Na Benedict Liwenga,Maelezo DSM
SERIKALI ya Tanzania imekanusha taarifa zilizochapishwa na gazeti la nchini Malawi lijulikanalo kama Malawi News, lililodai kuwa Wamalawi waishio Tanzania wamekuwa wakiogopa kutoka nje kutokana na ubaguzi wanaofanyiwa na Watanzania.Msemaji wa serikali ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Assah Mwambene alisema taarifa hizo ni za kupotosha umma na kuleta chuki dhidi ya Tanzania na nchi jirani na hazina ukweli wowote ule.
Alisema hakuna raia yeyote wa Malawi aliyebakwa wala kunyanyaswa kwa namna moja ama nyingine katika operesheni ya kuwaondoa wahamiaji haramu, ijulikanayo operesheni kimbunga.
“Hakuna raia kutoka Malawi aliyebakwa, wala anayeogopa kutoka nje kwa sababu ya ubaguzi wowote,” alisisitiza.
Alisema licha Tanzania kuwakamata wahamiaji haramu 1030 kutoka Malawi, serikali iliwapa fomu ili kama walikuwa wanahitaji kuishi nchini wahalalishe uwepo wao kwa wale walioonesha nia ya kuendelea kuwepo.
Aidha wahamiaji wote haramu 1030 kutoka Malawi waliachiwa huru na wanaendelea kukamilisha taratibu za kuhalalisha uwepo wao nchini.
Aidha alisema hakuna aliyewekwa ndani ama kushikiliwa na vyombo vya dola.
Kufuatia taarifa hizo,Mkurugenzi huyo amelitaka gazeti hilo kusahihisha taarifa hiyo na kuiomba radhi Tanzania kwa upotoshaji na kuongeza kuwa kauli hiyo ni sawa na matusi kwa Tanzania.
Alisema hadi sasa zaidi ya wahamiaji haramu 24,000 kutoka Jamhuri ya Kidemokarisia ya Kongo (DRC) , Rwanda, Burundi, Uganda na Zambia wamerejeshwa makwao kwa kosa la kuishi Tanzania bila vibali.
No comments:
Post a Comment