Na Kadama Malunde, Shinyanga
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Shinyanga, Hamis Mgeja amewataka wananchi kuacha kubeza mafanikio yaliyofikiwa na serikali ya CCM tangu iingie madarakani mwaka 2010 na kuongeza kuwa hakuna serikali yoyote duniani isiyokuwa na matataizo na njia pekee ya kuyaondoa ni kufanya kazi kwa juhudi na sio kukimbia chama.
Mgeja aliyasema hayo katika mkutano wa hadhara uliofanyika Ngokolo Mitumbani katika ziara yake kuangalia utekelezaji wa ilani ya CCM tangu iingie madarakani.
Alisema CCM imefanya mambo mengi mazuri ikiwemo masuala ya elimu, barabara, maji na afya na kusema wale wasioona mafanikio hayo wana shukurani za punda.
Alisema mkoa wa Shinyanga hivi sasa una mabadiliko makubwa kwani wananchi wanapata maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria huku viwanda mbalimbali vikiendelea kujengwa hali ambayo itasaidia vijana wengi kupata ajira.
Aidha aliwataka wananchi kuwapuuza wapinzani wanaohubiri maandamano ama nguvu ya umma na kusisitiza kuwa hakuna serikali yoyote duniani iliyoingia kwa njia ya nguvu ya umma imefanikiwa.
Mgeja alitumia fursa hiyo pia kuwashukuru wananchi wa mkoa wa Shinyanga kuchagua viongozi wa CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
No comments:
Post a Comment