Habari za Punde

60 wafanyiwa upasuaji wa macho

Na Amina Mmanga, Pemba
WANANCHI 60 kisiwani Pemba, wamefanyiwa upasuaji wa macho kuondoa mtoto wa jicho, na wawili kati yao walilazimika kusafirishwa Dar-es Salaam kwa matibabu baada ya kuonekana macho yao kuharibika zaidi.

Zoezi hilo la siku tatu lililofanyika hospitali ya Chake Chake liliendeshwa na madaktari bingwa kutoka shirika linalotoa matitabu ya macho la FEC la Dar -es Salaam kwa kushirikiana Wizara ya Afya Zanzibar.

Katika operesheni hiyo wanawake waliopatiwa matibabu hayo walikuwa 28 na wanaume 32.

Akizungumza na waandishi wa habari hizi, hospitalini hapo, Msimamizi wa zoezi hilo Dk. Ali Rashid Ali alisema, zoezi hilo limesaidia wananchi wa Pemba kupata matibabu ya haraka.

Alisema baadhi ya wananchi wenye matatizo kama hayo wamekuwa wakipata tabu ya kutafuta matibabu na wakati mwengine kugharamika.

Aliwataka wananchi wengine wenye matatizo ya macho na hasa ya mtoto wa jicho kufika katika kitengo hicho kila wanaposikia tangazo la kuwepo kwa madaktari hao bingwa.

Kwa upande wake Daktari mkuu wa upasuaji wa macho, Karumucabo Patrice, aliomba serikali kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusiana na maradhi ya macho, kwani inaonekana watu hawana uelewa ukizingatia macho ni kiungo muhimu katika mwili wa binadamu.

Hata hivyo alielezea kufurahishwa na ushirikiano mkubwa walioupata kutoka Wizara ya Afya pamoja na Hospitali ya Chake Chake.

Nae Mwakilishi wa shirika la SOS, Husna Juma Selingwi ambalo ndilo lililogharamia usafiri wagonjwa,alipongeza hatua ya kufanyiwa upasuaji wagonjwa hao ambao sasa wamenusurika na upofu.

Ali Abdala Ali (68) mkaazi wa Micheweni ambae ni miongoni mwa wagojwa waliofanyiwa matibabu hayo, aliyapongeza mashirika yote pamoja na Wizara ya Afya kwa kufanikisha zoezi hilo vyema.







No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.