Habari za Punde

Maalim Seif mgeni rasmi mashindano ya vyuo vikuu

 .  Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikabidhi kikombe cha ushindi kwa timu ya Chuo cha Afya Mbweni, baada ya kupata ushindi katika mashindano ya Vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu Zanzibar (ZAHLIFE). Kushoto ni Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Haji Mwita.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikagua timu ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu, wakati ikijiandaa kuvaana na timu ya Afya Mbweni, katika fainali za mashindano ya Vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu Zanzibar (ZAHLIFE) iliyofanyika uwanja wa Amaan Zanzibar.
 Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akikagua kikosi cha timu ya Chuo cha Afya Mbweni, wakati ilijiandaa kuvaana na timu ya Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu, katika fainali za mashindano ya Vyuo vikuu na Taasisi za elimu ya juu Zanzibar (ZAHLIFE) iliyofanyika uwanja wa Amaan Zanzibar.
 Mashabiki mbali mbali waliojitokeza katika mchezo wa fainali za mashindano ya Vyuo vikuu na Taasisi za elimu Zanzibar uliofanyika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
 Mashabiki mbali mbali waliojitokeza katika mchezo wa fainali za mashindano ya Vyuo vikuu na Taasisi za elimu Zanzibar uliofanyika uwanja wa Amaan mjini Zanzibar.
 Maandamano ya Taasisi za elimu ya juu Zanzibar yakipita mbele ya mgeni rasmi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, katika shamra shamra za fainali ya mashindano hayo yaliyofanyika viwanja vya Amaan.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, akipokea maandamano ya Taasisi za elimu ya juu Zanzibar, katika shamra shamra za fainali ya mashindano hayo yaliyofanyika viwanja vya Amaan. (picha na Salmin Said, OMKR

Na: Hassan Hamad, OMKR
Timu ya Chuo Cha Afya Mbweni, imetwaa ubingwa na kukabidhiwa kombe la mashindano ya Vyuo Vikuu na Taasisi za elimu ya juu Zanzibar (ZAHLIFE).
Afya Mbweni walitwaa ubingwa huo baada ya kuwashinda wapinzani wao Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu, katika fainali ya mashindano hayo iliyopigwa viwanja vya Amani mjini Zanzibar, na kuhudhuriwa na washabiki wengi hasa wanataaluma wa Elimu ya juu.
Mchezo huo uliokuwa na msisimko na ushabiki mkubwa, ulimalizika kwa timu hizo kumaliza dakika 90 za mchezo bila ya kufungana, na ndipo ilipoitishwa mikwaju ya penalti ambapo jumla ya penalti 7 zilipigwa kwa kila upande.
Timu ya Afya Mbweni ilishinda kwa penalti 4 dhidi ya wapinzani wao Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu waliofunga penalti 3.



Akiwa mgeni rasmi katika fainali hiyo ya Taasisi za elimu ya Juu Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, alipongeza hatua ya taasisi hizo kuandaa mashindano ambayo yameibua hamasa kubwa kwa wanamichezo hao.
Amesema ili kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanafanikiwa zaidi na kuibua vipaji vinavyohitajika, ni vyema maandalizi yake yakaanzia skuli za msingi, sekondari na vyuo.
Ameiagiza Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamadani, Utalii na Michezo kuhakikisha kuwa wanayaunga mkono mashindano hayo na kuleta ufanisi zaidi.
Katika hatua nyengine Maalim Seif amewaomba wafadhili na makampuni ya Zanzibar kujitokeza kwa wingi kufadhili michezo ili kurejesha hadhi ya soka Zanzibar.
Mashindano hayo yaliyozishirikisha timu 13 za taasisi za elimu ya juu Zanzibar, yalidhaminiwa na Benki ya Watu wa Zanzibar PBZ ambapo timu ya Chuo cha usimamizi wa fedha Zanzibar Chwaka, iliibuka mshindi wa tatu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.