TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 16/8/2013
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kwa mara nyengine tena
tunawakaribisha sana katika Afisi ya
Baraza la Wawakilishi, na kabla ya yote,
tunapenda kuwashukuru na kuwapongeza kwa dhati kwa mashirikiano mnayoendelea
kutupa kwa kututolea taarifa zetu kwa
wananchi kuhusiana na shughuli
mbali mbali zinazohusiana na Chombo chetu hiki cha Baraza la Wawakilishi.
Kwa kweli mchango wenu umekuwa
ukitupa faraja kubwa na tunakuombeni muendelee kuwa karibu nasi kwa lengo lile
lile la kuwapatia wananchi taarifa muhimu zinazohusiana na Baraza la Wawakilishi.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kufuatia mabadiliko ya Kanuni za
Baraza la Wawakilishi kuelekeza Miswada
kusomwa kwa mara tatu , imeshauriwa baada ya kusomwa kwa mara ya
kwanza na kabla ya kujadiliwa na Kamati husika, itangazwe kwa wananchi
ili waifahamu Miswada hiyo na waweze kushiriki na kutoa maoni yao.
Miswada minne tayari imeshasomwa
kwa mara ya Kwanza katika Mkutano uliopita
yaani Mkutano wa Kumi na Mbili wa Baraza hili la Nane na itajadiliwa katika mkutano ujao wa
Oktoba.
Miswada yenyewe ni kama ifuatayo:-
- Mswada wa Sheria ya Kufuta na Kuandika Sheria inayohusu Kampuni na Jumuiya nyengine
Kuweka Masharti Madhubuti zaidi ya Uratibu na wa Kampuni, Jumuiya na Mambo yanayohusiana
na hayo.
- Mswada wa Sheria ya Kurekebisha Sheria mbali mbali za
Ardhi na mambo yanayohusiana na hayo.
- Mswada wa Sheria ya Kufuta na Kuweka Sheria ya Biashara
ya Zanzibar No. 4 ya 1989 na Kuweka Vifungu vya Kuimarisha Biashara Zanzibar na Mambo yanayohusiana
na hayo.
- Mswada wa Sheria ya Kuanzisha Sheria ya Marekebisho ya
usimamizi wa Utoaji wa Leseni za Biashara na Mambo yanayohusiana na hayo.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Pamoja na kwamba Kamati zinazohusika na Miswada hii
zinakusudia kualika wadau wakati wa kuchambua Miswada hiyo , Afisi ya Baraza la
Wawakilishi inapenda kutumia fursa hii kuwaomba wananchi, taasisi na makundi mbali mbali kutoa
michango na maoni yao kuhusiana na
Miswada hii, na tunaamini kwamba maoni hayo yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika
Kamati zitakazochambua Miswada hiyo
Kabla ya Kusomwa kwa mara ya Pili katika Baraza la Wawakilishi.
Tunawasisitiza sana wananchi
kuitumia fursa hii muhimu ambapo lengo ni kupata mawazo mengi zaidi kutoka
pande mbali mbali na hatimae kupata Sheria zenye ubora na matakwa ya wananchi.
Nakala za Miswada hii zinapatikana katika Afisi ya
Baraza la Wawakilishi Chukwani, na tovuti ya Baraza La Wawakilishi www.zanzibarassambly.go.tz na maoni yote yaletwe katika Afisi ya Baraza la Wawakilishi Chukwani
kwa Unguja, na Wete kwa Pemba. Aidha
maoni hayo yanaweza pia kutumwa kwa kupitia Sanduku la Barua 902, Zanzibar au kwa Njia ya barua pepe
zahore@zanlink .co.
Ndugu Waandishi wa Habari,
Mwisho tunapenda kuwaahidi kwamba
Baraza la wawakilishi litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa uwazi ili kila mwananchi afahamu kinachoendelea
kwa lengo la kuendeleza utawala bora
hapa nchini.
Ndugu Waandishi wa Habari, kwa mara nyengine tena
napenda niwashukuru kwa dhati kabisa kwa kazi yenu ambayo sisi kama Baraza
tunaithamini sana na kwa kiasi kikubwa
inachangia kueneza Taaluma muhimu kwa maendeleo ya wananchi wetu.
Ahsante sana kwa kunisikiliza.
Imetolewa
na
………………………..
(Yahya Khamis Hamad),
Katibu,
Baraza la wawakilishi,
Zanzibar.
No comments:
Post a Comment