Habari za Punde

Maoni ya Kamati ya Kudumu ya Ofisi za Viongozi Wakuu.

  MAONI YA KAMATI YA KUDUMU YA KUSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU WA KITAIFA YA BARAZA LA WAWAKILISHI JUU YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA OFISI YA RAIS NA MWENYEKITI WA BARAZA LA MAPINDUZI KWA MWAKA WA FEDHA 2013/2014 NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA OFISI KWA MWAKA 2013/2014.


UTANGULIZI:

Mheshimiwa Spika,kwanza kabisa napenda kuchukua fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kukutana kwa mara nyengine tena tukiwa hai na wazima wa afya ambayo ni neema kubwa kwetu kwa lengo la kujadili bajeti mwaka 2013/2014 kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pia napenda kukushukuru wewe binafsi kuweza kunipatia nafasi hii mbele ya Baraza lako tukufu kuweza kuwasilisha maoni ya Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa juu ya utekelezaji wa Bajeti kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Mheshimiwa Spika, kabla ya kuwasilisha maoni ya Kamati pia napenda kumshukuru Mhe Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na watendaji wa Ofisi hii kwa utendaji mzuri wa kazi zao ambao unaipelekea Kamati kuweza kutekeleza majukumu ya kazi zake za kila siku kwa ufanisi mzuri. Hata hivyo, napenda kuishukuru Ofisi hii kuweza kuwasilisha mbele ya Baraza lako tukufu bajeti ya Wizara yao kwa mwaka 2013/2014 kwa umahiri mkubwa.

Mheshimiwa Spika, Aidha nitakuwa mwizi wa fadhila nisipowashukuru Wajumbe wa Kamati yangu kwa kazi kubwa walioifanya kwa muda wote na ushirikiano wao pamoja na moyo wa dhati katika kutekeleza majukumu yao katika kufanikisha kazi za Kamati ikiwemo hii ya kuchambua na kuijadili bajeti ya Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, sasa kwa ruksa yako Mhe Spika, naomba niwatambue wajumbe wa Kamati yangu kama ifuatavyo:-

1. Mhe Hamza Hassan Juma Mwenyekiti

2. Mhe. Saleh Nassor Juma Makamo Mwenyekiti

3. Mhe. Ali Mzee Ali Mjumbe

4. Mhe. Ashura Sharif Ali Mjumbe

5. Mhe.Shadya Mohammed Suleiman Mjumbe

6. Mhe. Makame Mshimba Mbarouk Mjumbe

7. Mhe. Subeit Khamis Faki Mjumbe

8. Ndg.Rahma Kombo Mgeni Katibu Kamati

9. Ndg.Makame Salim Ali Katibu Kamati

Mheshimiwa Spika, baada ya utangulizi huo naomba kutoa maoni ya Kamati kwa Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa bajeti hii ya mwaka 2013/2014 kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika,kamati yangu tunaungana na Mhe Waziri kwa kulaani tabia iliyoanza kujitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani pamoja na uhalifu wa kumwagiwa watu tindikali au (ACID )na kuwaharibia maisha yao na hata kuondoa maisha ya watu mbali mbali yaliyotokezea hivi karibuni. Mhe Spika, ni vyema na sisi sote tuliomo humu ndani hatunabudi kulaani vitendo vyote hivyo, kwani sisi sote ni banaadam tunapaswa kulinda usalama wa maisha yetu sote kwani tusione yametokea kwa wenzetu tukayaona madogo lakini inawezekana siku nyingine yakatokezea kwetu Mwenyezi Mungu atuepushie na hilo lakini ni vyema kama sisi ni viongozi basi wajibu wetu kutoa taaluma kwa wananchi wetu majimboni kwani huo ndio wajibu wetu.

Mheshimiwa Spika, nampongeza sana Mhe Waziri, kwa utaratibu aliouanzisha wa kutoa (summery) ya utekelezaji wa maagizo ya wajumbe wako wa Baraza yaliyotolewa wakati alipowasilisha Bajeti yake mwaka uliopita, staili hii itaweza kutusaidia sana kupata ufafanuzi wa mambo yote tuliyoiuliza wizara kwa niaba ya wananchi wetu jambo ambalo hata wananchi wetu wataridhika na utaratibu huu, na huu ndio utawala bora, nakupongeza sana waziri kwa hilo. Kwa hiyo ili kumpunguzia masuali waziri basi tuangalie viambatanisho alotuletea kwenye hotuba yake.

Mheshimiwa Spika, kama alivyoeleza Mhe Waziri mpango wa Bajeti inayotumia Progran ( PBB ) ikiwemo program ya kuimarisha ushirikiano kikanda , kimataifa na wa Wazanzibari wanaoishi nchi za nje, ( DIASPORA ) Mhe Spika, eneo hili ni muhimu sana kwani tukiweza kujipanga vizuri basi Nchi yetu inaweza kupiga hatua za haraka kwa maendeleo ya Nchi yetu, kwani mashirikiano ya kimataifa kwa Dunia ya leo ni kuangalia uchumi zaidi hasa kutokana na ongezeka la idadi ya watu hapa kwetu na Duniani kote kwa ujumla, na chanagamoto ya ukosefu wa ajira Duniani kote, na uchumi wa dunia ya ulimwengu wa leo basi eneo hili la ushirikiano wa kikanda na kimataifa ni muhimu sana, kwa hiyo ushauri wangu tuwatumie sana wenzetu wazanzibari walioko nchi za nje ili kutusaidia kutuunganisha na wawekezaji pamoja na wahisani , na mashirika mbali mbali ili kusogeza maendeleo ya Nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hapa naomba tuungane kwa pamoja kuacha mambo yetu yote na tujikite zaidi katika kuangalia nini tufanye ili kuliondoa taifa letu katika orodha ya nchi masikini na kuiweka katika nchi za wastani wa kati na hatimae kuingia katika nchi zilizoendelea, na uwezo huo upo ikiwa sote tutakuwa kitu kimoja, kwani nchi yetu ni ndogo na hata idadi yetu pia ni ndogo sana, kwa hiyo nnashauri eneo hili tujitahidi sana.

Mheshimiwa Spika, Pia miongoni mwa Program hizo ni kuimarisha ulinzi na usalama. Mhe Spika, eneo hili ndio muhimu sana kuliko maeneo yote kwani nchi yeyote Duniani hata iwe tajiri vipi lakini kama hakuna amani na utulivu basi hata maendeleo hayawezi kupatikana, kwani tumeshuhudia hivi sasa miongoni mwa nchi zilizokuwa na utajiri mkubwa na amani na utulivu lakini leo miji yao imekuwa magofu na wananchi wao wamekuwa wahanga wakubwa wa maafa ,wengi wao wamepata ulemavu wa kudumu ,vifo vya kila siku, uharibifu wa mali zao, wameingia kwenye umaskini wa maisha, na hata mitaji na biashara zao nyingi zimefilisika kabisa kutokana na vita na vurugu za kila siku kila kukicha mabomu, mizinga nk. Kwa mfano kama Libya, Misri, Syria, Iraq, nk.

Mheshimiwa Spika, na sisi tumuombe Mwenyezi Mungu asije kutupeleka huko, kwa hiyo katika Program hiyo kamati yangu inaomba kufanyike utafiti huo na kuangalia viashiria vyote vinavyoonyesha dalili ya uvujinfu wa amani na kutomuonea haya mtu yeyote ambae atoonekana kama ni chanzo cha vurugu za aina yoyote na kumchukulia hatua za kisheria kwa haraka sana , na kutokana na kuwa nchi yetu ndani ya miaka miwili ijayo inategemea kupita katika mkondo mkubwa wa wimbi la mabadiliko makubwa ya mfumo wa utawala na sheria za nchi zetu kwa hiyo, hiki ni kipindi kifupi cha mpito lakini kiutawala ni kipindi kikubwa cha maisha na uhai wa Taifa letu na maisha ya watu wetu, kwa hivyo, ni vyema kwa sasa na iko haja ya kuongeza bajeti ya vikosi vyetu vya ulinzi na usalama, kuongeza ulinzi katika mipaka yetu, anga yetu, Bahari yetu na hata mitaani kwetu na namuomba Mhe Waziri , akija aje anieleze je Serikali imejiandaa vipi na kukabiliana na kipindi hiki cha mpito na kuna bajeti yeyote ya akiba iliyoandaliwa kwa ajili ya kuihami nchi yetu kwa lolote litakalo jitokeza ili kuwahakikishia usalama wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, Kama alivyoeleza Mhe Waziri, mwakani tunategemea kusherehekea sherehe za kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, ambapo vimeandaliwa vipindi kwenye Redio na TV kuelimisha wananchi mafanikio ya mapinduzi lakini pia naomba ushauri wa kamati yangu pia kuandaa makongamano ya vijana ,kinamama, na wazee pamoja na wasomi ili kutoa maoni yao na kutuelekeza nini tufanye ili kuweza kuyaendeleza na kuyaboresha malengo ya Mapinduzi yetu. Lakini vile vile tunaomba maandalizi hayo yawe mapema na pia kungalia hali ya uwanja wetu wa Amani au uwanja mwengine wowote utakaotumika katika kusherehekea sherehe hizo, kwani tuna wasi wasi kuwa wananchi wengi watahitaji kushiriki wao wenyewe ili kuona nini kinachoenedelea , ushauri wangu pamoja na kamati yangu ni vyema kutafuta mapema Ma (SCREEN ) makubwa ( BILL BOARD ) na kuyaweka kwenye viwanja vya mpira mbali mbali unguja na Pemba mijini na vijijini ili kuweza kushuhudia moja kwa moja kile kitakachokuwa kikiendelea hapo uwanjani, sasa sijui hili kama Serikali wameliangalia au vipi.

Mheshimiwa Spika, pia Mhe Waziri katika kutekeleza program zake mbali mbali ambazo amezipanga ambazo ni nyingi nitawaachia wajumbe kuzichambua lakini kubwa ninalotaka kumkumbusha Waziri kuwa kuharakisha sheria ya Serikali za mitaa ili kuzijengea uwezo Halmashauri ,pamoja na mabaraza ya Miji ili ziweze kujitegemea na kuweza kujipangia malengo na kujisimamia wenyewe kwani hivi sasa sheria inawabana na kushindwa hata kuingia mikataba moja kwa moja na taasisi za nje, kitu ambacho kinawarejesha nyuma katika shughuli zao za maendeleo, lakini pia kamati yangu inaikumbusha Serikali kuwasomesha na kuwajenga uwezo watendaji wa Halmashauri na mabaraza ya miji kwani mageuzi ya Serikali za mitaa yananahitaji wataalam wa kubuni miradi , mipango miji, wanasheria kwa ajili ya kusimamia mikataba ya kisheria, wachumi, na wengineo ili kuziwezesha kukabiliana na changamoto za mabadiliko hayo.

Mheshimiwa Spika, vile vile Kamati yangu inapenda kusisitiza Halmashauri zote kuweza kusimamia mapato na kubuni vianzio vipya ili kuweza kupata mapato yatakayowawezesha kuendesha Halmashauri zao na kuweza kusaidia ujenzi wa bara bara za ndani na pia kuboresha mitaro ya maji machafu. Hata hivyo, kutokana na hali ya uchafu unaoongezeka kila siku katika maeneo ya miji na vijijini Kamati inashauri kuandaa utaratibu wa kuweka maeneo maalum ya taka lakini pia kuandaa mipango ya kuzoa taka hizo na kupeleka kwenye (slabu za kutuputia taka). Lakini pia Kamati inapenda kushauri Halmashauri ya Wilaya ya Chake Chake na Baraza la Mji Mkoani kuangalia upya vianzio vyao vya mapato kwani vipo chini sana.

Vile vile Baraza la Mji Chake kwa kushirikiana na idara ya ardhi na mipango miji Kamati inashauri kutafuta eneo la kuegeshea magari ili kuondoa tatizo la msongamano la magari katika soko la Chake Chake.

Mheshimiwa Spika, Kwa upande wa Baraza la Manispaa Kamati inasisitiza kukamilisha mpango wa kujenga shoping mall hapo Darajani ili kuweza kuondoa tatizo la msongamano la wafanyabiashara wadogo wadogo katika maeneo ya Darajani na Mchangani.

Mheshimiwa Spika, Mhe Waziri , tunaipongeza Serikali kwa kuweza kutafuta eneo huko kibele kwa ajili ya kutupa taka kwani hivi sasa katika mji wetu wa Zanzibar taka imekuwa ni tatizo kubwa sana na ndio maana hata watendaji wa Municipal hupata usumbufu kwa wananchi zinapokwenda kujengwa silabi za taka wanakuwa wagumu kwani hakuna uhakika wa kuzolewa kwa taka hizo, kwa hiyo, tunamtaka Waziri ajitahidi kukamilisha zoezi la upatikanaji eneo hilo ili hizo taka ziweze kwenda kuhifadhiwa, lakini vile vile si vyema kuweka silabi za taka kwenye maeneo ya shule kwani huwakosesha raha na utulivu watoto wetu wanaosoma kwenye shule hizo, lakini hasa wakati wa mvua husababisha nzi wengi na harufu mbaya kwa walimu na wanafunzi wanaosoma katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Spika, pia kuhusu mradi wa ZUSP tunamtaka Waziri kujitahidi kuharakisha utekelezaji wa mradi huo kwani umepitishwa siku nyingi na gharama za vifaa kila siku zinaongezeka ,na zaidi katika ujenzi wa mitaro ya kupitishia maji machafu hasa ujenzi wa mtaro Kwamtipura , Shauri Moyo na Saateni ambao katika kitabu chake ameusahau kuutaja sijui kwa makosa au ndio ameshautoa kwenye mpango naomba jawabu kwa hilo kwani mtaro huo unaathiri maisha ya wananchi waishio pembezoni mwa unapopita mtaro huo hasa wakati wa mvua kubwa na zile za masika, hivyo, iko haja wa kuharakisha hatua za ujenzi huo, kwani mimi nnavyojua mtaro huu ulikuwemo tangu hatua za mwanzo za mradi huu.

Mheshimiwa Spika, Pia tunaitaka Serikali kuyaboresha makaazi ya wakuu wa Mikoa na Wilaya ili kuweza kuishi katika mazingira yanayolingana na hadhi yao. Sambamba na uboreshaji wa sehemu zao za kufanyia kazi ikiwemo ofisi na vitendea kazi katika ofisi hizo. Tunaishukuru Serikali kwa kuwapatia usafiri wakuu wa mikoa na wilaya wote. Tunaomba magari hayo yafanyiwe service kwa muda muafaka kwani magari mengi ya Serikali huharibika mapeme kutokana na kutofanyiwa service kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, pia tunapongeza Serikali kwa kuboresha uwekaji taa za barabarani pia tunaomba mpango huu uende sambamba na taa za kuongozea magari lakini pia kua na mpango wa kuweka CCTV CAMERA ili kuzuia na kuweza kupata taarifa hasa za uvunjifu wa amani na viendo vya uvunjifu wa sheria katika nchi yetu wakati umefika hasa kwa dunia ya leo CCTV CAMERA , husadia sana katika kuwatambua na kuwakamata wahalifu kupitia camera hizo kwani tumeshuhudia hata hivi karibuni kule Buston Marekani ambapo kulitokea milipuko kwenye mbio za marathon ambapo watuhumiwa walipatikanwa kupitia kwa msaada mkubwa wa CCTV CAMERA kwa hiyo ni jambo jema na la busara kuweka camera hizo, ili kulinda usalama wetu.

Mheshimiwa Spika, kamati yangu inapongeza jitihada zinazochukuliwa na kikosi cha zimamoto na uokozi kwa kuweka mikakati ya kuziboresha huduma zao kwani zinaimarika kila siku tunaona jitihada za Kamishna na tumefurahi sana kusikia kuwa tayari wameshapatiwa eneo katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar ili kuimarisha huduma za zima moto katika uwanja wetu wa ndege ambao tunategemea kuongezeka kwa huduma zake hivi karibuni tu mara baada ya kukamilika kwake, lakini pia tunapongeza jitihada hizo kwa kutiliana saini upatikanaji wa magari manne ya kuzimia moto pamoja na vifaa vingine ambayo yataweza kusaidia sana kuokoa mali na maisha ya wananchi wetu pale moto utakapotokea, lakini pia mkazo uwekwe katika kuwapatia eneo muafaka na kuwajengea jengo la zima moto katika kiwanja cha ndege cha Pemba kwani yale makaazi yao hayaridhishi hata kidogo kwani wanapata taabu sana hasa wakati wa mvua zinaponyesha. Lakini pia kamati yangu kwa kushirikiana shirika la Bandari tunaomba kupatikana mahala maalum kikosi hicho pale Bandarini kwani pale walipo hapakidhi mahitaji hasa kwa shughuli zao za kila siku, kwa hiyo hili naomba wahusika wakae na uongozi wa shirika la Bandari ili kuweza kulitafutia ufumbuzi wa kudumu suala hilo.

Mheshimiwa Spika, kamati yangu inashauri pamoja na kazi kubwa inyofanywa na Idara ya faragha na kukabiliwa na ufinyu wa Bajeti lakini iko haja ya kuboresha Ikulu ya Mkokotoni alau kwa kuanzia na ukuta au fence ili kuiweka katika hali ya ulinzi pamoja na usalama wa eneo hilo kamati inapongeza jitihada zilizofanywa na Idara hii kwa kuweza kufanya ukarabati mkubwa wa Ikulu ya Mkoani Pemba ambapo ilikuwa imechakaa sana.

Mheshimiwa Spika, Mhe Waziri ameelezea ziara za Mhe Rais wa Zanzibar nje na ndani na kwa zile za nje ametueleza kuwa ameomba makampuni ya China kuja kuekeza hapa Zanzibar suala je tayari tunayo Master Plan ya hayo maeneo ya uwekezaji hapa Zanzibar? na Je tayari tumekwisha weka miundo mbinu katika hayo maeneo ya uwekezaji au wakija tena kama kawaida yetu tuwapeleke kwa wananchi wakalipe fidia na kusumbuliwa kama wawekezaji wengine tunavyowafanyia? Jambo ambalo natahadharisha ni kuwa wenzetu wachina sio watu wa masihara kwani wanalosema ndilo wanafanya hufanya na hawawezi danadana kama hiyo, maeneo hayo tujiandae vya kutosha kwani sera ya China hivi sasa ni kuimarisha masoko ya kimataifa na makampuni ya China kuekeza nje ya Nchi yao na kwa hilo wako tayari sana kwani leo Dunia nzima kuanzia Asia, Amerika, na hata Ulaya kuna makampuni mengi tu ya China yanaendelea kuekeza huko ,kwa hiyo na sisi isijekuwa tumeenda kuwaita lakini kumbe hatujajitayarisha kuwapokea.

Mheshimiwa Spika, lakini kamati yangu jambo ambalo linalo tusikitisha kuwa katika ziara ya ndani ya Mhe Rais amekuwa akitoa maagizo mengi lakini hatua za utekelezaji haziridhishi wakati huambatana na jopo la viongozi wa Serikali, miongoni mwa maagizo hayo ni lile suala la viongozi wa Mikoa na Wilaya kuyamaliza matatizo ya migogoro ya ardhi jambo ambalo limekuwa donda ndugu ,hadi leo kamati yangu inaendelea kupokea malalamiko ya migogoro ya ardhi ambayo hayaishi sasa naomba Waziri kuwasimamia viongozi wa mikoa na wilaya kuyamaliza matatizo hayo, kwani kuna baadhi ya maeneo wananchi hunyan”ganywa maeneo hayo na hawapati msaada wowote, kwa hiyo naomba Waziri kulivalia njuga suala hilo.

Mheshimiwa Spika, Ofisi ya Baraza la Mapinduzi imeendelea kufanya kazi zake vizuri lakini kamati yangu inawataka kuharakisha upatikanaji wa hati miliki ya majengo yote ya Ikulu hapa Zanzibar kwani hilo ni jambo la lazima hasa kwa wakati huu, tunawapongeza kwa kukamilisha upatikanaji wa hati ya Ikulu ya mnazi mmoja.

Mheshimiwa Spika, Idara ya ushirikiano wa kimataifa na uratibu wa wazanzibari waishio nchi za nje, Idara hii ina kazi kubwa ya kuwatafuta na kuwatambua na kuwaunganisha mawasiliano yao moja kwa moja na Serikali , lakini kamati yangu bado inasisitiza kufanywa kwa jitihada kubwa za kuwatafuta kwani tunajua kuwa wazanzibari wako wengi sana nchi za nje, na kuna wataalam wengi ambao wana ujuzi na utaalam mkubwa lakini bado hadi leo Idara haijaweza kuwatafuta, wazanzibari hawa wanazitumikia nchi za watu na kutumia utaalam wao huko nje, kwa hiyo kamati yangu inaitaka Serikali kuiwezesha Idara hii kufanya ziara za makusudi hasa katika nchi za Canada, Marekani , Oman, Uingereza , na nchi ambazo kuna wazanzibari wengi na kwenda kukaa nao na kuzungumza nao na kuwasikiliza nini ushauri wao na kuja kuufanyia kazi, kwani hawa huleta pesa nyingi kwa ndugu na jamaa zao lakini katika njia zisizokuwa rasmin kitu ambacho kinaikosesha Serikali mapato ambayo yangeliweza kuchangia hata pato la Taifa letu. Hapa Serikali iweke mikakati maalum kwani kamati haikuridhika na uingizwaji wa fedha katika Idara hii kwani hadi March ni 41% ya fedha tulizoidhinisha ndizo zilizopatikana kwa hali hii hatutegemei kama lile lengo lililokusudiwa kama litafikiwa.

Mheshimiwa Spika, Waziri ametuelezea ushiriki wa Idara ya ushirikiano wa kimataifa katika mikutano mbalimbali ikiwemo Indian Ocean Rim labda waziri angelikuja kutuelezea ni fursa gani zilizopo katika jumuia hii ya ( IOR ) na Zanzibar tumezitumia vipi. Pia kamati yangu inashauri kuwa Idara itafute jengo au ofisi ambayo itakuwa nje ya jengo la Ikulu kwani mazingira ya hawa Diaspora hasa wale wanaokuja kutembelea Zanzibar inakuwa ni vigumu kwao kwenda Ikulu kwani mazingira ya Ikulu ni mazingira maalum na sio kila mtu anapaswa kuingia kule hasa kama shughuli zake hazihusiani na Ikulu.

Mheshimiwa Spika, Kitengo cha usalama wa Serikali ( GSO ) tunawapongeza kwa kazi kubwa wanazozifanya , na tunaziomba taasisi zote za Serikali wanapokuwa na shughuli zao hasa za ajira na mafunzo ya maadili ya kazi basi kukitumia kitengo hiki, lakini kamati yangu bado haijaridhika na uingizwaji wa fedha hauridhishi kwani kazi zao ni kubwa na nyeti lakini kuna uhaba wa fedha na pia kutokana na kazi zao nyingi hufanya nje ya ofisi yao wakati mwingine hata hutumia usafiri wao wenyewe bila ya kufidiwa mafuta wanayotumia kutokana na uhaba wa usafiri katika ofisi yao na hii hupelekea kufanya kazi zao katika mazingira magumu.

Mheshimiwa Spika, Afisi ya usajili na kadi za vitambulisho vya Uzanzibari, kamati yangu inaipongeza kwa kazi kubwa na ngumu wanayoifanya kwa wazanzibari , kamati yangu inasikitishwa na kitendo cha Wizara cha kuwanyima posho nyeti kwa muda mrefu ambalo walistahili kupatiwa jambo ambalo tumelishauri kila tunapokutana na Wizara na Waziri amekuwa akituahidi kuwa atawapatia lakini hadi leo posho yao hiyo hawajapatiwa , kwa hiyo tunamuomba Waziri kuhakikisha suala hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu kwani hiyo ni haki yao na wala sio sadaka. Kwani tukiweza kuwalipa vizuri watendaji wetu ndio watakapoongeza bidii ya kufanya kazi. Kamati yangu inapongeza mpango maalum wa kuwapatia vitambulisho wageni wanaoishi Zanzibar hili ni jambo jema ambalo litasaidia kuweka usalama wa wananchi yetu. Pia kamati yangu inawapongeza Idara kwa kuendelea kutoa vitambulisho vyenye kiwango cha kimataifa ambacho kinatambulika duniani kote.

Mheshimiwa Spika, Idara ya Serikali za mitaa kamati yangu inaitaka kuharakisha mchakato wa kurekebisha sheria ya vileo kwani hivi sasa kumekuwa na malalamiko mengi kwa mabaa yalioko mitaani jambo ambalo kutokana na mila na desturi yetu wazanzibari kwanza pombe ni haram, kwa hiyo kuruhusu kuweka mabaa kwenye maeneo ya makaazi ya watu hupelekea vitendo vya aibu na fedheha vinavyofanywa na watu wakishalewa lakini pia wakati mwengine matusi na vurugu vinavyotokea baada ya watu kulewa inawasumbua sana wananchi wanaoishi katika maeneo hayo , kwa hiyo, tunaitaka Idara kuharakisha mchakato wa marekebisho hayo ili kuweza kuiokoa jamii kuepuka usumbufu wanaoupata kwenye mitaa yao.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mjini Magharibi, kamati yangu inashauri kamati ya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi katika Mkoa huu kwani mkoa huu ndio chimbuko la kila kitu mazuri yapo mkoa huu ,mabaya pia yako mkoa huu kwa hiyo ni vyema kuwa na ulinzi imara, pamoja na kuwa Waziri ameturipotia kuwa vitendo vya uhalifu vimepungua lakini tusibweteke, kwani katika siku za hivi karibuni kumeanza kujitokeza vitendo vya uvunjifu wa amani, pamoja na mauaji,pia kamati yangu inautaka mkoa huu ,kuhakikisha agizo la Mheshimiwa Rais la kuondoa wanyama wote wanaohatarisha usalama wa barabarani kwa mifugo hiyo kuzurura barabarani jambo ambalo linaweza kusababisha ajali wakati wowote, tunaomba zoezi hili liwe endelevu na isiwe la muda tu.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kaskazini Unguja kamati yangu unawashauri kuzidiasha ulinzi kwani majahazi hupakia na kuingiza abiria kupitia Bandari bubu ambazo hazijatambuliwa kisheria na Serikali, lakini pia katika eneo la Nungwi kunahitajika kufanyika kwa tathmini maalum kuhusu wageni walioko kule na kuwatambua wote na kuwapatia vitambulisho maalum vya Mkoa ili wale wageni wote watambulike na Mkoa ili jambo lolote litakalotokezea basi iwe ni rahisi kuweza kudhibiti, lakini pia kuwashirikisha katika kulinda usalama wa eneo hilo.

Mheshimiwa Spika,Mkoa wa Kusini Unguja, tunawapongeza Mkoa huu kwa kazi wanazozifanya kuwatumikia wananchi wetu, kamati yangu inaiagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa pamoja na wilaya zake kuhakikisha wanazitambua nyumba zote za wananchi zilizokodishwa wageni kutoka nje na kuziripoti Idara ya Uhamiaji pamoja ZRB, kwani wageni hawa hukodishwa nyumba hizo lakini Serikali haifaidiki na kodi yoyote kutoka kwao jambo ambalo ni kinyume na Sheria, lakini pia ni hatari kwa nchi yetu kwani hatuwezi kujua wageni hao wanajishuhulisha na nini, na wanakutana na watu wa aina gani na pia wana mikakati gani, kwani hakuna nchi inayokubali kuwaachia wageni wakiishi ndani ya nchi na kukwepa taratibu za nchi husika.

Mheshimiwa Spika,Mkoa wa Kusini Pemba, tunawapongeza kwa kazi nzuri wanazofanya kuwahudumia wananchi wetu ,pia tunawapongeza kwa kuweza kukamilisha upatikanaji wa kiwanja cha kujenga nyumba ya Mkuu wa Mkoa kwa hiyo kamati yangu inaitaka wizara kuhakikisha wanaanzisha ujenzi wa makaazi hayo kwa haraka ili kuweza kumpatia makaazi yanayolingana na hadhi ya Ofisi hiyo.

IDARA YA URATIBU YA IDARA MAALUM:

Mheshimiwa Spika, kamati yangu pia inawapongeza tume ya utumishi na Idara ya maalum kwa kuweza kukamilisha Scheme of Service kwa askari wetu wa vikosi vya SMZ kwani kwa muda mrefu askari wetu wamekuwa wakipata mshahara mdogo pamoja na stahiki zao nyengine mbali mbali kamati yangu inaamini kukamilika kwa Scheme hii sasa alau na wao wanaweza kutononoka kimapato na kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa, kwa hiyo, kwa kuwa Waziri ametueleza kuwa hivi sasa wameshaipeleka Serikalini, wizara ya utumishi wa umma jambo ambalo linahitaji marekebisho , kwa hivyo tunaitaka Serikali kupitia wizara ya utumishi wa Umma wakamilishe mapitio hayo ili marekebisho hayo yaingie kwenye bajeti hii tunayoipitisha, kwa hiyo tunamtaka waziri wa Utumishi wa Umma atupatie ufafanuzi katika hili kabla ya kusomwa bajet yake.

KMKM:

Mheshimiwa Spika, kamati yangu inawaponeza makamanda wote kwa kazi kubwa ya kutulindia mipaka yetu hasa huko Baharini, pia pongezi kwa kuweza kutafuta vifaa kwa ajili ya kazi ya uokozi ikiwemo kuwapatia mafunzo askari wetu wa KMKM pia na huduma wanayoitoa kwa Hospitali yao iliyopo Kibweni, hili ni jambo la faraja. Kamati yangu inaomba kutengwa fungu maalum ili kuweza kuwapatia posho maalum askari wetu wazamiaji pale inapotokea kazi maalum ya kuzamia baharini na kuokoa maisha ya watu na mali zao kwani tumeona ugumu wa kazi yao lakini inakuwa hakuna hata huduma ya chakula au maji kuwapatia askari wetu mpaka kusubiri Idara ya maafa.

JKU:

Mheshimiwa Spika, tunawapongeza makamanda wote wa kikosi hiki kwa kazi kubwa ya kuwalea vijana wetu kuwapatia mafunzo ya ukakamavu kabla ya kuanza ajira, pia tunawataka kuendeleza mashirikiano walioanzisha baina yao na JKT ya Tanzania Bara kwani wameweza kuchota ujuzi mwingi kutoka kwa wenzao, ushauri wetu yale mazuri wanayoyakuta kwa wenzao JKT basi waje kuanzisha hapa kwetu Zanzibar, kwa mfano JKT wameanzisha kampuni ya JKT ambayo hufanya miradi mbali mbali ikwemo kuanzisha Kampuni ya ulinzi na kuchukua Tender ya kulinda kwenye Mahoteli, na Makampuni mbali mbali ya watu binafsi kitu ambacho kinawasaidia kutoa ajira binafsi nje ya Jeshi, kwa hiyo, na hapa kwetu itaweza kusaidia kutoa ulinzi kwenye Mahoteli yetu ya kitalii na kuliondoa tatizo la uvamizi wa mara kwa mara unaofanywa kwenye Mahoteli ya kitalii.


KIKOSI CHA ZIMAMOTO:

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inawapongeza makamanda wote wa kikosi hiki kwa kazi kubwa wanayofanya kuokoa mali na maisha ya watu pale yanayotokea majanga mbali mbali ya moto na ajali nyingine, kwa kua mwanzoni nilieleza kuridhika na hatua waliofikia kwa kuweza kupatikana eneo la kuweka kituo chao hapo uwanja wa ndege wa Zanzibar sina haja ya kurudia tena, lakini naomba sana Kamishna wa kikosi hiki kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine ikwemo Halmashauri na Mabaraza ya miji hasa katika kusimamia taratibu za ujenzi wa nyumba za makaazi kwani watu huachiwa kujenga na kuweka aidha njia nyembamba au kuziba kabisa jambo ambalo wakati ukitokea moto inakuwa ni vigumu kuweza kufika kwa wakati kama malengo yao walivyojiwekea ndani ya dakika 15, kwa hiyo kamati yangu inawapongeza pia kwa kikosi kuwajenga uwezo askari wetu wa kikosi hiki.

KIKOSI CHA VALANTIA (KVZ)

Mheshimiwa Spika, Kamati yangu inawapongeza makamanda wote kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa kulinda taifa letu ikiwemo mali zetu, kamati yangu bado inashauri kikosi hiki kuweza kuharakisha upatikanaji wa hati miliki ya maeneo yao unguja na Pemba na pia kuweza kuboresha makaazi ya Askari wetu, vilevile kuhakikisha mgao wa fedha kwa upande wa Pemba unafanywa kwa wakati, lakini pia kuhakikisha madeni mengi ya muda mrefu kule Pemba yanalipwa ili kuweka heshima na taaswira nzuri kwa makamanda hasa kule Pemba lakini pia mkazo uwekwe kwa kuimarishwa kwa makaazi ya makamanda na wapiganaji katika kikosi hiki.

CHUO CHA MAFUNZO:

Mheshimiwa Spika, kamati yangu inapongeza kikosi hiki kwanza kwa kuwa wabunifu wa miradi lakini pia wasikivu kwa yale maelekezo tunayopeana wakati wa ziara za kamati, kwani kila siku zinavyoenda wanajitahidi kuboresha makaazi wa wanafunzi (wafungwa) ikiwemo kuwajenea vyoo, lakini pia kuwatenganisha wanafunzi watoto, mbali ya watu wazima, pia kuimarika kwa huduma za kisheria wanazowapatia wanafunzi ili kuwasaidia katika kukata rufaa, na kuwapatia wanafunzi vyombo vya kupata habari ikiwemo TV n Radio, ambapo mambo hayo yote hapo mwanzo yalikuwa hayapatikani, pamoja na hayo wamejaribu pia kuongeza milo kutoka miwili hadi mitatu kwa siku jambo ambalo huleta faraja na kutofautisha kuwafanya wanafunzi kuhisi wako chuo cha mafunzo na sio jela kama vile zamani.

Mheshimiwa Spika,Kwa maboresho hayo hatunabudi kutoa shukrani zangu za dhati kwa makamanda kwa kazi kubwa wanayoifanya kuboresha makaazi ya wanafunzi, pamoja na hayo kamati yangu ilishauri kikosi hiki kujenga uzio katika chuo cha Mafunzo kinu Moshi na Langoni ili kuviweka vyuo vile katika hali ya usalama zaidi na kuwapunguzia kazi askari wetu, lakini pia kuwapatia posho la kazi ngumu wale askari wanaokwenda kuwalinda wanafunzi hasa wanapokuwa maporini kwani wakati wowote wanaweza kutorokwa, kwani askari wetu wanakuwa wakiwalinda wanafunzi karibu kutwa nzima ikiwa jua au mvua, lakini pia kamati yangu imeishauri kikosi hiki kulijenga lango kuu la chuo cha Mafunzo cha ubago na kukipandisha hadhi kuwa ni Gerzeza la Mkoa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi katika chuo cha Mafunzo hapo mjini lakini pia kupunguza gharama za kuwasafirisha wanafunzi kutoka mkoa wa kusini, kamati yangu pia inakitaka kikosi hiki kuzifanyia ukarabati mkubwa nyumba za askri zilizoko kangani kwani askari huvujiwa wakati wa mvua wakati wanafunzi wao hawavujiwi jambo ambalo huwafanya askari wetu kujihisi kama na wao wako chuo cha mafunzo.

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizi naomba sana ndani ya bajet hii Serikali ihakikishe inaongeza maslahi ya askari wetu kwani wao ndio walinzi wetu ,huwezi kuwa na walinzi ambao huwajali kwenye maslahi yao.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache naomba wajumbe wenzangu tuichangie,tuiboreshe na baadae tuipitishe bajeti hii ili waende wakayatekeleze hayo yote tuliyowaagiza .

Ahsante sana,naomba kuwasilisha.

Hamza Hassan Juma,



Mwenyekiti,

Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa,

Baraza la Wawakilishi,

Zanzibar.





No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.