Habari za Punde

Mfanyabiashara mbaroni kwa kulawiti wanafunzi

Na Rose Chapewa, Morogoro
JESHI la polisi mkoani Morogoro linamshikilia mfanyabiashara wa mjini hapa, aliyefahamika kwa jina la Mohamed Mauji kwa tuhuma za kuwaingilia kinyume na maumbile wanafunzi wawili wa kiume wanaosoma shule ya msingi Mwere, Manispaa ya Morogoro.

Tukio hilo linadaiwa kutokea wiki iliyopita kwenye eneo la ofisi ya mfanyabiashara huyo anayejishughulisha na biashara ya kuuza vinywaji laini kwa bei ya jumla.

Akizungumzia tukio hilo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Mkuu wa polisi wilaya ya Morogoro, Sadick Tindwa,alisema watoto hao wanadaiwa kufanyiwa kitendo hicho Mei 31 mwaka huu majira ya saa 6:30 mchana dukani kwa mfanyabiashara huyo , na kuripotiwa kituo cha polisi cha mjini kati Juni tatu na wazazi wao.

Alisema wazazi hao walieleza kuwa waliwabaini kufanyiwa kitendo hicho baada ya kupewa taarifa na walimu wa shule hiyo kuwa watoto hao wamekuwa wakienda shuleni na fedha nyingi za matumizi pamoja na vitu mbalimbali.

Alisema baada ya wazazi hao kupewa taarifa hizo, walikataa kuwapa watoto fedha hizo na vitu ambapo waliwauliza mahali wanapopata fedha hizo na wao kueleza kuwa wamekuwa wakipewa na mtu waliyemtaja kwa jina la mzungu ambae amekuwa akiwafanyia vitendo hivyo.

Alisema baada ya kuwapekuwa sehemu za siri na kuamua kulifikisha suala hilo kwa Afisa Mtendaji wa kata ya kingo jirani na mfanyabiashara huyo.

Alisema Afisa Mtendaji aliamuru suala hilo lifikishwe kwenye kituo cha polisi kwa ajili ya kufanyiwa upelelezi.

Alisema baada ya kulifikisha suala hilo, jeshi la Polisi lilimkamata mtuhumiwa kwa uchunguzi ikiwa pamoja na watoto hao kupelekwa hospitali ya rufaa ya Morogoro kufanyiwa uchunguzi wa kina.

Hata hivyo mfanyabiashara huyo alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na tuhuma hizo, alikiri kuwafahamu wanafunzi hao ambao wamekuwa wakipita nje ya ofisi yake na kuomba fedha kwa ajili ya kununua soda.

Alisema yeye aliwahi kuwapatia kiasi cha shilingi 500 lakini hajawai kuwafanyia kitendo hicho cha kuwaingilia kinyume na maumbile kama wanavyodai.

Mfanyabiashara huyo alisema wanafunzi hao hupita nje ya ofisi yake, ambapo siku moja walimuomba fedha ya soda na ameshangazwa na kitendo cha polisi kufunguliwa kesi ya kuwalawiti.

Mtuhumiwa huyo kwa sasa yupo nje kwa dhamana kusubiri uchunguzi wa vipimo vya kidaktari kutoka katika hospitali ya rufaa ya Morogoro.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.