Habari za Punde

Mwalimu Aua Jambazi kwa Mkuki

Na Kadama Malunde,Shinyanga
KATIKA hali isiyo ya kawaida, mwalimu mmoja wa shule ya msingi Mihama katika kijiji cha Mihama kata ya Lagana tarafa ya Negezi wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, ameua mtu mmoja anayedaiwa kuwa jambazi kwa kumchoma mkuki kifuani.

Jambazi hilo likiwa na wenzake wawili walivamia nyumbani kwa mwalimu huyo usiku wa kuamkia jana.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla, alisema tukio hilo limetokea majira ya saa 7:00 usiku ambapo mwalimu huyo aliejulikana kwa jina la Paulo Nahembe (40) akiwa amelala nyumbani kwake ghafla alivamiwa na watu watatu wakiwa na silaha za jadi aina ya mapanga,mikuki na marungu.

Akielezea tukio hilo Kamanda Mangalla alisema, watu hao wakiwa wakiwa na silaha walikusudia kuvamia chumba anacholala mwalimu huyo alikini walikosea na kuingia chumba cha watoto.

Alisema baada ya mwalimu kugundua hali hiyo alianza kupambana nao na kufanikiwa kumchoma mkuki wa kifua mmoja wao na wengine kukimbia.

“Majambazi hao walikosea chumba wakaingia cha watoto na mwalimu akatumia nafasi hiyo kukabiliana nao na akamchoma mkuki kifuani jambazi mmoja ambaye hakufahamika jina mara moja na kusababisha kifo chake,” alisema Kamanda huyo.

Alisema upelelezi wa awali unaonesha mwalimu huyo alikuwa akijihami na kuongeza jeshi la polisi linaendelea kuwatafuta watuhumiwa wengine wawili.

“Watu waliomvamia mwalimu Nahembe inasemekana ni wakazi wa Igunga na walionekana siku ya tukio mchana wakirandaranda katika kijiji hicho, tunaendelea kuwasaka,” alisema.

Aliwataka wananchi wanapoona watu wageni na wanawatilia shaka kutoa ripoti polisi au maafisa watendaji wa vijiji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.