Vituo vipya vikiwa vitupu bila ya gari
Donge ilivyoemewa na magari baada ya mabadiliko ya vituo vya Daladala
Nipo Kijangwani, sehemu moja nzuri na ipo katikati. Nilipojengwa
miaka dahari iliyopita nilikuwa kitoo cha mabasi yaendayo mashamba.
Naam wakati Serikali yangu ilipokuwa na neema nilikuwa nikitoa
huduma ya mabasi yanayokwenda mashamba kwa muda mrefu mpaka serikali sijui kama ilinichoka au ikaniona sina umuhimu tena
basi ikaniacha kama nilivyo haikuniuliza ndewe wala sikio.
Tokea Mabasi ya mara mwisho yalipokoma kutoa huduma sijui ni miaka
mingapi sasa maana nimeshakuwa mtu mzima na kumbukumbu imenitoka sikuulizwa
tena hali yangu nnafanya nini.
Sikusikitika sana maana naijua serikali yangu nikabaki nipo nipo tu
kama vijana wa sasa wanavyotuambia. Mara mbele yangu wakaja vijana wakaanza
kucheza mpira kwenye viwanja, mara baadae wakaja wauza mbao wakakaa mbele wakijitafutia rizki zao.
Jirani yangu nikaletewa mjengo mzuri wa Posta nikawa nnauonea uchoyo
kwa uzuri wake ulipojengwa miaka hiyo. Mara hata Idara ya habari na utangazaji
pale studio, Rahaleo kijana wa zamani kama mimi au mtu mzima mwenzangu naye
akapata mfadhili sijui kutoka China akamjenga naye kidogo akaniacha mimi
vilevile kama nilivyo. Mara nikasikia Msikiti Mkuu wa Ijumaa Masjid Mushawwar
umejengwa Mwembeshauri nikadhani labda na mimi nitakumbukwa, wapi!
Nilipokumbukwa nikaambiwa sasa nitakuwa sehemu ya kuoshea magari (
car wash), Mara nikaambiwa ile Sheli ya zamani ya mabasi sasa tutaigeuza Sheli
kamili ya mafuta. Yote haya yanafanyika sijasikitika lakini nkaungulika maana
mimi nilipojengwa nilikuwa kituo cha mabasi sikuwa hayo mengine ninayoletewa tu
kwa sababu ya kuwepo kwangu hapo. Lakini nifanyeje na mimi pale nimewekwa tu
maskini wa Mungu mie.
Hivi majuzi nimesikia shaghalabaghala ya kuhamishwa kituo kikuu cha
Daladala Darajani na kuanzishwa vituo vidogo vidogo, Malindi, Donge na
Mnazimmoja jirani na baraza la wawakilishi la zamani ndipo nikapata na mshangao
mbona mimi nipo?
Nimenyamaza siku nyingi lakini sasa itanibidi niseme maana sijisifu
lakini nnaamini ninazo sababu za kuwa kituo kikuu cha Daladala.
Nipo sehemu ya kiistrateji nzuri kwani barabara zote zinazoingia
mjini zinaweza kunifikia hapo kiurahisi bila usumbufu wala msongamano tofauti
na Darajani ambapo msongamano unakuwa mkubwa kwa kuwepo Barabara moja tu
inayofikia stendi kuu.
Wa Bububu na wanaotokea nji hiyo watafikia wakitokea Kinazini. Wa
Amani na wanaotokea njia hiyo akina wa Daraja Bovu watafika wakitokea Mwembeladu. Wa Fuoni pamoja na wa Kwarara,
Nyarugusu, Chuo watafikia wakitokea Posta. Wa Uwanja wa ndege, Chukwani na
Kisauni na Jan’gombe watafikia wakitokea Miembeni. Na wanaotoka mjini watafikia
wakitokea Rahaleo. Umenipata hapo? Niambie nani mwengine ana sifa kama zangu?
Kweli nnaweza kuwa na udhaifu wangu kwamba Hawa wanaotaka kwenda
Hospitali nitawafanya nini nao ndio muhimu?. Ngoja niwaambie Nitawaomba wenye kupanga
njia (Route) waniandalie Ruti mpya ya town tu itakayoanza Kijangwani, ipitie
Mwembeladu, Kinazini, Mlandege, Malindi, Darajani, Hospitali, Michenzani na
Kurudi Kijangwani (Problem solved). Ila mwananchi kidogo itambidi apande,
wakati mwengine Daladala zaidi ya moja.
Pia kitu chengine nnachoringia ni kwamba miundo mbinu kwa ajili ya
kazi hii tayari ninayo, nitahitaji kuboreshwa tu kidogo kwe kutolewa Barabara
zitakazoniunganisha na Barabara kuu zilizopo. Nitaweza kuwa na sehemu kubwa ya
kuegesha magari ya daladala na kukidhi mahitaji ya Magari yaliyopo kama
nitapata mtaalamu mzuri wa kunishughulikia. Nnaringia bara ya Kinazini hadi
Kariakoo ambayo ni njia nne (dual carriageway) ahsante Mzee wetu Karume
alipoona mbali.
Pili Mji tayari umekuwa kwa kiasi kikubwa na wakaazi wengi hawaishi
sehemu za mijini bali wako sehemu nje ya miji na hivyo huduma nyingi sasa
zimeweza kusambazwa sehemu tofauti.
Hata hivyo itabidi wauza mbao pale wanisamehe kwa kuondoka na
kutafuta sehemu nyengine (nitawaomba radhi kama nimewaudhi) kama nikipata dili
( deal) pamoja na kiwanja cha Komba wapya kama wataweza kunisaidia na kujiunga
nami katika mkakati wangu huu wa kudai haki yangu ya asili ya kuwa ni kituo cha
Mabasi au daladala basi tutaendelea kuwa pamoja.
Ila sitokubali kirahisi kwamba nigeuzwe kituo tu bila ya kuletewa
plan yenye kukidhi mahitajio yangu maana wakati mwengine kizuri hujiuza ati! Si unaona hapo juu kwenye picha ya hicho kinachoitwa kituo kipya cha Daladala kilivyo? Hata barabara hakina Je siku za mvua na magari ingia toka patakuwaje?
Nnasema hivi kwasababu pia, ingawa si vizuri kusema, lakini nnaona
choyo kwamba jirani yangu pale mtoto wa juzi tu 1976, kiwanja cha kufurahisha
watoto Kariakoo tayari kimepata mfadhili wa kukiboresha tena kuwa cha kisasa na
kileo pamoja na maduka kadha wa kadha ( ZSSF). Je mimi wa mwaka 1947!? Hata
hivyo hapahajaribika kitu, nami nikiwepo
karibu pale basi tutasaidiana yeye atafurahisha watoto na mimi nitawaleta
karibu, kweli kufa kufaana.
Na nikunon’goneze , nimesikia pale Michenzani nako pamajuzi juzi tu
panataka kugeuzwa kuwa kituo cha kikuu cha biashara na kuna jimnara linajengwa
kuadhimisha miaka 50 ya mapinduzi. Basi kama wangelinifikiria na mimi hasa kwa
kuwepo karibu na kituo hicho nitawaletea wateja kede kede kutoka kila kona ya
mji wetu.
Basi nnawakumbusha tu mbona bado nipo msihangaike au hamjaijua thamani yangu bado? Kama
mnatafuta muarubaini wa Stendi kuu ya Daladala njooni tuzungumze nnawaahidi
sitowaangusha .
No comments:
Post a Comment