumizi katika sekta ya afya na kodi. Mkataba huo ni kati ya Serikali ya Zanzibar na Kampuni ya ZTE ya China.
Viongozi wengine waliohudhuria hafla ya kusaini mikataba hiyo ni pamoja na Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Ramadhani Abdalla Shaaban, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdillah Jihad Hassan, Balozi wa Tanzania nchini China Philip Marmo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar-ZIPA Salum Khamis Nassor, Mshauri wa Rais Ushirikiano wa Kimataifa na Uwekezaji Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa na wajumbe wengine katika msafara wa Rais.
Kabla ya kusainiwa kwa mikataba hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alifanya mazungumzo, kwa nyakati tofauti, na viongozi na watendaji wa sekta husika ambapo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano katika nyanja hizo ili kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya Zanzibar na China.
Dk. Shein aliwaeleza viongozi hao kuwa kutiwa saini kwa mikataba hiyo kunadhihirisha sio tu udugu na urafiki uliopo kati ya Serikali na wananchi wa Zanzibar na Jamhuri ya Watu wa China bali pia dhamira ya kisiasa waliyonayo viongozi wa nchi hizo kuenzi historia iliyoandikwa na viongozi waanzilishi wa urafiki huo ambao ni Mwalimu Julius Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume kwa Tanzania na Mao Zedong kwa upande wa China.
Wakati huo huo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein jana alikutana na ujumbe wa makampuni ya China yanayotoa huduma katika biashara ya utalii.
Mkutano huo uliofanyika katika hoteli ya China World Hotel Dk. Shein aliyaeleza makampuni hayo kuwa yana nafasi nzuri kuleta watalii katika visiwa vya Unguja na Pemba na Tanzania kwa jumla kwa kuwa kuna vivutio vingi vya kitalii.
Aliueleza ujumbe huo kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuendeleza na kuimarisha huduma katika sekta utalii kwa kuwa kwa sasa ndio sekta inayoipatia serikali mapato mengi zaidi.
Dk. Shein ambaye yuko nchini China kufuatia mwaliko wa Rais wa China Bwana Xi Jinping aliwasili jana katika mji wa Nanjing katika jimbo la Jiangsu ambapo leo anaendelea ziara yake katika jimbo hilo kwa kutembelea hospitali ya Drum Tower ambako atakutana na madaktari waliowahi kufanya kazi Zanzibar.
Mchana atakutana na viongozi wa jimbo la Jiangsu na baadae atatembelea Kituo cha Utafiti cha Kampuni ya ZTE.

2 comments:

  1. Hii kweli ni nchi ya kusadikika! yaani mpaka mzee wangu Bw.Ramadhani Abdalla Shaaban amekwenda China wakati wizarani kwake mambo hayaendi.

    Ninavyoandika, ofisini kwake kumejaa mafaili ya uhaulishaji yanayosubiri saini zake.

    ReplyDelete
  2. Ha ha ha .
    NCHI YA KUSADIKIKA.

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.