Na A K Simai
Katika kuperuzi katika
mitandao mingi nimebahatika kuona jinsi watu binafsi, makampuni, viongozi wa
serikali na watu wengine wakijitahidi katika kuandaa futari na kuwalisha
walioalikwa.
Hili ni jambo zuri sana
katika mwezi wetu huu mtukufu wa Ramadhaan ambapo tumehimizwa pia zaidi ya
kufunga sisi wenyewe pia kukithirisha kufany aibada nyengine ikiwemo kuwalisha
na wengine na kufanya hivyo kuna fadhila kubwa ndani yake.- endapo tu
kutafanywa kwa ajili ya kupata radhi zake Allaah Subhaanahu Wata’ala na si
vyenginevyo. Allaah Subhaanahu anatukumbusha katika Qur’aan Suuratul Insaan
8-12
Na
huwalisha chakula, juu ya kukipenda kwake, masikini, na yatima, na wafungwa
Hakika
sisi tunakulisheni kwa wajihi wa Allaah. Hatutaki kwenu malipo wala shukrani
Hakika
sisi tunaiogopa kwa Mola wetu hiyo siku yenye shida na taabu
Basi
Allaah atawalinda na shari ya siku hiyo, na atawakutanisha na Allaah wakiwa na raha
na furaha
Na
atawalipa kwa Bustani za Peponi na maguo ya hariri kwa vile walivyosubiri.
Hivyo
ndivyo anavyotukumbusha Subhaana juu ya wenye kulisha kwa ajili tu ya kupata
radhi zake.
Hali halisi ya maisha katika
visiwa vyetu inajulikana kuwa ni duni na wananchi wengi ni wale wasiokuwa na
uwezo na wasiojiweza. Kuna familia hushindwa hata kupata mlo mmoja wa futari ya
maana kwa siku kutokana na ugumu wa maisha unaowakabili.
Tukiwa kama ni viongozi,
watu binafsi na hata makampuni , hatuoni haja ya kuwaangalia hawa kwa jicho la
huruma japo kwa mwezi huu tu wa Ramadhaan?
Mifano ya mialiko ya futari
tunayoiona kwenye mitandao haiakisi hali halisi ya maisha ya mtu wa kawaida
kuwa kuona waalikwa wengi ni watu ambao wanaojiweza na kuwepo pale ni kwa
sababu tu ya nafasi na hadhi waliyojaaliwa na Muumba.
Kinachosikitisha zaidi ni
kwamba mpaka viongozi wa dini nao huingizwa katika mtihani huu kwa kuelewa au
kutoelewa kwamba kuwepo kwao katika sherehe za futari za aina hii ambazo
zimekuwa za kijamii zaidi kuliko kidini maana yake ni kuzipigia muhuri kwamba
hazina tatizo lolote.
Viongozi wetu ndani ya mwezi
huu tunawahitajia katika misikiti wakidarsisha, wakisalisha, wakiwaongoza
waislamu katika mwezi mtukufu huku wao wenyewe wakiwa mstari wa mbele katika
kuzirudisha imani za waumini na dini yao. Kuwaona katika mialiko ya futari
ambayo haijalishi kama ni kwa ajili ya Allaah au vyenginevyo kunaweza kupeleka
ujumbe mwengine kwa jamii.
Tuna dhamana kama ni
viongozi kuhakikisha hatujengi misingi ambayo tutakuja kuwa mas-uul mbele ya
Allaah Subhaanahu Wata’ala na pia kuwanasihi viongozi wengine kwa yale yaliyo
na kheri na muwafaka kufanywa na waislamu pamoja na wasiokuwa waislamu
wanaotaka kulisha katika mfungo wa Ramadhaan kwamba kuzifanya shughuli hizi kwa
malengo yale yale yaliyokusudiwa na si kuyageuza kwa malengo mengine.
Viongozi wajenge moyo wa
kuweza kufanya maamuzi magumu ya kuzisamehe aina ya shughuli ambazo zitaweza kuwaweka
katika mtihani mbele ya Allaah licha ya kuwa karibu na watu. Suuratul Ahzaab
/37
Nawe
ukawachelea watu, hali Allaah ndiye mwenye haki zaidi kumchelea
Hizi ni nasiha tu kama
tulivyoamrishwa na Mtume rehma na amani zimshukie kwamba dini yetu inajengwa na
msingi wa nasiha. Ninaamini zitaweza kuwazindua na kuwafaa wale watakaokumbuka
kama walikuwa wameghafilika.
Ni kweli hizi pikiniki za kufutarisha zimetia fora tena. Mpaka rais nae anakuwa masikini anafutarishwa? Taireni tena masheikh. Utadhani nchi haina masheikh, au ndio masheikh wetu wako ndani! Ama kweli kufa kwa mdomo, mate kutawanyika..............
ReplyDelete