Na Aboud Mahmoud
WAISLAMU nchini wametakiwa kuondosha tofauti zao katika kulingania dini na kuendelea kuwaelimisha vijana juu ya mustakabali mzima wa dini yao.
Wito huo umetolewa na Sheikh Al-Alama Bahassan kutoka Lamu nchini Kenya, wakati wa ufunguzi Masjid Alyamin uliopo Kiyanga Wilaya ya Magharibu Unguja na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali wa dini.
Sheikh Al-Alama alisema kumekuwa na tabia kwa wananchi wengi kugombana na kuleta tofauti katika misingi ya dini jambo ambalo linazorotesha kusimama uislamu na kufanya dini hiyo idharaulike.
Alisema hivi sasa imekuwa jambo la kawaida kuwaona watu wengi wanawashawishi watu kujitumbukiza katika vyama vya siasa na sio kuwashawishi kutetea dini yao.
Aidha alisema kwamba kufunguliwa kwa msikiti huo isiwe sababu ya kuwagombanisha waislamu wa kijiji hicho bali iwe kichocheo cha kuendeleza umoja na kufuata misingi mizuri ya dini.
Nae Msimamizi Mkuu wa Msikiti huo Sheikh Thabit Noman Jongo, alisema kwamba kumekuwa na tabia katika misikiti mengi kuwa na migongano kutokana na masheikh wengi kutaka kutoa elimu aliyoipata na anayoijua jambo ambalo huleta madhara kwa binaadamu na kwa uislamu kwa ujumla.
Alisema tabia hiyo ya masheikh imekuwa ikileta athari kubwa kwa waumini wa dini ya kiislamu kwani husababisha ugomvi baina ya waislamu na pia kuifanya dini hiyo kudharauliwa.
Aliishukuru Jumuiya ya Alyamn kwa uamuzi wake wa kujenga msikiti katika kijiji hicho na kuwapa urahisi waumini wa kiislamu.
No comments:
Post a Comment