Na Rose Chapewa, Morogoro
KIKOSI cha kuzuia ujangili kutoka Dar es Salaam (KDU), kwa kushirikiana na polisi mkoani hapa, wamegundua kiwanda bubu kinachotengeneza silaha na kukarabati kinyume cha sheria.Kiwanda hicho kipo mtaa wa kingo Manispaa ya Morogoro.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa polisi mkoani hapa Faustine Shilogile, alisema tukio hilo lilitokea Septemba 14 saa sita mchana,huku watu sita wakiwa wanashikiliwa na watano wanatafutwa kutokana na kujihusisha na kiwanda hicho.
Alisema kiwanda hicho bubu kulikuwa kikifanya shughuli hizo kwenye nyumba ya Ally Mavumila ambaye ni marehemu, na baada ya kufanya upekuzi walikamata vitu mbalimbali zikiwemo bunduki 11 ambapo kati ya hizo rifle ziko 7, shortgun 2, magobore mawili na risasi za rifle 22.
Vitu vingine vilivyokamatwa ni maganda ya risasi 13, mitutu 23 ikiwemo ya magobore miwili, shortgan 2 na rifle 458, mideki ya kusafishia bunduki, mitambo ya bunduki, utumbo wa bunduki, mechanism 15, magazine za rifle na vitako vya bunduki.
Kamanada Shilogile alisema katika upekuzi huo pia walikamata, mifuko ya kubebea silaha, mkanda wa kubebea bunduki,vyuma vya kushindilia baruti kwenye magobole, baruti robo kilo, firing pin pamoja na mitambo ya kutengenezea bunduki.
Alisema licha ya watu hao kujishughulisha na utengenezaji wa silaha,watuhumiwa walikuwa wakichonga funguo za aina mbalimbali zikiwemo za magari, pikipiki na za majumbani,ambapo alikataa kuwataja majina na kudai kuwa uchunguzi unaendelea na watafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.
Aidha Kamanda huyo aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao wa kutoa taarifa na kufanikisha kukamata silaha hizo.
Kwa upande wake Mhifadhi wa hifadhi ya Seleous, Kisiro Magesa Nsabo, alisema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya majangili kukamatwa na kudai kuwa wao wametumwa na matajiri wakubwa.
“Tuna changamoto kubwa sana hawa majangili tukiwakamata wanasema wametumwa na matajiri wakubwa, hawa matajiri ndiyo wanasababisha huu ujangili unaendelea ingawa tunajitahidi sana kukabiliana nao,” alisema.
Alisema msako huo ni maalumu ambao umeshirikisha hifadhi za Mikumi, Milima ya Udizungwa, Seleous na Kikosi cha kuzuia ujangili kutoka Dar es salaam (KDU) na kwamba ni endelevu na lengo lake ni kuzuia uhalifu wa wanyamapori.
No comments:
Post a Comment