Habari za Punde

Wafanyakazi wa Benki mbaroni kwa kumuibia mteja 400m/-

Na Rose Chapewa,Morogoro
WAFANYAKAZI wa benki ya Barclays tawi la Morogoro wamekumbwa na kashfa wakidaiwa kuiba kwa nyakati tofauti fedha zaidi ya shilingi milioni 399.8 kwenye akaunti ya mteja wao ambaye ni mfanyabiashara.

Wizi huo unadaiwa kufanywa kati ya mwezi Septemba mwaka jana hadi Aprili mwaka huu kwenye akaunti namba 0096000138 ya mfanyabiashara maarufu wa mjini Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, mfanyabishara huyo, Ajay Gokal alisema alibaini wizi huo mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuona fedha kwenye akaunti hiyo zinapungua siku hadi siku na kuamua kuomba taarifa za fedha,(bank statement).

Mfanyabiashara huyo alisema baada ya kubaini upungufu huo aliomba taarifa za kibenki mwezi Novemba mwaka jana na kubaini kuwepo kwa upungufu wa shilingi milioni119 na kushtushwa na upungufu huo wa fedha na hivyo kuamua kuomba ya taarifa za mwaka mzima.

Gokal ambaye ni mfanyabiashara maarufu wa moja ya kampuni ya simu ya mikononi alisema baada ya kuomba taarifa hiyo ya fedha ya mwaka alikuwa akizungushwa na uongozi wa benki hiyo hali iliyomlazimu kwenda kufungua jalada katika kituo cha polisi cha Morogoro.

Alisema kalilazimika kufanya hivyo kutokana na risiti za wateja wake walizoingiza fedha katika akaunti yake kuonyesha kuna fedha zilizoingizwa.

Alisema baada ya kufungua kesi maafisa wa jeshi la polisi waliamuru uongozi wa benki ya Barclays kumpatia taarifa hizo kwa kuwa ni haki yake lakini cha kushangaza ilikuwa ikimpatia miezi miwili huku mingine ikirukwa .

Mfanyabiashara huyo alisema baada ya kupitia kumbukumbu hizo toka Novemba mwaka jana hadi Aprili mwaka huu alibaini kuibiwa zaidi ya shilingi milioni 399.8.

Hata hivyo alipowasilina na uongozi wa benki hiy, ulidai suala hilo wanalishughulikia na kumtaka kutolifikisha kwenye vyombo vya habari kwani haliwezi kupatiwa ufumbuzi.

Akizungumzia wizi huo kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro,Faustine Shilogile alikiri kupata taarifa ya wizi huo baada ya mteja huyo kuomba taarifa za kibenki katika benki hiyo.

Alisema polisi ilianza kufanya uchunguzi baada ya uongozi wa benki hiyo kudai risiti zilizotumika kuweka fedha katika akaunti ya mteja huyo hawazitambui.

Hata hivyo, baada ya uchunguzi huo ilibainika kuwa risti hizo ni sahihi na zimetolewa na benki hiyo ikiwa pamoja na sahihi na mihuri yake.

Kutokana na hilo jeshi hilo limewahoji wafanyakazi wa benki hiyo na kuwashikilia watatu kwa tuhuma hizo huku uchunguzi zaidi ukiendelea na kwamba baada ya kukamilika jalada litapelekwa kwa mwanasheria wa serikali ili kufunguliwa mashtaka.

Mwandishi wa habari hizi alimtafuta Meneja wa benki hiyo tawi la Morogoro, Angelo Mahembe kupata ukweli wa suala hilo lakini hakukubali wala kukataa na kumtaka mwandishi awasiliane na makao makuu ya benki hiyo.

1 comment:

  1. ikiwa benki kubwa kama hizo na majina makubwa duniani wanafanya wizi , jee hizi benki zetu za walalahoi itakuwaje? jee sisi wakulima na wafanyakazi tukaweke wapi akiba zetu? nyumbani utaingiliwa na majambazi origino , ukiweka benki kuna majambazi feki , dah hii taabu imekuwa 'ukitaka cha mvunguni pindua tanda '

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.