Na Juma Khamis
CHAMA cha Walimu Zanzibar (ZATU), kimesema licha ya kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya elimu nchini, lakini hakikushirikishwa kuandaa bajeti ya wizara ya elimu kwa mwaka fedha 2013/2014.Akizungumza na wanahabari katika wiki ya maadhimisho ya siku ya walimu duniani, Katibu Mkuu wa ZATU,Mussa Omar Tafurwa, alisema kawaida bajeti ya wizara inapaswa kujadiliwa na kamati ya uongozi ya wizara ambayo ZATU ni mjumbe, lakini hilo halikufanyika.
Alisema hali hiyo imesababisha kasoro nyingi na walimu kukisiwa mahitaji yao yasiyozingatia uhalisia.
Kwa mfano alisema, kutoshirikishwa kumesababisha vitengo muhimu vinavyohitaji bajeti ya kutosha kutokana na umuhimu wake kutengewa fedha kidogo.
“Ofisi ya Mkaguzi ambao ina hadhi ya kurugenzi imetengewa shilingi milioni 106 lakini kitengo cha ushauri nasaha kimetengewa shilingi milioni 380, jee ni kweli elimu ya Zanzibar ina idadi kubwa ya wavuta bangi wanaohitaji ushauri nasaha kwa kiasi hichi na kukisahau kitengo cha ukaguzi ambacho ndio roho ya ufundishaji,” alihoji.
Aidha alisema hakuna jukwaa la moja kwa moja kati ya muajiri (wizara ya elimu) na chama cha wafanyakazi (ZATU) kuzungumzia changamoto zinazowakabili walimu.
Kuhusu mshahara, alisema mshahara wa mwalimu ni mdogo na haukidhi kabisa mazingira magumu ya ufundishaji hali inayosababisha wasomi kuendelea kuikimbia sekta ya elimu.
“Mshahara wa mwalimu anaeanza kazi ni shilingi 170,000 kwa mwezi, lakini fedha hizi analipwa afisa mwengine wa serikali kama posho lake la kikao kwa siku,” alisema.
Alisema wizara lazima iishirikishe ZATU inapopanga mishahara na posho za walimu baadala ya kuwaamulia.
Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Salim Ali Salim, alisema Tume ya Utumishi ya Walimu ni muhimu katika kuboresha hadhi ya kada ya ufundishaji.
Aidha alisema muda umefika kwa serikali kuajiri wafanyakazi nje ya kada ya ualimu watakaofanya kazi maskulini badala ya waalimu kufanya kila kitu.
“Walimu wanafanya kazi za uhasibu, ushauri nasaha wakati sio kazi yao ya msingi, muda umefika kwa serikali kuajiri wafanyakazi nje ya kada ya ualimu,” alisema.
Nae Rais wa chama hicho, Maalim Salim Kitwana Sururu, alisema serikali iangalie maisha ya wanafunzi katika skuli zenye dakhalia.
Kwa mfano alisema katika skuli ya Fidel Castro, wanafunzi wanaoishi dakhalia mbali ya kuchangia huduma za chakula lakini wanalazimishwa kuchangia shilingi 1,000 kwa mwezi kwa huduma za umeme.
Katika maadhimisho ya siku ya walimu, chama hicho kimepanga kufanya mijadala mbali mbali Unguja na Pemba na kilele chake kitaadhimishwa Jumamosi ya Oktoba 5 katika hoteli ya Bwawani, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Kauli mbiu ya siku hii kimataifa ni “Mwalimu aongoze kupatikana elimu bora’ wakati kauli mbiu ya ZATU ni “Mwalimu na Motisha ni watoto pacha.”

No comments:
Post a Comment