na Edson Kamukara, Dodoma
JUMLA ya askari polisi 114 wamefukuzwa kazi kutokana na makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa maadili ya kazi na wengine wamefikishwa mahakamani kati ya mwaka 2007 hadi 2010.
Hayo yalielezwa bungeni jana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereila Amme Silima, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Baraza la wawakilishi, Jaku Hashim Ayoub (BLW-CCM).
Mbunge huyo alitaka kuelewa serikali ina mpango gani wa kudhibiti vitendo vya baadhi ya askari polisi kuwabambikia kesi raia kinyume cha misingi ya haki za binadamu.
Pia alitaka kujua serikali imewachukulia hatua gani za kinidhamu na kisheria askari waliojihusisha na vitendo hivyo ili liwe fundisho kwa askari wengine.
Katika swali la msingi, pia mbunge huyo alitaka kuelezwa iwapo ripoti ya haki za binadamu na utawala bora imesema askari polisi wamekuwa na tabia ya kuwatishia wananchi na kuwasababishia kushindwa kufuatilia kesi zao vituoni, je, serikali imechukua hatua gani za kukabiliana na tatizo hilo?
Akijibu maswali hayo, Silima alisema serikali ina mikakati ya kukabiliana na kudhibiti vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu na utawara bora ikiwa ni pamoja na vitendo vya baadhi ya askari polisi kuwabambikia kesi na kuwatishia wananchi ili wasifuatilie kesi zao vituoni.
“Kuanzia mwaka 2007 hadi 2010 jumla ya askari polisi 114 wamefukuzwa kazi kwa makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa maadili na baadhi yao wamefikishwa mahakamani.
“Mafanikio ya Jeshi la Polisi yanategemea upatikanaji wa taarifa ya matukio hayo kutoka kwa wananchi ambao wanatendewa vitendo hivyo na baadhi ya askari ambao si waaminifu katika utendaji wao wa kazi,” alisema Silima.
Chanzo: Tanzania Daima
Jee swala la Jeshi la Polisi kutumiliwa na Wana siasa kwa ushabikiaji wa Chama, hili Mh Jaku vipi? Maana Kuanzia Makamishna na Polisi wadodo wadogo wadogo wate niwafuasi wakereketwa wakubwa wa ccm na kuna malalamiko mengi tu kuhusu Polisi kukanyaga Sheria na kuvunja haki za binadamu kwa Uchabiki wao wa kisiasa. jee hili vipi? au ccm haina zambi?.
ReplyDelete