Na Othman Khamis Ame OMPR
Sheha wa Shehia ya Tomondo Mohd Omar Said { Kidevu } anayeendelea kupatiwa huduma za afya katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Mnazi Mmoja baada ya kujeruhiwa kwa kumwagiwa Tindikali { Acid } tarehe 22 Mei mwaka huu anatarajiwa kupelekwa Nchini India mapema wiki ijayo kwa uchunguzi zaidi.
Sheha Mohd Kidevu alipatwa na mkasa huo wakati akiwa katika harakati za kuteka maji mara baada ya kurejea kwenye ibada ya sala ya ishaa usiku wa tarehe 22 mei mwaka huu wa 2013.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alipata fursa ya kumkagua sheha huyo kufuatilia maendeleo ya afya yake ambapo sheha Omar alieleza kwamba bado anaendelea kukabiliwa na maumivu katika sehemu alizoathirika.
Sheha Mohd Kidevu alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba huduma za madaktari wanaomshughulikia zimelata faraja kwake na familia yake na kuishukuru serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada zake zilizomsaidia kupatiwa huduma hizo.
Akimfariji sheha huyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliiagiza Wizara ya Afya Zanzibar kuhakikisha kwamba taratibu za safari ya mgonjwa huyo zinakamilika mara moja ili mapema wiki ijayo apelekwe nchini India.
Balozi Seif alionyesha kutoridhika kwake na hatua za taratibu zinazochukuliwa na watendaji wa Sekta ya Afya na kusababisha kucheleweshwa kusafirishwa kwa mgonjwa huyo nje ya Nchi wakati agizo tayari limeshatolewa.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuhakikishia Sheha Kidevu kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itajitahidi kadri ya uwezo wake ili kuona huduma za tiba yake zinasimamiwa na kutekelezwa kama wanavyofanyiwa wananchi wengine.
“ Nimefarajika kuona hali yako imerejea kidogo katika matumaini tofauti na ile siku niliyokuja kukukagua mwanzo. Hata uso wako umeonyesha uchangamfu “. Alifafanua Balozi Seif.
“ Hii ni fursa pekee kwako utakapokutana na wataalamu na wajuzi zaidi Nchini India usisite kuwaeleza matatizo yote ambayo bado yanaendelea kukusumbua hadi sasa “. Alimsisitiza Sheha huyo.
Balosi Seif alimuahidi sheha Omar Kidevu kumuaga wiki ijayo wakati anapotarajiwa kuelekea Nchini India kwa uchunguzi pamoja na matibabu zaidi ya kina.
No comments:
Post a Comment